Tuesday, August 18, 2015

KIPINDU PINDU CHAZUKA DAR CHAUA WATU WAWILI


UGONJWA wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na watu wawili wamethibitika kufa.

Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni. Kutokana na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo kuwa zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1). Alisema watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine ni mwanamke na wanatoka Manispaa ya Kinondoni.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema ugonjwa huo umethibitika baada ya vipimo vya maabara vya watu hao, kuthibitisha. “Watu wawili akiwemo mwanamume na mwanamke wamefariki dunia baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha ugonjwa huo.

Hata hivyo, hakuna taarifa zozote za ugonjwa huo katika manispaa za Temeke na Ilala,” alisema Sadiki. Alisema endapo hali hiyo itaendelea kuwa mbaya, itabidi mamlaka za Dar es Salaam kusogeza mbele kampeni za kisiasa, zinazotarajiwa kuanza mwisho mwa wiki hii ili kuepusha mikusanyiko ya watu.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema wagonjwa wengine 30 wapo chini ya uangalizi maalumu katika hospitali za Mwanayamala na Sinza, ambapo 19 wapo Sinza na 11 Hospitali ya Mwananyamala.

Wengine wanne wameruhusiwa na kurudi nyumbani. “Sampuli za wagonjwa sita zilizochukuliwa, wanne kati yao wamethibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo,” alisema Natty.

Alisema wamepata dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo. Jitihada mbalimbali zinaendea kuchukuliwa ikiwemo kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Dk Jackson Makanjo, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula, na unapotoka chooni.

Alitoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuepuka kula ovyo vyakula vya mitaani. Alisema ugonjwa huo ulianzia eneo la Kwa Ali Maua huko Kijitonyama na kisha kuenea maeneo ya jirani ya Tandale, Manzese na Mwananyamala.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...