WABUNGE WAUNGANISHA NGUVU KUTAKA KUMSULUBU BUNGENI
RIPOTI
ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa mwaka
2006 kuchunguza ujenzi wa maghorofa katika Jiji la Dar es Salaam,
imemweka mahala pabaya na inaweza kumtoa kafara, Waziri Mkuu wa sasa,
Mizengo Pinda, Tanzania Daima Jumatano limedokezwa.
Pinda
anatolewa kafara katika sakata la jengo la ghorofa 16 lililoporomoka
katikati ya Jiji la Dar es Salaam wiki iliyopita na kusababisha vifo
vya zaidi ya watu 40.
Kutokana
na janga hilo, Pinda analalamikiwa kukalia ripoti ya Tume ya Lowassa
ambayo ilikuja na mapendekezo ya kukabiliana na maghorofa yaliyojengwa
chini ya kiwango.
Duru
za siasa kutoka ndani ya Bunge zinasema kuwa tayari kuna baadhi ya
wabunge bila kujali itikadi zao, wameunganisha nguvu kutaka kumsulubu
Waziri Pinda katika mkutano ujao wa Bunge kupitia hoja binafsi au
maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu.
Mmoja
wa mawaziri waandamizi wa serikali ambaye aliomba jina lake
lihifadhiwe, alisema: “Pinda anastahili kubeba mzigo, kwani baada ya
kukabidhiwa ripoti hiyo alimwajibisha nani tangu 2008 hadi sasa?
“Kwa
uzembe huu, Pinda ameshiriki kwa kuwa hakuwawajibisha waliojenga
kinyume na utaratibu hadi Watanzania wengine wakafa. Zamu hii hata
akilia anahusika.” Mbunge wa Vunjo Augustino Mrema (TLP) alimshangaa
Waziri Pinda kwa kushindwa kuchukua hatua zilizopendekezwa na tume ya
Lowassa kwani ilipendekeza baadhi ya majengo yabomolewe na wahusika
wachukuliwe hatua.
Alisema athari ya ukimya huo ni kuendelea kuangamia kwa Watanzania kunakosababishwa na uzembe wa viongozi wa serikali.
“Hili
tatizo la kushindwa kuchukua uamuzi mgumu litaendelea kutugharimu kila
siku, yale maghorofa yaliyotakiwa kubomolewa kipindi kile hayajaguswa
na hayataguswa kwa sababu ya kubebana, hili hatuwezi kulinyamazia,
lazima tukawashe moto bungeni,” alisema Mrema.
Alisema Watanzania hawapo tayari kuletewa danganya toto ya tume nyingine ikalete majibu ambayo tayari yako mezani kwa Pinda.
Mbunge
wa CCM aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema kitendo cha Jeshi la
Polisi kuwakamata watendaji wa Manispaa ya Ilala hakitoshi kama Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
ataendelea kubaki ofisini.
Mrema
ambaye amepata kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa
nyakati tofauti, alisisitiza kuwa Waziri Tibaijuka anapaswa aige mfano
wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Lowassa walioamua kuachia ngazi
kutokana na uzembe wa watendaji wao.
“Kwa
wenzetu leo inapotokea boti ikazama kwa uzembe na kupoteza maisha ya
watu watatu waziri mwenye dhamana anawajibika, iweje sisi leo
tuwachekee mawaziri wetu?” alihoji mbunge huyo.
Mbunge wa kuteuliwa na rais, James Mbatia, ameapa kuwasha moto katika Bunge lijalo hadi kieleweke.
Mbatia
ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema lazima Waziri Mkuu
atoe majibu ya msingi kwa Watanzania kwanini hakutekeleza maazimio ya
tume ya Lowassa.
Alienda
mbali na kuhoji utendaji wa kitengo cha maafa cha Waziri Mkuu kwani
kimekuwa kikishughulika kutoa vyakula vya misaada kwenye maafa badala
ya kudhibiti yasitokee.
“Tangu
tume zianze kuundwa kuhusu maafa ni akina nani walichukuliwa hatua?
Kuanzia tume ya MV Bukoba hadi tume ya matokeo ya kidato cha nne,
Watanzania tumechoka kuneemesha mifuko ya wajumbe wa tume na kufilisi
rasilimali zetu, hivyo Pinda, Tibaijuka lazima wajiuzulu,” alisema.
Wakati
wabunge hao wakitaka Pinda na Tibaijuka waachie ngazi, habari zaidi
ndani ya serikali zinasema kuwa ripoti ya Tume ya Lowassa haikufanyiwa
kazi kwani baadhi ya majengo yaliyopendekezwa kubomolewa, yanawahusu
viongozi wa juu serikalini.
“Ile
ripoti iliwasilishwa wakati Lowassa bado yuko madarakani. Alishindwa
kuifanyia kazi na haiwezi kufanyiwa kazi kwani baadhi ya majengo
yanawahusu viongozi au yanamilikiwa na watu wa karibu wa viongozi, na
ndio wachangiaji wakubwa wa fedha wakati wa kampeni,” kilisema chanzo
chetu cha habari.
Akifanya
majumuisho katika hotuba ya matumizi ya ofisi yake bungeni kwa mwaka
2008/09, Pinda alizungumzia jinsi Tume ya Lowassa ilivyofanya kazi
katika sakata la ghorofa kuanguka jijini Dar es Salaam.
Pinda
alilithibitishia Bunge kuwa zaidi ya maghorofa 100 jijini Dar es
Salaam yalibainika kuwa yalijengwa kinyume na taratibu za ujenzi.
Kwa mujibu wa ripoti iliyoundwa na Lowassa, kati ya maghorofa 505 ambayo waliyakagua, 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.
Lowassa
aliunda tume baada ya jengo la hoteli ya Chang’ombe Village Inn, Keko,
Dar es Salaam kuanguka mwaka 2006 na kuua mtu mmoja na kujeruhi
wengine kadhaa. Ilidaiwa kwamba ulikuwapo ukiukwaji katika ujenzi wake.
Pinda
aliliambia Bunge kuwa tume hiyo ya Lowassa ilibaini pia maghorofa 81
yalikutwa yamekiuka masharti ya ujenzi huku mengine 22 wenyewe
hawakupatikana na yalikuwa yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi
pamoja na uzembe wa baadhi ya watendaji wakiwamo wahandisi wa manispaa
husika.
NHC yatoa kauli
SHIRIKA
la Nyumba la Taifa (NHC) limesema kuwa mbia wao alikuwa na vibali vya
mamlaka zinazohusika kusimamia ujenzi wa majengo makubwa vya kumruhusu
kuongeza ghorofa 16 kutoka kumi za awali.
Kauli
hiyo inakuja kukiwepo na mvutano kutoka mamlaka mbalimbali ikiwemo
Manispaa ya Ilala kwamba mbia wao huyo ambaye ni M/s Ladha Construction
alipewa kibali cha kujenga ghorofa kumi, lakini cha kushangaza
aliongeza nyingine sita bila taarifa na hivyo kusadikiwa kuwa huenda
ndiyo chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa NHC, Nehemiah Mchechu akizungumza jana na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaa, alisema Agosti 22 mwaka jana mbia wao huyo
aliwataarifu kuwa ameshapata vibali kutoka mamlaka husika, na kwamba
angependa aingie nao mkataba mdogo kutambua ongezeko la ghorofa hizo na
mabadiliko ya tarehe ya kumaliza mradi.
“Shirika
lilimjibu kuwa hakuna pingamizi kama mbia ataleta nakala ya vibali
kutoka mamlaka husika kwa ajili ya kumbukumbu za shirika na pia ili
kufikia hatua za maamuzi ya ndani na mawasiliano yote hayo yapo kwenye
rekodi zetu na endapo mamlaka husika itazihitaji tuzazipatia,” alisema.
Kutokana
na hali hiyo, aliutaka umma kutoliingiza shirika hilo katika sakata
hilo kwa madai kuwa zipo taasisi na vyombo vinavyokasimiwa mamlaka ya
kusimamia ubora wa ujenzi wa nyumba nchini, na NHC nayo husimamiwa na
taasisi na vyombo hivyo.SHUKRANI TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment