Tuesday, August 18, 2015

KIPINDU PINDU CHAZUKA DAR CHAUA WATU WAWILI


UGONJWA wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na watu wawili wamethibitika kufa.

Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni. Kutokana na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo kuwa zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1). Alisema watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine ni mwanamke na wanatoka Manispaa ya Kinondoni.

MENINAH AOLEWA NA MTOTO WA PROF. MUHONGO


MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Meninah Atick ‘Mennahladiva’ mwishoni mwa wiki aliuaga ukapera kwa kufunga ndoa na mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Abdukarim Haule.

Meninah, ambaye kipaji chake cha muziki kilianza kuonekana kupitia shindano la Bongo Star Search, ametamba na nyimbo za ‘Dream Tonight’, ‘Ka-Copy Ka-Paste’. Mtoto huyo wa Waziri Muhongo, Peter Haule, amebadili dini na kuitwa Abdukarim Haule na harusi yao ilifanyika Kigamboni, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Licha ya wengi kumpongeza msanii huyo, ameandika katika ukurasa wake wa Instagram kwamba: “Usichague msichana ambaye ni mzuri duniani, chagua anayekupa furaha duniani, maisha ni mafupi na huwezi jua kesho kuna nini, fanya mazuri, asante Mungu kwa kila njia ninayopitia, nazidi kukumbuka kwa kubadilisha maisha yangu na kutumaini milele”.

IRENE UWOYA AFANYIWA SHEREHE YA KUPONGEZWA

Irene Uwoya

MWIGIZAJI wa filamu ambaye jina lake limepitishwa nafasi ya ubunge viti maalumu Mkoa wa Tabora kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Irene Uwoya, amesema malezi aliyopewa na wazazi wake ndiyo yatakayomsaidia kuwa kiongozi bora. 

 Irene alisema hayo juzi katika hafla fupi iliyoandaliwa na wazazi wake kumpongeza kupitishwa katika nafasi hiyo ambapo pia marafiki zake wa karibu walihudhuria sherehe hiyo.

“Nisingekuwa hapa nilipofika kama wazazi wangu wasingenionyesha moyo na ushirikiano wa kutosha, najivunia kwani wamenisaidia kujenga moyo wa ujasiri ndani yangu na naamini nitawatendea haki kwa kuhakikisha ninakuwa kiongozi bora,” alisema Irene.

Irene alieleza kuwa lengo lake la kugombea nafasi hiyo ni kuhakikisha anaingia bungeni kuwatetea vijana wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali, hasa katika Mkoa wa Tabora.

SAUTI SOL KUTAFUTA WACHUMBA TANZANIA


KUNDI linalofanya vizuri na wimbo wao wa ‘Nerea’ kutoka nchini Kenya, Sauti Sol, limetangaza kutafuta wachumba wa kuoa nchini Tanzania, huku wakiwaomba radhi wasichana wa Kenya. 

“Samahani kwa wasichana wa nchini Kenya kutokana na maamuzi yetu ya kutaka kuoa huku Tanzania. Dar es Salaam. Kwa sasa tunatafuta warembo wa kuwaoa,” waliandika wasanii hao kupitia akauti yao ya Twitter. 

Wasanii hao kwa sasa wanafanya vizuri nchini humo na wamefanikiwa kuchukua tuzo mbalimbali nje ya nchi ya Kenya.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...