Mwanariadha wa Afrika Kusini ambaye ana ulemavu wa miguu na ambaye ni mashuhuri sana katika riadha ulimwenguni Oscar Pistorius, anatarajiwa kufika mahakamani leo kwa mara ya pili, ili kuwasilisha ombi la kuwachiwa kwa dhamana, baada ya kushtakiwa kwa kumuuwa mchumba wake.
 Waendesha mashitaka wanatarajiwa kupinga ombi lolote la dhamana katika kikao cha leo.
Kukamatwa kwa mwanariadha huyo wa Olimpiki ya walemavu mwenye umri wa miaka 29 kumewashangaza mamilioni ya watu ulimwenguni ambao walimwona kama shujaa aliyeweka kando ulemavu wake na kushindana na watu wasio na ulemavu katika Olimpiki.
Mpenzi wake, mwanamitindo Reeva Steenkamp alipatikana akiwa amepigwa risasi na kuuawa nyumbani kwa mwanariadha huyo mjini Pretoria mapema Alhamis iliyopita, huku ripoti za mwanzo zikisema Pistorius huenda alimdhania kuwa mwizi.
Hata hivyo polisi inasisitiza kuwa Steenkamp ambaye atazikwa leo, aliuawa na zaidi ya risasi moja, na Pistorius ndiye mshukiwa pekee na kwamba majirani walisikia vurugu hapo kabla.