Wednesday, September 06, 2017

WANAFUNZI 917,072 KUFANYA MTIHANI WA DARASA LA SABA LEO

Baraza la Taifa la Mitihani nchini (NECTA) limesema maandalizi ya kuanza mtihani wa Taifa wa darasa la saba utakaofanyika leo jumatano Septemba 6 na kesho alhamisi ya Septemba 7 yamekamilika.

Akizungumza na wanahabari kuhusu maandalizi hayo, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde. Tayari mitihani imesafirishwa katika maeneo yote nchini na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza kwa mtihani.

“Leo na kesho katika shule zetu 16,583 za msingi nchini kutakuwa ana mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, watahiniwa ni 917,072 wataufanya wavulana wakiwa 432,744 sawa na asilimia 47.19%, wasichana ni 484,328 sawa na asilimia 52.81%, mwaka jana watahiniwa walikuwa 795,761.

EMIRATES TANZANIA YAPATA BOSI MPYA

Uongozi wa shirika la ndege la kimataifa la Emirates umemteua Bwana Rashed Alfajeer kuwa meneja mkuu mpya wa shirika hilo nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa shirika hilo nchini Tanzania inasema, Bwana Alfajeer, kutoka katika nchi za Falme za Kiarabu, atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli zote za Emirates za kibiashara, wateja na mizigo kwenye soko.

"Nina furaha kwa kuchaguliwa kuwa meneja mpya wa Emirates nchini Tanzania na ninatarajia kufanya kazi na timu ya ndani, pamoja na washirika wetu wa biashara katika kuendeleza biashara zaidi ya Emirates kwenye soko," alisema Alfajeer.

"Mtazamo wangu utakuwa kuendelea kuwapa wateja wetu wa Tanzania huduma bora kulingana na thamani ya pesa, tunapowaunganisha kwenye maeneo zaidi ya 150 ulimwenguni kote," aliongeza.

Bwana Alfajeer alijiunga na Emirates mwaka 2013 kama sehemu ya mpango wa Emirates kama msimamizi wa Taifa wa Uendeshaji wa Biashara. Tangu wakati huo, amefanya kazi za biashara nchini Sri Lanka kabla ya kuchukua nafasi ya Meneja wa Wilaya huko Dammam, Saudi Arabia mwaka 2015.

Emirates hufanya safiri mara moja kwa siku kati ya Dar es Salaam na Dubai na ndege kubwa aina ya Boeing 777.

HASHIM RUNGWE ASHIKILIWA NA POLISI

Aliyekuwa mgombea Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Hashim Rungwe anashikiliwa na polisi kwa siku nne sasa.

Rungwe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Chaumma anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Mwanasiasa huyo anashikiliwa akituhumiwa kughushi nyaraka.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema jana Septemba 5 kuwa, Rungwe anashikiliwa kituoni hapo kwa siku nne.

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo akisema hana taarifa za kutosha.

JAJI MARAGA AMJIBU UHURU KENYATTA

JAJI Mkuu David Maraga amejibu shutuma kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wa Chama cha Jubilee, kufuatia uamuzi wa  Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais.

Viongozi wa Jubilee wamemkosoa Maraga wakidai anatumiwa na upinzani kutoa maamuzi yanayoupendelea muungano wa NASA, na wameapa  kuupitia uamuzi huo wa mahakama wakati uchaguzi utakapomalizika.

“Mimi si mwanasiasa na ninafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya kiapo cha utii nilichoapa kuwatumikia Wakenya. Siungi mkono Jubilee wala NASA au  mtu yeyote,” alisema Jaji Maraga katika taarifa yake fupi jana.

Rais Kenyatta mwishoni mwa wiki iliyopita alimkosoa Maraga akimwita ‘mkora’, kwamba ‘alipindua’ matakwa ya mamilioni ya Wakenya waliomchagua.

Kufuatia vitisho hivyo, ambavyo vimelaaniwa vikali na wanaharakati na katika mitandao ya jamii, Maraga ambaye ni mzee wa Kanisa la Sabato (SDA),  alisisitiza kuwa anamwogopa Mungu pekee.

“Ninafuata katiba yetu. Nendeni mkaendeshe uchaguzi na iwapo mtu anapinga, lete shauri ukiwa na ushahidi mzuri na nitalifanyia kazi ipasavyo.  Kumbuka namhofia Mungu pekee,” alisema Maraga ambaye anaongoza mfumo wa mahakama

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...