Saturday, February 16, 2013

MICHUANO YA KOMBE LA SHIRIKISHO, AZAM YAIFUNGA EL NASIR 3-1

Kiungo wa timu ya Azam FC, Bolou Kipre (kushoto) akitafuta mbinu za kumtoka mshambuliaji wa El-Nasir FC ya Sudan ya Kusini, Abdallmelik Sebit katika mchezo wa Kombe la Shirikisho uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Wachezaji wa Azam FC wakishangilia bao la pili la timu yao lililofungwa na Kipre Tchetche (katikati) wakati ilipoibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya El Nasir ya Sudan ya Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
 Jabir Aziz akitafuta mbinu za kuwatoka mabeki wa El Nasir FC ya Sudan ya Kusini katika mchezo wa Kombe la Shirikisho uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Mshambuliaji wa Azam FC, Brian Umomy akiwatoka walinzi wa timu ya El-Nasir FC ya Sudan ya Kusini, Jacob Osuru na Abdallmelik Sebit katika mchezo wa kombe la Shirikisho uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 Kikosi cha el Nasir ya Sudan ya Kusini
 Kikosi cha Azam FC
Mashabiki wa Azam

ZIARA YA MAMA SALMA KIKWETE LINDI LEO

 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na wananchi wa kijiji cha Narunyu, Kata ya Tandangongoro, alipokwenda kuhutubia mkutano wa hadhara katika kijiji hicho leo.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwasalimiana na watoto wa kijiji cha Narunyu, Kata ya Tandangongoro, alipokwenda kuhutubia mkutano wa hadhara katika kijiji hicho leo.
 Mkazi wa Kijiji cha Ng'apa wilaya ya Lindi mjini, akionyesha kadi yake ya matibabu ya Huduma ya Kadi ulkiopo chini ya Bima ya Afya, wakati wa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika kijiji hicho, leo Feb 16, 2013. Mama Salma Kikwete alimpatia fursa ya kuzungumza wakati akihimiza umuhimu wa wananchi kujiunga na mpango huo wa matibabu.
 Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa amegoma kushuka katika gari lake, kukataa kwenda kwenye mkutano wa ndani wa Chama Kata ya Tandangongoro, uliokuwa umepangwa na viongozi wa kata hiyo kufanyika katika chumba cha darasa la shule ya msingi ya kijiji cha Ng'apa, mkoani Lindi, leo Februari 16, 2013. Hatua hiyo iliwalazimu viongozi kutafuta ukumbi mwingine wa dharura. Mama Salma alisema si sahihi mkutano wa ndani wa Chama cha siasa kufanyika katika chumba cha darasa la shule ya serikali
Umati wa wananchi wa Kijiji cha Ng'apa wakimsiliza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akilipowahutubia mkutano wa hadhara leo. PICHA ZOTE NA BASHIR NKOROMO.

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ASIMAMIA ZOEZI LA UTEKETEZAJI SILAHA HARAMU JIJINI DAR LEO

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akivuta waya kuashiria kufyatua mtego wa kuwasha moto wa kuteketeza Silaha haramu, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo la uteketezaji wa silaha haramu, Lililofanyika katika Kambi ya Magereza jijini Dar es Salaam, leo Feb 16, 2013. Kushoto kwake ni Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Siro na wa pili kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perera Ame Silima na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kmataifa, Benard Membe.
 Sehemu ya Silaha hizo zikianza kuteketea kwa moto baada ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, kufyatua waya maalumu wa kuwasha moto huo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi, baada ya kusimamia zaoezi la uteketezaji wa Silaha haramu, lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, wakati wakipita kukagua sihala hizo haramu kabla ya kuanza kwa zoezi la uteketezaji wa silaha hizo haramu lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.


 Silaha haramu zilizoteketezwa hii leo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa zoezi la uteketezaji wa Silaha Haramu, lililofanyika Ukonga Jijini Dar es Salaam leo.
Wimbo wa Taifa, kabla ya kuanza kwa zoezi hilo. 
*******************************************************

DKT. BILAL AWATAKA WANANCHI KUWAFICHUA WANAOMILIKI SILAHA HARAMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameongoza zoezi la uteketezaji silaha haramu na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuwafichua wanaomiliki silaha hizo mapema kabla athari haijawa kubwa zaidi.

Akizungumza katika zoezi hilo la kuteketeza silaha haramu, ambalo limefanyika pamoja kwa  nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye viwanja vya Magereza, Ukonga Jijini Dar es salaam Dkt. Bilal alisema  kila mwananchi ni mlinzi wa kwanza wa amani ya nchi yake  na  wanaomiliki silaha haramu ni wazi kuwa siyo raia wenye malengo mema na amani ya nchi zao.

“Naomba kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanikisha zoezi hili ambalo linalenga kutukumbusha kuwa ili tuwe na Jumuiya bora yenye kupiga hatua, hatuna budi kuhakikisha eneo letu linabaki kuwa salama na kwamba wananchi wetu wanapata nafasi ya kufanya kazi zao za kujiongezea kipato bila kuwa na hofu ya usalama wa maisha yao,”

Alisema ndani ya Jumuiya kumekuwa na migogoro mbalimbali sambamba na matukio ya kihalifu ambayo mengi huchangiwa na uwepo wa silaha ndogo na kubwa ambazo hazimilikiwi kihalali.

Alisema takwimu zilizopo zinabainisha kuwepo kwa silaha haramu zipatazo 500,000 (laki tano) katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki hali ambayo inaonesha kuwa kuna kazi kubwa ya kukabiliana na migogoro ya aina mbalimbali ya uhalifu inayojitokeza katika jamii.

Alisema kufuatia raia wasio waaminifu kumiliki silaha haramu kumekuwepo na ongezeko la matukio ya kihalifu yanayotumia silaha na matukio mengi katika ukanda wa Afrika Mashariki yanatokea katika maeno ya mipakani na yale yanayohusisha muingiliano wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, matukio ya ujambazi,  uvamizi na mengine ya aina hiyo.

Alisema ongezeko la silaha haramu lina athari nyingi katika maisha na maendeleo kwa ujumla na kutaja athari ya wazi kabisa inayotokana na ongezeko la silaha hizo kuwa ni ile inayojitokeza katika sekta ya Utalii ambako watu wameshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujangili unaofanywa katika mbuga za wanyama ambao unahatarisha kwa kiasi kikubwa mafanikio katika sekta ya Utalii.

“Tusipowadhibiti majangili mapema, siku wanyama wakipungua watahamia katika sekta nyingine. Kazi hii itakuwa rahisi kama tukiifanya kama Jumuiya na sio nchi moja moja,” alibainisha Makamu wa Rais.

Dkt. Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki kukabiliana na tatizo la silaha haramu na hasa Shirika la Maendeleo la Ujerumani GTZ ambalo limesaidia katika kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini Klaus Brandes alisema  Serikali ya Ujerumani itaendelea kuisaidia Jumuiya katika kukabiliana na tatizo la silaha haramu ili kuhakikisha eneo la ukanda wa Afrika Mashariki linabaki kuwa na amani na salama.   

Alielezea kufurahishwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kutatua migogoro kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Februari 16, 2013

Watanzania tunaitakia kila la kheri Azam FC katika mechi yake ya leo dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.


Mashabiki wa soka nchini Tanzania leo wataelekeza macho na masikio yao katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam kushudia mechi ya kiataifa baina ya timu ya Azam Fc ikipambana na Al Nasir Juba  ya Sudan Kusini   
Mabingwa hao mara mbili wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar Azam Fc leo watakuwa wakicheza kwa mara ya kwanza michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Africa (CAF).
Katika mechi ya leo Azam itaingia uwanjani kwa lengo la kupata ushindi mkubwa ili kujiweka mazingira mazuri katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Juba.

HATIMAYE SISTA ALIYEFUMANIWA AHUKUMIWA


MAHAKAMA ya Mwanzo mjini Sumbawanga,  imemtia hatiani aliyekuwa mtawa wa Shirika la Kitawa la Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga, Sista Yasinta Sindani, kwa kufumaniwa na mume wa mtu na kuamriwa kumlipa fidia ya
Sh 700,000 mlalamikaji.
Katika kesi ya msingi ya madai, mlalamikaji Asteria Mgabo alimtaka Sista Yasinta amlipe Sh milioni 3 baada ya kumfumania na mumewe wa ndoa, Martin Msangawale (39) ambaye pia ni mkazi wa mjini Sumbawanga.

Sista huyo ambaye ni daktari katika Hospitali ya Mkoa wa Rukwa mjiniSumbawanga, kwa sasa anaishi nje ya nyumba ya utawa eneo la Kantalamba.
Katika hati ya awali ya madai, inadaiwa mshitakiwa alifumaniwa na Asteria akiwa na mumewe Msangawale wakiwa kwenye nyumba ya kulala wageni  ijulikanayo kwa jina la Chipa iliyopo eneo la Katandala mjini Sumbawanga, Desemba 24  mwaka jana majira ya saa 7 usiku  ikiwa ni siku ya mkesha wa Sikukuu ya Krismas.
Akisoma  hukumu  hiyo juzi, hakimu wa  mahakama  hiyo, Jaffar Mkinga alisema kuwa ushahidi uliotolewa na mlalamikaji ulikuwa mzito wenye kuondoa shaka zote  kuwa mdaiwa alitenda kosa hilo tofauti na utetezi  uliotolewa na mdai kuwa ulikuwa dhaifu.

Awali katika  utetezi wake  mdaiwa  aliiambia mahakama  hiyo kuwa  kwanza alikuwa hajui kuwa Martin alikuwa  mume wa mtu na kukiri mbele ya mahakama hiyo kuwa alimweleza kuwa hana mke hivyo alimwomba amuoe.
Lakini Hakimu Mkinga alipinga utetezi huo kwa sababu usiku  huo wa mkesha  wa Krismas  mwaka jana, saa saba na robo usiku, mlalamikaji akiongozana na mwenyekiti wa mtaa wakiwa na mashahidi wengine watatu,  walimkuta mdaiwa na Martin wakitoka katika   moja ya vyumba katika nyumba ya kulala  wageni ya Chipa, akasainishwa.
“Kama hukufahamu kuwa Martin alikuwa  hana  mke ilikuwaje ukakubali kusaini karatasi hiyo ya fumanizi  iliyoandaliwa na mwenyekiti  huyo?” alihoji hakimu, akamhukumu kulipa sh 700,000.

Rais Deby wa Chad awafukuza kazi mawaziri wawili, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuwasimamisha kazi askari wa jeshi la polisi nchini humo.


Rais Idriss Deby wa Chad amewafukuza kazi mawaziri wawili wanaohusika na masuala ya ulinzi ikiwa ni baada ya wiki iliyopita kuwasimamisha kazi takriban polisi zaidi ya 6,000 kwa tuhuma za rushwa, upendeleo na udhalilishaji.
Katika tangazo lililotolewa katika radio ya taifa, rais Deby amemfukuza Waziri wa Usalama wa Umma Ahmat Mahamat Bachir na Waziri wa Usimamizi dhidi ya Ugaidi Bachar Ali Souleymane.
Kufukuzwa kwa mawaziri hao kunafuatia pia kufukuzwa kazi kwa Mkuu wa Polisi nchini humo, ikiwa ni siku mbili baada ya kulisimamisha kazi jeshi hilo.

Uso mtoto wa Jay – Z Blue Ivy Carter kwa mara ya kwanza waanikwa hadharani.!


Pichani ni Jay-Z na mtoto wake Blue Ivy mwenye umri wa mwaka mmoja kwa mara ya kwanza imewekwa hadharani kuonyesha baba na mwana wanavyofanana.
Blue Ivy akiwa na mama yake.

urais Kenya pamoja na mashitaka yanayomkabili ICC.


Mahakama Kuu nchini Kenya imemsafishia njia mmoja kati ya wagombea urais Bw. Uhuru Kenyata kuwania kiti cha urais wa taifa hilo katika uchaguzi mkuu ujao pamoja na kukabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Ikiwa imebakia muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu wa Machi 4 mwaka, uamuzi huo umemuweka Kenyatta huru kuwania kiti hicho akionekana kama mmoja kati ya viongozi wanaongoza katika kinyang’anyiro cha urais.
Jopo la majaji watano waliokuwa wanasikiliza kesi hiyo wanasema mahakama kuu ndiyo yenye uwezo wa kuamua kesi hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa kupinga ushiriki wa watu hao katika uchaguzi wa mwezi Machi, kwa kile walichokiita kukosa uadilifu kwa sababu tayari wamefunguliwa mashtaka ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC.

WABUNGE 47 KIJIUNGA NA JKT, WAMO ZITTO KABWE,HALIMA MDEE,KAFULILA, MBOWE, JOSHUA NASSARI,ESTHER BULAYA,LEMA,NYAMBARI NYANGWINE N.K



 JUMLA ya wabunge 47 kutoka vyama CCM, Chadema na NCCR-Mageuzi, wamekubali kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa ajili ya mafunzo na uzalendo kwa taifa.
Habari za kuaminika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Makao Makuu ya JKT, zinasema wabunge hao wametawanywa katika vikosi mbalimbali na wanatakiwa kuripoti kwenye vikosi vyao kunzia Machi mosi, mwaka huu.
Msemaji wa JKT, Meja Emmanuel Mruga, alipoulizwa kuhusu wabunge hao kujiunga na jeshi hilo, alisema mpaka sasa wana orodha ya wabunge 47 kutoka vyama mbalimbali.
Alisema wabunge hao, wametawanywa katika kambi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ambayo yatarajia kuanza mwezi ujao.
Alisema wabunge hao, waliomba wenyewe kwa ajili ya kupata mafunzo ambayo wanaamini yatawajengea uzalendo zaidi kwa taifa lao.
Baadhi ya wabunge ambao MTANZANIA imepata majina yao na vyama wanavyotoka kwenye mabano ni David Kafulila (NCCR-Mageuzi), Zitto Kabwe (CHADEMA), Halima Mdee (CHADEMA), Freeman Mbowe (CHADEMA), Abdulkarim Shaha (CCM), Esther Bulaya (CCM), Twaida Galusi (CCM), Neema Hemed (CCM), Ezekiel Wenje (CHADEMA), Joshua Nassari (CHADEMA), Raya Ibrahim (CHADEMA), Godbless Lema (CHADEMA) na Nyambari Nyangwine (CCM).
Akizungumzia mafunzo hayo, Zitto Kabwe alisema kuanzia sasa anajiandaa kuanza maisha mapya ya jeshi na atapumzika siasa kwa muda wa miezi sita.
“Najiandaa kupumzika siasa, kwa ajili ya kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), nadhani ni hatua nzuri ambayo tunataka kuwaonyesha Watanzania wazalendo na vijana wenzetu,” alisema Zitto.
Naye Mdee, alisema zaidi ya robo tatu ya wabunge wote vijana wa chama hicho, waliomba kujiunga JKT na tayari wamepangwa katika vikosi mbalimbali.
“Si mimi na Zitto, nakwambia karibu robo tatu ya wabunge vijana wa CHADEMA, tumeamua kujiunga kwenye mafunzo ya JKT,” alisema Mdee.
Alisema yeye amepangwa kikosi cha 842 KJ kilichopo Mlale, mkoani Ruvuma.
Alisema wengine ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye amepangiwa kikosi cha JKT Ruvu, Mkoa wa Pwani.
Habari zinasema Mbowe aliomba kujiunga JTK na amepangiwa kambi moja mkoani Tabora.
Akizungumzia sababu za kujiunga na jeshi hilo, Mdee alisema wanataka kujifunza mambo tofauti yatakayowasaidia kutekeleza wajibu wao wa kisiasa na kijamii sawasawa.
“Unajua sisi ni viongozi wa watu, tunadhani mafunzo ya kijeshi yatatusaidia kutekeleza kazi za kila siku, kujifunza ukakamavu, na zaidi kwa vipi tunaweza kujilinda kwa mantiki ya usalama binafsi.
“Kingine ni kujifunza kazi za kila siku za maisha, kiuchumi, kijamii, kilimo na vitu kama hivyo ukizingatia sisi ni viongozi tunaopaswa kuongoza watu, hususani wapiga kura kwa mifano.
Kuhusu kujifunza zaidi uzalendo kama ambavyo imekuwa ikisemwa na viongozi serikalini, Mdee alisema uzalendo ni tabia ya mtu binafsi na kamwe jeshi haliwezi kumfundisha mtu uzalendo.
“Ninakubaliana na suala la nidhamu, jeshi linaweza kumfundisha mtu nidhamu, lakini siyo uzalendo.
“Walioharibu nchi na kuitumbukiza katika ufukara na ufisadi karibu wote wamepitia jeshini, hatuna cha kujifunza kwao kutokana na kwenda kwao jeshini,” alisema na kuongeza:
“Ngoja twende huko tukajifunze mambo ya ziada, naamini tutapata kitu cha ziada kwa ajili yetu na jamii tunayoiongoza”.

FAMILIA YA NYERERE YAMKANA ANAYEJIITA MAKONGORO NYERERE

Mwalimu Nyerere

 



Familia ya Joseph Nyerere, imejitokeza na kusema haimtambui mtuhumiwa wa kesi ya mauaji, anayejitambulisha kwa jina la Makongoro Joseph Nyerere.

Taarifa iliyotolewa na Nuru Nyerere-Inyangete, kwa niaba ya familia hiyo jana, ilisema hadi kifo cha baba yao, Joseph Kizurira Nyerere, mwaka 1994 haina taarifa zozote za kuwa na ndugu yao anayeitwa Makongoro Joseph Nyerere.

“Hadi baba anafariki dunia hatukuambiwa tuna ndugu anayeitwa Makongoro Joseph Kizurira Nyerere …watoto wote wa Mzee Joseph tunafahamiana, lakini kwa huyu ndiyo kwanza tunaambiwa kuwa ni ndugu yetu. Tunauhakikishia umma kwamba hadi kifo cha baba yetu hatukuambiwa juu ya kuwapo kwa ndugu mwenye jina hilo; hii ina maana kwamba hatumtambui,” alisema Nuru.

Naye mtoto mwingine wa Joseph, Matare, alisema, “Tangu kutangazwa kwa habari hizi tunapata simu nyingi za pole. Tunashangaa kwa sababu huyu mtu hatukuwahi kuambiwa kuwa ni ndugu yetu, na wala yeye mwenyewe hakuwahi kuja kwetu kujitambulisha kama ni mmoja wa watoto wa Mzee Joseph.”

Matare aliongeza, “Tumesoma kwa mshituko kwenye magazeti ya Februari 14, 2013 na katika mitandao ya kijamii, kuwa kuna mtu anayejiita Makongoro Joseph Nyerere. Huyu huyu hatumtambui kwa uhusiano, taarifa wala sura. Watoto wote wa marehemu Joseph Nyerere wanafahamika, hakuna mtoto wa marehemu mwenye jina hilo.”
Juzi, Makongoro ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo akikabiliwa na mashitaka ya mauaji ya mfanyabiashara mwenzake, Onesphory Kitoli. Mtuhumiwa huyo anatarajiwa kuunganishwa katika kesi hiyo na mtuhumiwa mwingine mfanyabiashara maarufu, Marijani Abubakari marufu kama Papaa Msofe (50). Kesi hiyo itatajwa Februari 20, mwaka huu.

Wakili wa Serikali, Charles Anindo, alimsomea Makongoro mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome, na kudai kuwa Novemba 6, 2011 huko Magomeni Mapipa, Makongoro alimuua kwa makusudi Kitoli kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Anindo alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na aliomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Februari 20, mwaka huu, ambako Makongoro ataunganishwa na Papaa Msofe kwenye mashitaka hayo.

Mtuhumkiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Mzee Mwinyi kuzindua kampeni ya uboreshaji wa wodi za kinamama jijini Dar


Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Taasisi ya Africa Youth Cross Cultural Exchange & Environment Conservation inatarajia kuzindua rasmi kampeni za uboreshaji wa wodi za kina mama wajawazito na watoto.
Mratibu wa Kampeni hiyo William Kotta amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wodi hizo zinakuwa na vifaa vinavyo jitosheleza kwa ajili ya kusaidia kina mama na watoto wanaoteseka na kupoteza maisha hasa wakati wa kujifungua.
Amesema taasisi hii katika kuanza kutekeleza kampeni hiyo, siku ya tarehe 22 Februari 2013 wameandaa chakula cha hisani kwa lengo la kuchangisha fedha na kusaidia upatikanaji wa vifaa hivyo.
Shughuli hiyo kwa heshima kubwa itaongozwa na Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi rais mstaafu wa awamu ya pili.

Balozi Seif Idd aitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuhamasishana kuanzisha miradi ya kijamii.


Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Mfuko wa  Jamii (NSSF) Kanda ya Dodoma Bibi Maryam Ahmed akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kumsajili rasmi kuwa mwanachama wa Mfuko huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijaza Fomu Maalum ya kuomba uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
 Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliofika Ofisini kwake Vuga kumsajili rasmi kuwa mwanachama wa mfuko huo.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Halima Bushir Abeid mchango wa Shilingi 100,000/- kwa ajili ya ulipaji huduma ya umeme ya kituo hicho mbaleni Jimboni humo.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) umeombwa kufanya utaratibu wa kuishawishi mifuko mingine ya Jamii kuanzisha  miradi ya Jamii ili kuongeza pato la wanachama pamoja na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  wakati akijaza fomu maalum ya kuomba kujiunga kuwa mwanachama rasmi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) shughuli ambayo aliifanya Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif amesema Mfuko huo umeonyesha mwanga na matumaini makubwa kwa wanachama wake hasa kutokana na miradi mingi iliyoianzisha ambayo kwa asilimia kubwa inalenga kuwanufaisha wanachama wake hasa wale wenye kipato cha chini.
Amesema NSSF ni chombo cha wananchi kwa vile kinajihusisha moja kwa moja na hatma ya washirika wake ambao wengi wao ni wafanyakazi wenye kipato cha chini.
Balozi Seif aliuahidi Uongozi wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwamba amehamasika ya mfumo wa mfuko huo na kupelekea moja kwa moja kuamua kujiunga ambapo ameahidi kuchangia kila baada ya kipindi cha miezi mitatu.
Mapema Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Dodoma ambao ndio uliopewa jukumu la kuhudumia Viongozi wa ngazi ya Juu Bibi Maryma Ahmed amesema zaidi ya Wabunge 165 wamekubali kujiunga kwa hiari kuwa wanachama wa Mfuko huo.
Bibi Maryam alimueleza Balozi Seif kwamba wabunge hao hupatiwa mafao yao mara wamalizapo utumishi wao wa Bunge sambamba na huduma za matibabu wakati wa kipindi chote cha kazi zao.
Wakati huo huo Balozi Seif akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope amekabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa Tawi la CCM la Mbaleni liliomo ndani ya Jimbo hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni Mchanga, Matofali pamoja na Saruji Balozi Seif amesema wana CCM lazima waendelea kushikamana kwa lengo la kukiwezesha chama hicho kuendelea kushika dola.
Alifahamisha kwamba amani ya Tanzania itaendelea kuwepo na kuleta matumaini iwapo chama cha Mapinduzi kupitia Serikali zake zote mbili kitaendelea kuliongoza Taifa hili.
Vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa Tawi la CCM Mbaleni Jimbo la Kitope sambamba na ahadi ya Seti moja ya Jezi na Mipira iliyotolewa na Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi vimegharimu jumla ya shuilingi Milioni  Moja Nukta Tisa (1,960,000/)

IBF Yachukua nafasi ya Katikati Barani Afrika.


Upimaji uzito katika mapambano mawili ya IBF yanayofanyika katika majiji ya Johannesburg na Tunis umefanyika vizuri leo.
Mapambano haya yaliyopewa jina la “Barabara ya kutoka Cape Town mpaka Cairo kwa IBF” kutokana na majiji haya kukaa moja kusini na lingine kaskazini mwa Afrika, yanafanyika wakati IBF ikijipambanua vyema katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi.
Kusini mwa Afrika, leo imeshughudia mabaondia mawili wanaopambania ubingwa wa dunia kwa vijana walio chini ya miaka 25 wakipima uzito mbele ya mashirika mbalimbali ya habari ya ndani na nje ya Afrika ya Kusini.
Illunga Makabu kutoka Jamhuri ay Watu wa Kongo (DRC) alipima uzito kumkabili Gogota Gorgiladze wa Georgia. Upimaji huo ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa ulio katika hotel ya nyota tano ya Emperors Palace iliyoko katika jiji la Johannesburg!
Rodney Berman mtu anayeheshimika kwa kuwa promota wa kwanza kuandaa pambano la IBF la dunia katika bara la Afrika mwaka 1990, ndiye anayepromoti pambano hili!
Tayari wadau na mashabiki wa ngumi kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwamo Namibia, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe na Tanzania wameshawasili nchini Afrika ya Kusini tayari kuangalia mpambano huo. Wengine walibaki Afrika ya Kusini wakati wa mashindano ya kombe la Afrika yaliyomalizika wiki iliyoita.
Msimamazi mkuu wa mpambano huu ni Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi aliyesimama pichani na mabondia Gogita Gorgiladze (kushoto) na Ilunga Makabu (kulia)
Kaskazini mwa Afrika,
Bondia ambaye ameshajizolea sifa kemkem Ayoub Nefzi wa Tunisia anayeishi nchini Belgium atapigana na bondia Ishmael Tetteh kutoka nchi ya Ghana kugombea ubingwa wa Afrika, Ghuba ya Uajemi  na Mashariki ya Kati (IBF AMEPG) katika uzito wa Light Middle.
Mpambano huo uliopewa jina la “Uzuri wa Jasmine” kutokana na jina hilo kutumika katika mapinduzi yaliyomwondoa Rais wa zamani wa Tunisia Ben Ali unafanyika wakati Ayoub Nefzi akijiandaa kugombea mkanda wa juu wa IBF wa mabara mwezi wa tatu nchini Belgium.
Mabondia wote wawili wanatagemea kuonyesha moto mkali katika mpambano ambao tayari mashabiki wa ngumi kutoka katika nchi za Nigeria, Ghana, Libya, Misri, Algeria tayari wameshawasili nchini Tunisia kuangalia mpambano huo!
Tunisia inasifika kama nchi iliyowahi kutoa viongozi wengi wa mchezo wa ngumi katika bara la Afrika.

Fastjet yatoa mafunzo kwa Mtanzania wa Kwanza Mmaasai kuongoza ndege aina ya Airbus.


William Zelothe Stepehen akiwa ndani ya ndege aina ya Airbus A319.
William Zelothe Stepehen akiwa na marubani wa ndege ya Fastjet.
 
William Zelothe Stepehen ni Mtanzania wa Kwanza Mmaasai aliyepewa ithibati ya kuiongoza ndege aina ya Airbus A319 punde tu baada ya kupokea mafunzo ya urubani yaliyodhaminiwa na shirika la ndege la fastjet. Alipata mafunzo hayo nchini Uingereza kwa muda wa takriban miezi miwili na amerudi nchini Tanzania hivi karibuni. William alikulia Olosipe jijini Arusha ambapo ni nyumbani kwa wazazi wake.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI



JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
15 Februari 2013


 
Meli vita tatu (3) kutoka Jeshi la Wanamaji la Urusi zijulikanazo “MARSHAL SHAPOSHNIKOV”, “ALATAU” na “IRKUT” zikiongozwa na Rear Admiral Vladimir Vdovenko, watawasili nchini tarehe 16 February 2013 na kuondoka tarehe 20 Februari 2013 katika bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kufanya ziara ya kirafiki baina ya Jeshi la Wanamaji wa Tanzania na Urusi.
Waandishi wa Habari mnakaribishwa kufanya ‘coverage’ ya tukio hilo
Siku ya Jumatatu, tarehe 18 February 2013 saa 1.00 hadi saa 3.00 usiku.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano, Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
SLP 9203, Simu: 0764 742161
Email: ulinzimagazine@yahoo.co.uk
K U M B U K U M B U
MMJ/JB/
Feb 13
DP ADMN
Kufanya mahusiano na uongozi wa Bandari
1. Kurugenzi ya Habari imefanya zoezi la kuwaita waandishi wa Habari kutoka vyombo vya habari vifuatavyo TBC, ITV, CLOUDS TV, MLIMANI TV, STAR TV, na CHANEL TEN.
2. Uongozi wa Bandari hauruhusu Waandishi wa Habari kuingia kufanya “coverage” kwenye eneo hilo bila taarifa rasmi.
3. Inaombwa mahusiano yafanyike na bandari kuhusiana na mapokezi ya waandishi wa habari watakao hudhuria siku hiyo ili kukwepa usumbufu kwa waandishi hao.

 
(KM Mgawe)
Col
DIPR

NEY WA MITEGO APATA AJALI MBAYA YA GARI

Usiku wa juzi kuamkia jana, Rapa Ney wa mitego, alipata ajali mbaya ya gari maeneo ya Oysterbay jijini Dar na mguu wake ukshtuka kidogo, ila rafiki yake aliekuwa nae, ameumia kichwani na jana ndio aliruhusiwa kutoka hospitali

ajali hiyo ilitokea maeneo ya mataa ya St Peters, alipokuwa akitokea masaki kuelekea moroko, na  baada ya mataa yake kumruhusu kupita, alikutana na Lori lililokuwa likitokea Mjini kuelekea Moroko pia, likiwa halina taa na kumvaa kwa nyuma na kupelekea gari lake kuingia mtaroni na kuharibika vibaya

ndinga aliyokuwa nayo Ney ni aina ya Altezza, ina thamani ya shilingi millioni 14, kama angekuwa amelipia bima katika kiwango cha Comprehensive, yaani bima kubwa, angerudishiwa gari ndinga mpya, akini kwa bahati mbaya alilipa bima ya kawaida


Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...