Sunday, June 18, 2017

UTHAMINI MOYO WAKO, KAA MBALI NA MAUMIVU

HAKUNA ubishi kuwa mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu, ipo dhahiri kwamba mapenzi yanaweza kuleta furaha maishani mwako lakini wakati huohuo  maumivu, mateso na karaha.

Watu wengi bado wanalizwa na mapenzi na hii ni kwa sababu hawafuati kanuni sahihi za mapenzi. Ndiyo… mapenzi yana kanuni zake.

Kwa bahati mbaya kabisa, kwa sasa mapenzi yamegeuzwa na kuwa kama kitu cha kujaribu au kufanyia biashara ndiyo maana yanawatesa wengi.

Lakini ni kwa nini mapenzi yaendelee kututesa?  Au ni kwa sababu hatujui maana halisi ya mapenzi? Hebu tuyaangalie mapenzi kwa jicho la tatu, kisha tuchukue hatua.

MAPENZI NI NINI?
Katika hali ya kawaida, mapenzi hayaelezeki kuwa ni nini. Ni vigumu sana mtu kukueleza maana ya mapenzi ndiyo maana kila mtu ana uelewa tofauti juu ya suala hilo.

Saturday, June 17, 2017

MANGULA AWATAKA WAPINZANI KUACHA KUDANDIA TRENI KWA MBELE SAKATA LA MCHANGA WA MADINI

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara, Philip Mangula amesema kitendo alichokifanya Rais John Magufuli cha kuwafichua wanaotorosha mchanga wa madini kipo kwenye ilani ya chama hicho hivyo wapinzani waache kudandia treni kwa mbele.

Mangula amesema hayo leo (Jumamosi) wakati akizungumza na wanachama wa CCM kwenye kongamano la kuunga mkono juhudi za Rais na kumpongeza kwa kuwafichua mafisadi lililoandaliwa na wanachama hao.

"Alichokifanya Rais kipo ndani ya ilani ya chama, wapo wanaotaka kudandia treni kwa mbele wakidai wao ndiyo walikuwa na mawazo hayo, nataka niwaambie Rais anatekeleza ilani hiyo ni mipanngo ya CCM, "amesema.

Pia, Mangula amewaonya watu wanaoibuka na kutaka kukwamisha kazi anayofanya Magufuli kuwa hawataweza na nchi haitashtakiwa kama wanavyodai.

“Niwatoe hofu wananchi na wanachama wote kuwa nchi iko salama zaidi tumuunge mkono Rais wetu kuwafichua wezi wa mali za nchi, "amesema

MTANZANIA ATUPWA JELA UINGEREZA KWA KOSA LA KUPOST PICHA ZA MAREHEMU FACEBOOK

Mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa ni Mtanzania amehukumiwa kifungo cha miezi mitatu jela nchini Uingereza kwa kosa la kurusha katika ukurasa wake wa Facebook, picha za mtu aliyefariki dunia kutokana na moto uliounguza jengo la ghorofa la Mnara wa Grenfell lililopo nchini humo.

Pia, mtu huyo ametakiwa kulipa faini ya Sh579,880 kwa mwathirika wa tukio hilo.

Mtanzania huyo, Omega Mwaikambo (43) alituma video na picha za mwili wa marehemu uliokuwa kwenye begi  na baadaye picha nyingine tano zikionyesha uso wa  marehemu huyo.

Friday, June 16, 2017

HII NDIO NDEGE BINAFSI ALIYOKUJA NAYO MWENYEKITI WA KAMPUNI YA BARRICK GOLD CORPORATION KWAAJILI YA KUJA KUFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS MAGUFULI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na  Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

WANAFUNZI 56 WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO 207 WABADILISHIWA SHULE

Taarifa kutoka ofisi ya Rais-TAMISEMI imeonyesha mabadiliko ya kuwapangia shule wanafunzi 56 waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano katika Shule ya Sekondari Madibira Tahasusi ya PCB na kuwapeleka katika shule zingine zenye tahasusi (Combination) hiyo ndani ya Mkoa wa Mbeya na Mikoa ya jirani. Mabadiliko haya ni kwa sababu maalum.

Aidha, wanafunzi wapya 56 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha Tano katika shule ya Sekondari Madibira Tahasusi ya CBG kama inavyoonekana kwenye tovuti. Wanafunzi hawa wanapaswa kuripoti katika shule walizopangiwa tarehe 17 Julai, 2017. 
TAARIFA KWA UMMA (15-06-2017)

 Tafadhali bofya chini Kujua Orodha ya Wanafunzi waliochaguliwa na Waliobadilishwa kidato cha 5 kwa sababu maalum.

Wednesday, June 14, 2017

USHAHIDI WA KESI YA WEMA WAKWAMA KUTOLEWA

Kesi ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Wema Sepetu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirishwa hadi Julai 10.

Wema ambaye ni mshindi wa taji la urembo, maarufu Miss Tanzania kwa mwaka 2006 na msanii wa filamu, anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kutumia na kupatikana na bangi.

Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa alisema kesi ilipangwa leo (Jumatano) kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka lakini Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba anayeisikiliza kesi hiyo yupo likizo.

Kutokana na hilo, aliomba iahirishwe hadi Julai 10 ombi lililokubaliwa na mahakama. Wema na wenzake Angelina Msigwa na Matrida Abbas wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na dawa za kulevya na kutumia dawa hizo.

Inadaiwa Februari 4, katika makazi ya Wema, Kunduchi Ununio, walikamatwa wakiwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08. Wema pia anadaiwa Februari Mosi katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam alitumia bangi.

MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA ACACIA, WAKUBALI KULIPA FEDHA WANAZODAIWA NA PIA KUSAIDIA UJENZI WA MTAMBO WA KUCHENJULIA DHAHABU NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika picha ya pamoja na  Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton pamoja na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiagana Mhe. Ian Myles balozi wa Canada Nchini pamoja na  Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton alipofoika ikulu kwa mazungumzo juni 14,2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na  Mwenyekiti wa Barrick  Gold Corporation  Profesa John L. Thornton baada ya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es salaam  Juni 14, 2017. wakiwa na  Waziri wa Sheria na Katiba Profesa Palamagamba Kabudi na Balozi wa Canada nchini Mhe. Ian Myles.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ni mmiliki mkubwa wa kampuni ya Acacia Mining Limited Prof. John L. Thornton na kukubaliana kuwa kampuni hiyo ipo tayari kufanya mazungumzo na Serikali ya Tanzania ili kulipa fedha ambazo Tanzania imezipoteza kutokana na kampuni hiyo kuendesha shughuli zake hapa nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano Ikulu ni kwamba, Prof. John L. Thornton ambaye amesafiri kwa ndege binafsi kutoka nchini Canada hadi Tanzania amekutana na Mhe. Rais Magufuli leo Juni 14, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam na mazungumzo yao yamehudhuriwa na Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles na Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Tuesday, June 13, 2017

LISSU AMGEUKIA KIKWETE ATAKA NAE AJUMUISHWE KWENYE ORODHA YA WASHTAKIWA WA MAKINIKIA.

Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu ameipa changamoto Serikali kwa kuitaka kumuingiza Jakaya Kikwete katika orodha ya watuhumiwa wa sakata la makinikia.

Akichangia bungeni leo Jumanne, katika hotuba ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18, Lissu amesema kuwa wakati wa kusaini mikataba ya madini Kikwete alikuwa ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini.

“Katika taarifa hii ya jana wamependekeza watu fulani fulani washtakiwe makamishna, mwanasheria mkuu, Andrew Chenge (Mbunge wa Bariadi), Wiliam Ngeleja (Sengerema) jamani naombeni niwaambie kitu ili  wabunge muwe na maarifa,” amesema na kuongeza:

“Mtu wa kwanza kusaini mikataba na leseni za madini alikuwa ni Meja Jakaya Mrisho Kikwete, Agosti 5 mwaka 1994 alisaini leseni ya Bulyankulu inayopingwa leo hii wakati akiwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini wakati huo hakuwa na kinga ya urais.”

Amesema wakati aliposaini leseni na mikataba hiyo alikuwa hana kinga kwa masuala ambayo aliyafanya.

“Rais (Kikwete) alisaini si ya Bulyankulu pekee ya Nzega, ya Geita hizo leseni zina saini ya Kikwete anaponaje kwa mapendekezo haya? Anaponaje kama kweli mnataka kuwashughulikia watu walioshiriki kwenye mambo haya?” amehoji.

“Mbona mnachagua chagua hizi? Leseni na hizi sheria tangu mwaka 1999 tumesema tatizo kubwa ni sheria.”

Amemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kama anataka kukumbukwa wakati wa uongozi wake basi asikubali kupitisha miswada ya sheria kwa hati ya dharura.

Akijibu swali hilo, Ndugai amesema atairuhusu miswada hiyo ya madini na gesi iingie bungeni kwa hati ya dharura.

“Kwanza wanaoamua siyo mimi tu ni kamati ya uongozi ya Bunge, lakini kama itakuja kwa hati ya dharura hii (madini) itaruhusiwa kwasababu moja tu tunaibiwa sana.” amesema.

Wednesday, June 07, 2017

SHILOLE: WATOTO WANGU HAWATAIGA MAISHA YANGU


MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, amesema kwamba watoto wake hawataiga maisha wala mavazi anayovaa kwenye shoo zake wala maisha ya sanaa anayoishi kwa kuwa wanatambua yupo kazini kwa ajili yao.

Shilole akiongea na mwandishi wa habari hii alisema kwamba, malezi anayowalea watoto wake ni tofauti na maisha anayoishi yeye na watoto hao wanatambua kwamba mama yao ni msanii hivyo hawataiga anachofanya.

 “Watoto wangu nawalea katika maadili kama mama, siwezi kuwalea maisha ya kistaa kama ninavyoishi mimi na wanatambua kwamba mama yao nipo kazini kwa ajili yao na pia hawana ndoto za kuishi maisha yangu ya kisanii,” alieleza Shilole.

Shilole aliongeza kwamba licha ya kulea watoto wake kwa maadili ya dini, lakini hataacha kuendelea kuwapa elimu, mafunzo ya maisha na biashara.

HUDDAH: SITAKI KUOLEWA

MWANAMITINDO maarufu nchini Kenya, Huddah Monroe, amefunguka na kusema kwamba hana mpango wa kuolewa katika maisha yake.

Mrembo huyo ambaye hakauki mitandaoni, amekuwa akihusishwa kutoka na nyota wa soka wa timu ya Taifa ya Kenya na klabu ya Tottenham ya nchini England, Victor Wanyama, lakini amekuwa akikana taarifa hizo na sasa ametangaza kwamba hana mpango wa kuolewa kwenye maisha yake.

“Kila mtu ana mipango yake, hivyo kwa upande wangu sina mpango wowote wa kuolewa. Hata hivyo, kama itakuja kutokea nikaolewa hatakuwa mwanamume wa Nigeria.

“Maana kuna taarifa kwamba natoka na Wizkid, sikushangaa sana kwa kuwa niliwahi kuposti picha nikiwa na msanii huyo nilipokutana naye nchini Marekani, picha hizo zikaleta maneno mengi nina uhusiano naye wa kimapenzi hakuna ukweli na sitaolewa na mwanamume wa Nigeria,” alisema Huddah.

ACT WAZARENDO WAMVUA CHEO MAMA MGHWIRA

Chama cha ACT Wazalendo kimmevua uongozi aliyekuwa mwenyekiti wake, Anna Mgwhira ambaye ameteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Chama hicho kimefikia hatua hiyo kwa kuzingatia ibara ya 17 ya katiba yake ambayo inatamka kuwa kiongozi wa chama atakoma kuendelea na madaraka yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba alisema kamati ya uongozi wa ACT ulikutana leo lengo kuu ni kutafakari lililotokea kuona namna gani Mgwhira anaweza kutimiza majukumu yake kama Mwenyekiti na Mkuu wa Mkoa.

“Kama chama baada ya kutafakari kwa kina na baada ya mashauriano baina yake na viongozi kutumia katiba ya chama anakoma kuwa kiongozi kwa kuwa kutakuwa na mgongano wa majukumu, maslahi hivyo anakoma kuwa mwenyekiti,” alisema Mwigamba.

Mwigamba alisema kamati ya chama imemchagua Yeremia Maganja kuwa  Kaimu Mwenyekiti na kamati ilimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Mgwhira.

Hata hivyo, Mwigamba alisema Mghwira bado ataendelea kuwa mwanachama halali wa chama hicho.

Saturday, June 03, 2017

WEMA SEPETU ABADILISHIWA HATI YA MASHTAKA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeanza kusikiliza kesi inayomkabili msanii wa filamu, Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili, huku upande wa mashtaka ukiiomba mahakama hiyo kubadili hati ya mashtaka.

Akiwasilisha hoja hiyo juzi mbele ya Hakimu Thomas Simba, Mawakili upande wa jamhuri, Constantine Kakula na Paulina Fungameza, walianza kuwasomea  upya mashtaka washtakiwa hao ambao ni Wema Sepetu na wafanyakazi wake wawili, Angelina Msigwa na Matrida Abas.

Alidai shtaka la kwanza linalowakabili watuhumiwa hao ni pamoja na kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya ambapo mnamo Februari 4, mwaka huu katika maeneo ya Kunduchi Ununio, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kukutwa na msokoto mmoja na vipisi vya dawa za kulevya aina ya bangi yenye gramu 1.08.

MNYIKA ATOLEWA NJE YA BUNGE KWA AMRI YA SPIKA

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika ametolewa nje ya Bunge jana Ijumaa kwa agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Licha ya adhabu hiyo, amemzuia kutohudhuria vikao vya Bunge kwa siku saba kuanzia hiyo jana.

Mnyika ametolewa baada ya mmoja wa wabunge kusema 'Mnyika mwizi' akimhusisha na wizi wa madini, hoja inayochangiwa na wengi kwenye mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini unaoendelea.

Kutokana na hali hiyo Mnyika alimtaka Spika kuchukua hatua kwa mbunge aliyesema kuwa yeye ni mwizi lakini Spika akasema hajui hilo na haijaingia kwenye hansadi. Hata hivyo Mnyika alisisitiza kuwa mambo hayaweze kwenda hivyo.

Baada ya majibizano kati yake na Spika, Spika akaamuru walinzi wamtoe Mnyika nje ya Bunge na asihudhurie vikao saba vinavyofuata.

Mnyika alikuwa akitoa maelezo baada ya Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde kusema upinzani wa Tanzania ni wa ajabu kwani unatetea wezi wa madini.

Saturday, May 27, 2017

JAMBO TZ INAWATAKIA KHERI NA SWAUM NJEMA WAISLAMU WOTE DUNIANI


MAMBO YANAYOPENDEZA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI


Allah (Subhaanahu wa Ta’ala)  alipanga kuwa mwaka uwe na miezi kumi na mbili, na katika hiyo akaichagua baadhi akaitukuza na kuifadhilisha zaidi ya mengine.

Mwenyezi Mungu anasema;

“Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni miezi kumi na mbili kati ya hiyo mna mine iliyo mitukufu."

Nayo ni (Dhulqaada, Dhulhijja, Muharram, na Rajab).

Baada Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuifadhilisha miezi hii minne akaufadhilisha vile vile zaidi kuliko hata miezi hii minne mwezi tuliyo ndani yake nao ni mwezi wa Ramadhani, usiku wa cheo (Laylatul Qadr), katika mwezi huu, tokeo kubwa ni kuteremshwa kwa Qurani.

Kwa ilivyokuwa mwezi huu ndio bora wa miezi yote, hivyo basi mema yafanywayo ndani yake yanakuwa ni bora na yanalipwa ziada kuliko miezi mengine. Hivyo basi inatakiwa kwa muislam kujibidiisha katika kufanya mema na kuepuka  mabaya hasa awapo katika mwezi huu mtukufu. Baadhi ya mambo tutakiwayo kuyatekeleza:

1. Kusoma Qurani

 Amesema Allah (Subhaanahu wa Ta’ala);

“Mwezi wa Ramadhani ambayo imeteremshwa ndani yake Qur-an hali ya kuwa ni uongofu kwa watu …………"

Friday, May 26, 2017

MAJERUHI WAWILI WA LUCKY VICENT WARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALI

Watoto wawili majeruhi wa ajali ya gari la Shule ya Lucky Vincent wameruhusiwa kutoka hopitalini.

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa watoto hao, Sadia Ismael na Wilson Tarimo waliokuwa wamelazwa katika hospitali ya Mercy ya Marekani wameruhusiwa na sasa wapo katika makazi mapya.

“Watoto Sadia na Wilson waruhusiwa rasmi kutoka hospitali ya Mercy  na wanaelekea kwenye makazi yao mapya mjini Sioux City IA. Mungu azidi kuwaangazia nuru ya uso wake. Amani iwe nawe na Nesi wetu mpendwa kwa huduma kubwa mmefanya kwa watoto hawa na Tanzania,”ameandika Nyalandu.

Jana Nyalandu aliandika kuwa mtoto Doreen ataendelea kuwepo hospitali katika wodi ya watoto akiendelea kupata huduma za karibu hadi itakapoamuliwa vinginevyo.

MTOTO ALIYEISHI KWA KULA MAFUTA ATAMANI KUWA DAKTARI BINGWA

MTOTO Shukuru Kisonga (16) ambaye ameishi muda mrefu kwa kula sukari robo tatu, mafuta ya kula lita moja na maziwa lita tatu, amesema ndoto yake ni kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya damu.

Shukuru alisema hayo jana alipozungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu maendeleo ya afya yake na kuongeza kuwa ataongeza juhudi katika masomo yake afikie ndoto yake hiyo.

"Niliteseka muda mrefu, namshukuru Mungu sasa sijambo naendelea na matibabu wodini, nikiruhusiwa kurejea nyumbani nitaongeza juhudi katika masomo yangu nitimize ndoto yangu ya kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya damu, " alisema.

Shukuru alisema anataka kuwa daktari bingwa wa magonjwa ya damu   awasaidie watu wengi hasa wanaoteseka na ugonjwa kama unaomsumbua yeye.

" Namshukuru daktari wangu hapa Hospitali ya Taifa Muhimbili, amenisaidia mno ndiyo maana na mimi ninataka kuwa kama yeye   niweze kuwasaidia wengine wanaougua Mungu akinijalia, " alisema.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya damu, Stella Rwezaula, juzi alisema mtoto huyo anaugua selimundu, ugonjwa ambao amezaliwa nao baada ya kurithi vinasaba kutoka kwa wazazi wake.

Thursday, May 25, 2017

RIPOTI YA MCHANGA YAONESHA NCHI ILIVYOLIWA

 Kamati maalumu iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza mchanga wa madini, imebaini kwamba makontena 277 yaliyozuiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam yana tani 7.8 za dhahabu yenye thamani ya kati ya Sh676 bilioni na Sh1.147 trilioni.

Rais John Magufuli akizungumza awali alisema kiwango cha juu kinaweza kufika tani 15.5.

Kiwango hicho ni tofauti na kile ambacho kamati hiyo ilielezwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), kwamba makontena hayo yalikuwa na tani 1.1 za dhahabu yenye thamani ya Sh97.5 bilioni.

Kutokana na tofauti iliyopo kati ya taarifa ya TMAA na hali halisi, kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe wanane imebaini kwamba Taifa limekuwa likiibiwa kupitia usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia).

Akitoa muhtasari wa kamati hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kumkabidhi Rais Magufuli ripoti ya uchunguzi, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma alisema kamati yake ilipewa hadidu za rejea ambazo ziliwaongoza katika uchunguzi wao ambazo alizitaja kuwa ni kuchunguza makinikia yaliyopo kwenye Bandari ya Dar es Salaam, bandari kavu na migodini kwa kupekua na kubaini vilivyo ndani. Pia, kufanya uchunguzi wa kimaabara kujua aina, kiasi na viwango vya madini vinavyoonekana kwenye makinikia.

ZARI WA DIAMOND ATHIBITISHA KIFO CHA MUMEWE WA ZAMANI

Zarinah Hassan ‘ZariTheBossLady’ amethibitisha taarifa za kifo cha aliyekuwa mpenzi na baba wa watoto wake watatu, Ivan Semwanga.

Zari ametoa taarifa hzo kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram kwa kuandika,” God loves those that are special and that’s exactly who you were & I guess that’s why he wanted you to himself. You have touched and helped thousands, you did wonders and I remember you telling me “life is too short let me live it to the fullest”, this very dark hour it makes sense why you always said those words to me. To your sons, you were a hero-some kind of superman. Anyone who has ever been in your presence knows what a charming person you were. You will be missed and remembered in so many ways. You were IVAN THE GREAT! Rest in peace DON”

Kwa Kiswahili, “Mungu anawapenda wale walio muhimu na hakika ndivyo ilivyokuwa kwako, nadhani hiyo ndiyo sababu ya yeye kukuhitaji kwake. Umewagusa na kuwasaidia maelfu, ulifanya maajabu na ninakumbuka ulinambia ”maisha ni mafupi sana acha niishi kwa ukamilifu”, muda huu wenye giza ndiyo inaleta maana kwanini ulisema maneno hayo kwangu. Kwa watoto wako ulikuwa shujaa. Kila mtu aliyekuwepo sehemu ulipokuwa alijua kwa kiasi gani wewe ni mcheshi. Nitakukumbuka kwa namna nyingi. Ulikuwa IVAN THE GREAT. Pumzika kwa amani DON”

Kabla ya taarifa hiyo kulikuwa na taarifa nyingi zikisema kuwa Iavn amefariki lakini Zari alikuwa akikanusha, na taarifa za uhakika akizitoa Zari mwenyewe ambaye wamezaa watoto watatu wote wakiwa wa kiume alfajiri ya alhamisi ya Mei, 25.

RAIS WA FIFA AIPONGEZA YANGA KWA KUSHINDA UBINGWA WA VPL 2016/2017

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino ametuma salamu za pongezi kwa uongozi, wachezaji na mashabiki klabu ya Yanga kwa kuibuka washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2016/2017.

Salamu za Infantino zimetumwa kwa Yanga kupitia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na kuwa pamoja na kuwapongeza kwa ushindi walioupata pia anaitakia kila la kheri Yanga katika michuano iliyopo mbele yake.

Wednesday, May 24, 2017

MBUNGE MSUKUMA AOMBA BUNGE KUCHANGIA RAMBIRAMBI KWA WANAFUNZI WALIOFARIKI GEITA, WABUNGE WENGINE WAZOMEA....!!!

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, ameomba mwongozo akiliomba Bunge liangalie namna ya kuchangia rambirambi kwa wanafunzi watatu waliofariki kwa kuzama Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, Bunge hilo limekuwa na utamaduni wa kuchangia maafa na majanga mbalimbali na kutolea mfano wa ajali iliyoua ya shule ya msingi ya Lucky Vicent Jijini Arusha.

Katika ajali hiyo, wanafunzi 32 walifariki dunia pamoja na watu wengine watatu ambapo wabunge walichanga rambirambi inayofikia Sh86 milioni ambapo ofisi ya Bunge ilichanga Sh14 milioni.

Hata hivyo, wakati Mbunge huyo akiwasilisha mwongozo huo, baadhi ya wabunge wa upinzani walionekana kupaza sauti yao, hadi mwenyekiti Zungu alipolazimika kukemea hali hiyo.

Zungu akitoa mwongozo wake, alisema ni utamaduni wa chombo hicho kuchangia maafa na majanga mbalimbali kama njia za kuonyesha mshikamano na kwamba hilo analichukua atalitolea majibu baadae.

ANGALIA MAJINA YA VIJANA WALIOHITIMU KIDATOCHA SITA WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUZO YA JKT KWA MUJIBU WA SHERIA MWAKA 2017

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), limechagua vijana waliohitimu Elimu ya Sekondari Kidato cha Sita kwa mwaka 2017, kutoka Shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria.

Sanjari na Uchanguzi huo, JKT limewapangia Makambi watakayokwenda kupatiwa mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na wanatakiwa kuripoti Makambini kuanzia tarehe 25 – 30 Mei 2017.

Vijana waliochanguliwa, wamepangiwa katika kambi za JKT Rwamkoma – Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Makutopora – Dodoma, JKT Mafinga – Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga, JKT Makuyuni – Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma.

Aidha, wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) wanatakiwa kuripoti kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

JKT linawataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa vifuatavyo:

Bukta ya rangi ya ‘Dark blue’ yenye mpira kiunoni (lastic), iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini, isiyo na zipu.

Raba za michezo zenye rangi ya kijani au blue.

    Shuka mbili za kulalia zenye rangi ya blue bahari

    Soksi ndefu za rangi nyeusi.

    Nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa mikoa yenye baridi.

    Track suit ya rangi ya kijani au blue.

    Nauli ya kwenda makambini na kurudi majumbani.

Mkuu wa JKT anawakaribisha Vijana wote waliochaguliwa ili waweze kujiunga na Vijana wenzao katika kujifunza Uzalendo, Umoja wa Kitaifa, Stadi za kazi, Stadi za maisha na Utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa letu.

Tuesday, May 23, 2017

HUYU NDIYE MWANAFUNZI ALIETUMIA UZOEFU WA KUOGELEA KUWAOKOA WENZIE WASIFE MAJI, GEITA.

Mwanafunzi Tisekwa Gamungu wa shule ya msingi Butwa wilayani Geita, aliyetumia uzoefu wake wa kuogelea kuokoa wenzake tisa baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kupinduka jana jioni. Wanafuzni watatu wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyohusisha mtumbwi uliokuwa umewabeba wanafunzi 12.

MIILI YA WANAFUNZI WATATU WALIOZAMA NA MTUMBWI GEITA YAPATIKANA

Wanafunzi watatu kati ya 24 wa shule ya msingi Butwa, waliozama katika ziwa Victoria, kisiwa cha Butwa, wamefariki dunia.

 Awali wanafunzi 21 waliokolewa na watatu hawakuonekana lakini saa chache baadaye, miili mitatu iliopolewa. Ajali hiyo ilitokea jana saa 10 alasiri.

 Mkuu wa Wilaya ya  Geita, Herman Kapufi amesema wanafunzi hao walikuwa kwenye mtumbwi waliotumia kuvuka wakitoka shuleni.

YUSUF MANJI AJIUZULU UENYEKITI YANGA.....!!!

Barua iliyosainiwa na Yusuf Manji Mei 22, 2017 inaonesha kwamba Manji ameachia rasmi nasasi ya uenyekiti wa klabu ya Yanga na makamu mwenyetiki wa klabu hiyo Clement Sanga atakuwa mwenyekiti na kuiongoza klabu hadi hapo uchaguzi utakapofanyika ili kumpata mwenyekiti mpya.

Kwa mujibu wa maelezo ya barua, Manji alifikia uamuzi wa kujiuzulu Mei 20 mwaka huu siku ambayo Yanga ilitangazwa kuwa bingwa wa ligi kuu Tanzania bara 2016/2017.

Katika barua hiyo, Manji amsema ameamua kuachia ngazi ili kutoa nafasi kwa wengine nao kushika uongozi ndani ya klabu hiyo.

Friday, May 19, 2017

UPASUAJI WA MAJERUHI WA AJALI ARUSHA WAFANIKIWA

 Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu anaandika katika ukurasa wake wa factbook kuwa, "Mtoto Doreen amemaliza kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo, kwa kile ambacho madaktari wamesema kumefanikiwa kwa ufanisi mkubwa, kupita matarajio yao." 

Nyalandu anaeleza zaidi, "Mtoto Doreen alikuwa afanyiwe upasuaji kwa makadrio ya saa 5:30, lakini zoezi hilo lilikamilika kwa muda wa saa 4:00, Huku timu ya "Surgical Support" ikiwa na watu 6 na kwa pamoja wakiongozwa na madaktari bingwa 2, Dk Meyer na Dk Durward."

"Mtoto Doreen amehamishwa kutoka chumba cha upasuaji na kupekewa ICU, na madaktari wamesema kwa kuwa hali yake imeridhisha sana, baadaye leo watamtoa ICU ambako wamempumzisha baada ya upasuaji na kumrudisha wodi yawatoto ambako ataendelea na mapumziko."

DR. SLAA: SINA MPANGO WA KURUDI TANZANIA

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dr. Willibrod Slaa, amesema hana mpango wa kurudi nchini kwa sasa na kwamba taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii hazina ukweli wowote.

Jana katika mitandao mbalimbali ya kijamii ilisambaa taarifa kwamba mwanasiasa huyo ambaye aliondoka nchini baada ya kujiweka kando na chama chake wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, angewasili leo nchini.

“Dk. Slaa ataingia kesho (leo) nchini na kwamba atazungumza na waandishi wa habari saa tano asubuhi,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kutokana na hilo, mwandishi wa habari hii alimtafuta Dr. Slaa kupitia simu yake ya kiganjani akiwa nchini Canada jana, ambapo alieleza kushangazwa na taarifa hizo akisema watu wakikosa ajenda hubaki kutunga mambo.

Thursday, May 18, 2017

SERENGETI BOYS YAWASHIKISHA ADABU WAANGOLA KATIKA MICHUANO YA AFCON U17

Serengeti Boys imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya AFCON U17 baada ya kuifunga Angola kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kundi B uliochezwa jioni ya leo Alhamisi Mei 18, 2017.

Vijana wa Serengeti Boys ndio walikua wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya sita kipindi cha kwanza baada ya Kelvin Naftal kupasia kamba kwa kichwa akiunganisha krosi ya Nickson Kibabage.

Dakika ya 18 Angola walisawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro baada ya kutumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Serengeti Boys na kufanya timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare kwa kufungana 1-1.

Kipindi cha pili Serengeti waliongeza kasi kutafuta bao na kufanikiwa kufunga dakika ya 69 mfungaji akiwa ni Abdul Suleiman baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Yohana Mkomola. Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania.

SHILOLE AWATAJA DIAMOND, ZALI KWENYE KESI YAKE

 
MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ameieleza mahakama jinsi mwanafunzi wa Chuo cha Bandari, Thomas Lukas, alivyokuwa akitumia mtandao wa kijamii wa Instagram kutuma meseji za matusi ya nguoni kwa watu mbalimbali.

Shilole alitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni mbele ya Hakimu, Boniface Lihamwike.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Tumaini Mfikwa, Shilole alidai shughuli zake ni muziki na anatambulika kwa jina la Shilole ama Shishi baby.

Shilole: Mheshimiwa mimi nafanya kazi sehemu nyingi hasa kwenye Instagram, WhatsApp, Facebook na Twitter…, nipo kwenye mitandao hiyo tangu nilipokuwa superstar miaka mitano iliyopita.

Alieleza Shilole huku akidai kwamba mwaka jana alipokea simu za watu tofauti wakiwemo wasanii wenzake na mashabiki wake wakimlalamikia kuhusu meseji za matusi anazowatumia kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Shilole: Yaani mimi kama mwanamke nilidhalilishwa sana na hayo matusi, mheshimiwa Hakimu ukitaka nayataja hapa.
Hakimu: Subiri…
Shilole: Ndipo nikaamua kwenda kituo cha Polisi Osterbay kuonyesha jinsi mtuhumiwa alivyotumia jina langu vibaya.

Hata hivyo, alipotakiwa na Wakili wa utetezi, Julias Kamote na Christina Roman ataje baadhi ya majina ya wasanii waliomlalamikia, aliwataja kwamba ni Queen Darlin, Diamond, Zali, Ant Ezekiel na Harmonize mwingine ni mtangazaji, Efrahim Kibonde.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 6, mwaka huu na mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana.

TRUMP AIMWAGIA TANZANIA FEDHA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI

Serikali ya Marekani kupitia mpango wa dharura wa Rais wa nchi hiyo wa kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), umeidhinisha Dola 526 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kwa ajili ya kukabiliana na VVU na Ukimwi nchini.

Msaada huu utaongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa matibabu ya kufubaza VVU kufikia milioni 1.2.

Pia utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini imesema fedha hizo zitafadhili miradi inayotekelezwa chini mpango wa utekelezaji wa  Pepfar utakaoanza kutekelezwa Oktoba hadi Septemba 2018, na ni ongezeko la asilimia 12.3 ya bajeti ya mwaka jana.

Bajeti iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Pepfar pia itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume, walengwa wakiwa 890,000.

Mpango huu unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa mafanikio maambukizi ya VVU.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser alisema, “Kwa pamoja tunafanya kazi ili hatimaye kuwa na kizazi kisicho na Ukimwi Tanzania – ambacho hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma.”

MWILI WA MTOTO ALIEPOTEA, WAKUTWA HAUNA MACHO, ULIMI NA MENO MAWILI

Mtoto Felister Isack Skali (7) pichani, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya msingi Mwagala Mbuyuni Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu mei 11 mwaka huu, mwili wake umekutwa porini ukiwa hauna baadhi ya viungo kama ulimi, macho na meno mawili ya chini.

Akithibitisha kupatikana kwa mwili wa marehemu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Athanas Hamis amesema alipata taarifa kutoka kwa wachungaji wa mifugo ambapo alifika eneo la tukio jioni na wanachi kulazimika kulinda mwili hadi asubuhi walipofika askari Polisi wa kituo cha Galula na Daktari na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kisha mazishi kufanyika jana.

Tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji cha Mbuyuni ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

Friday, May 05, 2017

UPELELEZI ALIYEJITOSA BAHARINI WAKAMILIKA

Wakati Polisi Zanzibar ikisema imekamilisha kumhoji msichana aliyejitosa Bahari ya Hindi eneo la Chumbe alipokuwa akisafiri na boti ya Kilimanjaro (V) kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, mtaalamu anasema binti huyo amethirika kisaikolojia ni bora angeachwa apumzike.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Hassan Nassir Ali alimwambia wa habari hii jana kuwa, msichana huyo anayesoma kidato cha tatu Sekondari ya Glorious na watu wengine wameshahojiwa kuhusu tukio hilo la Aprili 3.

Hassan alisema miongoni mwa walihojiwa ni wanafamilia, msichana huyo na manahodha wa boti ya Kilimanjaro ambao walimuokoa.

Alisema polisi imepata taarifa kamili juu ya tukio hilo, hivyo wakati wowote jalada litafikishwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.

PENGO APELEKWA MAREKANI KWA MATIBABU

ASKOFU wa Kanisa Katoliki  Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amepelekwa nchini Marekani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana na Askofu Msaidizi wa jimbo hilo, Eusebius Nzigilwa alisema Kardinali Pengo alisafirishwa Mei 2, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kufanyiwa uchunguzi.

Alisema Kardinali Pengo, anatarajiwa kuwapo nchini Marekani kwa mwezi mmoja.

“Tuendelee kumuombea Baba Kardinali Pengo ili mwenyezi Mungu amjalie nguvu na afya njema ya mwili na roho ili aweze kuliongoza vema Taifa la Mungu alilokabidhiwa,”alisema  Nzigilwa.

Hivi karibuni, hali ya afya ya Kardinali Pengo, ilionekana kudhoofu kutokana na maradhi yanayomsumbua, kitendo kilichosababisha ashindwe kuongoza misa za ibada kanisani.

Wakati wa misa ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika hivi karibuni, Kardinali Pengo alionekana kudhoofu na kufikia uamuzi wa kukataa kupigwa picha na waandishi wa habari waliohudhuria misa hiyo.

Thursday, April 20, 2017

TFDA YAPOKEA MAOMBI 767 YA VIWANDA VIPYA

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TDFA), Hiiti Sillo amesema kuanzia Machi mwaka huu taasisi yake ilimepokea maombi mapya ya usajili wa viwanda 767.

Amesema katika maombi hayo, viwanda 635 vipya vimesajiliwa kati ya hivyo, 613 vya chakula, kimoja cha dawa na 21 vya vipodozi akisema hiyo ni asilimia 82.8 ya maombi yote jambo linaloashiria kwamba waombaji wengi wanazingatia sheria.

Amesema katika kipindi hicho TFDA ilifanya tathmini ya maombi 4,762 sawa na asilimia 82.1 ya usajili wa bidhaa za dawa, chakula, vifaatiba na vipodozi, kati ya maombi 5,802 yaliyowasilishwa na 4,322 (75%) yaliidhinishwa na 440 yalikataliwa kwa kutokidhi vigezo vya ubora.

Sillo ameeleza hayo leo kwenye mkutano na wahariri wa vyombo vya habari walipokutana mkoani Tabora.

'UPINZANI HAUNINYIMI USINGIZI' MUGABE

Viongozi wawili wa vyama vya upinzani nchini Zimbabwe wamekubaliana kuunda umoja kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao nchini humo.

Kiongozi wa Movement for Democratic, Morgan Tsvangirai na aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo Joice Mujuru wa National people's Party walitia saini makubaliano hayo siku ya Jumatano.

Rais wa nchi hiyo Robert Mugabe awali alitoa maneno ya dhihaka kutokana na mipango ya upinzani aliyodai kuungana kumuondoa madarakani.
Morgan Tsvangirai na Joice Mujuru wameonekana kumaliza baadhi ya tofauti zao.Tsvangirai anasema makubaliano yaliyotiwa saini baina ya vyama viwili ni msingi kuelekea kuunda umoja wa vyama kwa ajili ya kupambana na chama tawala Zanu PF.

Changamoto iliyopo hivi sasa ni kuamua nani kati ya hao wawili ataongoza muungano huo.

Tayari, vyama vingi vidogo vya upinzani vimemuidhinisha Morgan Tsvangirai kuwa mgombea wao wa urais.

Kiongozi wa miaka mingi madarakani Robert Mugabe , alieleza kuwa upinzani umejaa watu wasio na kitu vichwani.

Amesema hakosi usingizi kwa kile kinachoitwa umoja wa wapinzani.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...