Saturday, May 24, 2014

ZIJUE KANUNI ZA SAYANSI ZA KUSAIDIA MTU KUISHI MAISHA MAREFU


Nyama nyekundu inaelezwa kuwa ni moja ya vyakula vinavyopunguza urefu wa maisha. 

Na Clifford Majani, Mwananchi


Kwa miaka mingi sana binadamu wa karne zote wamekuwa wakitafuta siri za maisha marefu, kuzuia uzee na hata kuzuia kifo. Lakini pamoja na jitihada nyingi mambo haya yameendelea kuwa changamoto kubwa kwenye maisha ya mwanadamu katika nchi mbalimbali duniani.  Kwa Tanzania, inakadiriwa kuwa umri wa kuishi kwa wanaume ni takriban miaka 58.2 na kwa wanawake ni miaka 60.5.
Muda huu wa kuishi ni mfupi sana ikilinganishwa na wenzetu katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani ambako wastani wa kuishi ni unakadiriwa kuwa ni miaka 78.2. Wanasayansi wamekuwa na nadharia nyingi kuhusu sababu zinazosababisha binadamu azeeke na kufa mapema. Ila wengi hufikiri kuwa tunazeeka mapema kutokana na sababu za maumbile na vinasaba tunavyorithi kwa wazazi wetu.
Wengine husema kuwa tunazeeka haraka kutokana na kuwa na mtindo usiofaa wa maisha. Mtaalamu wa Afya, Dk Mark Stibich  anasema kwamba kuzeeka haraka na kuishi maishi mafupi ni suala mtambuka na linahusisha mambo kama vile vinasaba, kemia, fiziolojia ya mwili pamoja na tabia zetu kwa mujibu wa makala yake ya Mei 10, 2014 liyowekwa kwenye tovuti ya longevity.about.com.
Mtaalamu wa maabara nchini Ujerumani, Dk James Vaupel anadai kuwa vinasaba huchangia kasi ya kuzeeka kwa asilimia tatu pekee na sehemu kubwa ya visababishi vya kuzeeka haraka hutokana na mtindo wa maisha usiofaa pamoja na lishe duni. Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Dk Vaupel anaongeza kusema kuwa tafiti nyingi zinaonyesha kuwa hata pacha wanaozaliwa siku moja, hupishana urefu wa maisha kwa karibu miaka 10 kutokana na kuwa na mitindo tofauti ya maisha.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wakazi wa maeneo wanaoishi maisha marefu zaidi duniani kama vile Japani, Italia na Marekani, pamoja na mambo mengine,  wanajiepusha na matumizi ya vileo, tumbaku na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu.
Pia huvuta hewa safi ya kutosha na kupata mapumziko ya kutosha baada ya kazi ngumu kila siku.
Watu hawa pia huwa na mtazamo chanya wa maisha, mazoezi na chakula asilia cha mimea kama vile mbogamboga na matunda kwa wingi. Vyakula vya asili vineelezwa  kuchangia kwa kiasi kikubwa matokeo ya watu kuishi miaka mingi kuliko wale ambao hawazingatii utaratibu huo.

Katika utafiti mmoja uliofanyika huko Japan, iligundulika kuwa chakula  chenye asili ya mimea kinaongeza ubora na urefu wa maisha. Katika utafiti huo, wanawake vikongwe 200 walioshiriki katika utafiti walithibitika kuwa katika kipindi cha juma moja, hutumia zaidi ya aina 100 za vyakula vyenye asili ya mimea.
Jambo lingine likaonekana kwamba wamekuwa wakifanya hivyo kwa kipindi kirefu cha maisha yao. Ripoti hii ni kwa mujibu wa Cook, G.C na Zumla A katika kitabu chao cha Manson’s Tropical Diseases, toleo la 21. Katika utafiti wa Dk Pan A na wenzake uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Archives of Internal Medicine, la Machi, 2012, inaonekana kuwa kula nyama nyekundu kwa wingi, hupunguza  umri wa kuishi.
Nyama yenye shida kubwa ni ile yenye mafuta mengi, nyama choma iliyoungua na ile iliyosindikwa.
Nyama ya namna hii huchangia kutokea kwa magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na saratani ya utumbo.
Hii inasababishwa na uzalishaji wa kemikali kama n-nitrosa na polycyclic aromatic hydrocarbons (PAHs) zinazodhuru afya. Ingawa jamii ya Wamasai wanakula nyama nyekundu kwa wingi, tafiti zinaonyesha kuwa wanatumia pia mitishamba (acacia goetzei na albizia anthelmintica). Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz
Pia hutumia vyakula vya mimea kwa wingi vikiwa katika uasilia wake, jambo ambalo huwapunguzia hatari itokanayo na nyama. Hilo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Johns T na wenzake walioufanya Ngorongoro mwaka 1999 na kuchapishwa katika jarida la dawa za asili lijulikanalo kama J. Ethnopharmacology. Katika utafiti mwingine uliofanywa na Dk Dean Ornish na madaktari wenzake wa Chuo Kikuu cha Califonia na San Francisco (UCSF), iligundulika kuwa mazoezi na mtindo bora wa maisha huimarisha afya ya vinasaba vya mwili vinavyohusika na kuzeeka vijulikanavyo kama telomeres.
Mazoezi yanaelezewa kuwa hufanya telomeres virefuke, hivyo kuongeza maisha. Telomeres zinapoathirika na kuwa fupi husababisha seli za mwili kudhurika na maisha kuwa mafupi. Utafiti huu ulichapishwa kwenye jarida la The Lancet Oncology la Septemba, 2013. Jambo jingine linalochangia kuwa na maisha marefu, ni uhusiano mzuri katika familia na jamii, kwa mujibu wa utafiti wa Rikke Lund wa Chuo Kikuu cha Copenhagen Denmark na wenzake katika jarida la Epidemiolojia na afya ya jamii mwaka 2014.
Wataalamu wengine wa masuala ya afya ya jamii wanaongeza kusema kuwa, uhusiano bora na mtazamo chanya katika maisha huongeza urefu wa maisha kwa miaka saba na nusu. Katika utafiti mwingine uliochapishwa katika jarida la tiba la Uingereza la British Medical, watafiti pia waligundua kuwa kutoelewana, ugomvi na mabishano ya mara kwa mara ya wanafamilia au wanandoa, huchangia watu kufa mapema zaidi.
Taarifa hii ilichapishwa katika mtandao wa kisayansi wa Science Daily la Mei 8, mwaka huu.
Kutokana na maelezo ya tafiti hizo, unaweza kubaini kuwa kuishi maisha marefu duniani, kunaweza kutegemea  mfumo wa maisha wa mtu pamoja na mazingira yake. Ukizingatia baadhi ya kanuni hizo za kitaalamu unaweza kuishi muda mrefu duniani.
Clifford Majani ni mmoja wa watafiti, Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Mbeya (NIMR-MMRC)
 Tafadhari Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...