Thursday, July 13, 2017

MABADILIKO MADOGO NDANI YA JESHI LA POLISI, MOHAMED MPINGA RPC MPYA MKOA WA MBEYA

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saimon Sirro,  amefanya mabadiliko ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi  Mohamed Mpinga anaenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Fortunatus Musilimu.

Aidha,  Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (DCP) Dhahiri Kidavashari amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi.

Uhamisho huo ni wa kawaida katika kuboresha utendaji wa kazi za Polisi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya Jeshi la Polisi.

TRA YAZIFUNGIA OFISI ZA SAHARA MEDIA KISA DENI LA BILLION 4.5

Ofisi za Kampuni ya Sahara Media Group inayomiliki kituo cha televisheni cha Star na cha redio cha Radio Free Africa (RFA) zimefungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa deni la Sh4.5 bilioni.

Ofisi hizo zimefungwa leo Alhamisi (Julai 13) na wakala wa TRA, Kampuni ya Sukah Auction Mart and Court Brokers ya jijini Mwanza.

Meneja utumishi na utawala wa Sahara Media Group, Raphael Shilatu amesema ni kweli wana malimbikizo ya madeni yanayotokana na kuhama kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali.

WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na kukabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa.

Amesema kati ya magari hayo, moja ni kwa hospitali hiyo ya wilaya na la pili litapelekwa katika Kituo cha Afya cha Mandawa.

Alikabidhi magari hayo jana alipotembelea hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema magari hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.

“Rais wetu Dk. John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono,” alisema.

Waziri Mkuu alisema magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa  wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.

Kabla ya kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama na ya  watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na akasema kwamba ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya, alisema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.

LOWASSA ATAKIWA KURUDI KWA DCI ALHAMISI IJAYO

Nusu saa baada ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kuwasili katika ofisi ya mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, kama alivyotakiwa kufanya Juni 29, ameruhusiwa na kutakiwa kurudi tena Alhamisi ijayo.

Mwanasheria wa Lowassa, Peter Kibatala amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Lowassa ametakiwa kurudi Alhamisi bila sababu za kuahirishwa kwa mahojiano hayo kuwekwa wazi.

“Hatujaambiwa kwa nini ila tumeambiwa tuje alhamisi ijayo kwa ajili ya maelekezo na kuwasikiliza zaidi,” alisema

SERIKALI YATANGAZA AJIRA 10, 000 KUZIBA PENGO LA WALIOGHUSHI VYETI

Ofisi ya  Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa vibali vya ajira 10,184 kwa mamlaka za serikali za mitaa, sekretarieti za mikoa, wakala za serikali na taasisi na mashirika ya umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amesema hayo leo katika kikao na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Mgawo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki

Ameongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgao wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuziwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi za wazi zilizojitokeza.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...