Tuesday, October 29, 2013

MAGAZETI YA LEO JUMANNE OKTOBA 29, 2013

.
.
.

ASKARI ALIYEUAWA DRC ALIKUWA MBIONI KUFUNGA NDOA DESEMBA



Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani, katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (Monusco), Luteni Rajab Ahmed Mlima, alikuwa katika hatua za mwisho za kufunga ndoa.

Askari huyo aliuawa katika  uwanja wa mapambano na vikosi vya wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23, katika Milima ya Gavana, karibu na Goma, DRC- Congo wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani

Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk Aziz Mlima, alisema kuwa ndugu yake alikuwa tayari amekamilisha mipango yote na kilichokuwa kikisubiriwa ni siku ya kufunga ndoa hiyo.

“ Alikuwa yuko mbioni kufunga ndoa, lakini kwa sasa sitapenda kutaja jina la mchumba wake kwa kuwahayupo hapa lakini naye ni askari,” alisema Dk Mlima.

MWIGAMBA AZIDI KUANIKA MADUDU YA CHADEMA


*Awaonya wanaomwita msaliti
*Dk. Slaa aibua mapya

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, aliyesimamishwa uongozi asema atakichafua chama hicho kama ataendelea kuitwa msaliti.

Hatua hiyo, imekuja baada ya Mwigamba kukiri hadharani kusambaza waraka unaowatuhumu viongozi wa chama hicho katika mtandao wa Jamii Forum (JF), akitumia jina la Maskini Mkulima. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mwigamba aliwaonya viongozi wa Chadema wanaomwita msaliti. 
 
Alisema kama wanataka awe msaliti, yupo tayari kumwaga mambo yote hadharani, tena kwa ushahidi usio na shaka hata kidogo.

Mwigamba, aliyejiunga na Chadema mwaka 2004, akiwa mwanachama wa kawaida, alisema akiwa makao makuu mjini Dar es Salaam kama mhasibu mkuu wa chama, ndipo alipoanza kutambua udhaifu mkubwa wa kiuongozi ndani ya chama chake.

“Niliondoka pale makao makuu kwa mizengwe, kiongozi mmoja mkubwa kabisa alinifukuza kazi kwa kunipigia simu, tena baada ya kuwasiliana na Mkurugenzi wa Fedha,Anthony Komu akiwa nje ya Dar es Salaam na kumwagiza anifukuze,” alisema Mwigamba.

WAZIRI AANGUA KILIO MAHAKAMANI



ALIYEKUWA Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Arcado Ntagazwa, jana alijikuta akiangua kilio ndani ya kizimba, baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutamka yeye na wenzake wawili wameachiwa huru.
Ntagazwa alitokwa na machozi, mbele ya Hakimu Mkazi, Geni Dudu, alipokuwa akisoma hukumu katika kesi ya kujipatia tisheti 5,000 na kofia 5,000 za kumbukumbu ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, mwaka 2009 kwa njia ya udanganyifu.

“Ukiangalia ushahidi hapakuwa na udanganyifu katika kuagiza kuchapwa kwa tisheti na kofia, waliamini wangeweza kulipa fedha hizi, ukiangalia uhalisia wa tisheti hazikuwa za kibishara… zilikuwa za kugawa bure kwa wananchi, zilikuwa kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa kupiga vita rushwa na ufisadi, zilikuwa kama mabango.

“Ni kweli washtakiwa walihujumiwa na kushindwa kulipia gharama za uchapishaji, tayari nina shaka hiyo inatosha sana kuwaona washtakiwa si wakosaji, shaka hata ikiwa ndogo kiasi gani manufaa yanakuwa kwa washtakiwa.

“Kutokana na ushahidi na vielelezo vilivyopo mahakamani, naona washtakiwa hawana kosa, wako huru, mlalamikaji akafungie kesi ya madai ili aweze kupata haki yake,” alisema Hakimu Dudu na kutamka washtakiwa wako huru.

Ntagazwa, alianza kujifuta machozi yaliyokuwa yakibubujika akiwa kizimbani na hata baada ya kushuka kizimbani aliendelea kububujikwa na machozi, huku akitembea taratibu mno kuelekea nje ya jengo la mahakama.

Hakimu Dudu kabla hajafikia uamuzi wa kuwaachia huru washtakiwa, alisema katika ushahidi hapakuwa na ubishi washtakiwa walichapisha tisheti na kofia, ushahidi huo unasapotiwa na vielelezo kwamba kampuni mbili zilikubaliana kuingia mkataba huo.

Alisema upande wa Jamhuri ulileta mashahidi watano mahakamani kuthibitisha mashtaka hayo na kuomba katika majumuisho ya mwisho, kwamba washtakiwa watiwe hatiani kwani waliweza kuthibitisha makosa yao bila kuacha shaka.

YANGA, MGAMBO JKT KUVAANA TAIFA LEO

Yanga-Mgambo_d3a44.jpg
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Bara leo itashuka katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kupambana na Mgambo JKT katika mchezo wa raundi ya kumi na moja ya ligi hiyo.
Yanga inaingia uwanjani leo ikiwa na pointi 19 ilizopata katika mechi 10 ilizocheza huku ikiwa nafasi ya nne. Azam inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 23 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 20 huku zote zikiwa zimecheza mechi 10. Mbeya City ni ya tatu ikiwa na pointi 20 katika mechi 10.
Kwa upande wao, Mgambo wanaingai uwanjani wakiwa na pointi tano walizopata katika mechi 10. Timu hiyo inaburuza mkia katika ligi hiyo.
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya leo kutakuwa mchezo utakaozikutanisha timu mwenyeji za mkoa huo ambazo ni Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.


Raundi ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja huo huo.
Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...