Friday, August 18, 2017

MAPACHA WALIOSHIKANA WAFARIKI MUHIMBILI

Pacha walioshikana ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili mjini Dar es Salaam wamefariki kwa mujibu wa msemaji wa hospitali hiyo.

Pacha hao waliokuwa wakifanyiwa vipimo ili kuwaanda kwa upasuaji walifariki siku ya Jumanne kulingana na bi Neema Mwangomo. Watoto hao walizaliwa wilayani Kilosa katika eneo la Morogoro. Familia yao ilitoka katika kijiji cha Chaumbele.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Bi Mwangomo alisema kuwa wataalam watatoa maelezo katika wakati ufaao.

Pacha hao walioshikana chini ya kifua na tumboni walikuwa wakitumia ini moja na mishipa ya moyo lakini kila mmoja alikuwa na tumbo lake.

Awali daktari wa watoto Dkt Zaituni Bokhary alitumai kwamba pacha hao wanaweza kutenganishwa watakapofikisha umri wa miaka sita.

MUGABE: 'WALIOWAUA WAZUNGU HAWATASHITAKIWA'

Rais Robert Mugabe, ameuambia umati wakati wa sherehe za siku ya mashujaa jijini Harare Jumatatu wiki hii kuwa watu waliowaua wakulima wa kizungu wakati wa mabadiliko ya sheria ya ardhi nchini Zimbabwe hawatashtakiwa.

“Ndiyo, tuna wale waliouawa wakati wakipinga ukoloni. Hatuwezi kuwashtaki wale waliowaua wazungu. Je, tutawashtaki vipi?” alisema Mugabe.

Wakati wa ukoloni, ardhi nzuri ilitengwa kwa wazungu, lakini mwaka 2000, Mugabe aliongoza kutwaliwa kwa ardhi hiyo kutoka kwa wakulima 4,000 wa kizungu.

Rais Mugabe awali alikiri kuwa mifumo ya ardhi ya nchi hiyo ilishindwa na mwaka 2015 alisema: “Nafikiri mashamba tuliyowapa watu wetu ni makubwa, hawawezi kuyasimamia.”

Kutwaliwa ghafla mashamba kutoka kwa wakulima wazungu, inaonekana kuwa sababu kuu ya kuporomoka kwa uchumi wa Zimbabwe tangu mwaka 2000.

DANGOTE: 'NIKIINUNUA ARSENAL NITAMFUKUZA WENGER'

Mfanyabiashara tajiri raia wa Nigeria Aliko Dangote, ambaye anaorodheshwa kuwa mtu tajiri zaidi Afrika, amesema kuwa atamfuta kazi meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, ikiwa atafaulu kuinunua klabu hiyo ya Uingereza, kwa mujibu wa shirika la Bloomberg.

Wakati wa mahojiano na shirika hilo, Dangote alisema kuwa atajaribu kuinunua klabu hiyo, wakati ujenzi wa kiwanda chake cha kusafisha mafuta cha gharama ya dola bilioni 11 mjini Lagos utakapokamilika.

Bw. Dangote anasema amekuwa shabiki wa Arsenal tangu mwaka 1980.

Wenger ni mmoja wa mameneja wa kandanda wanaosifika sana barani Ulaya na hivi majuzi, alisaini mkataba wa miaka miwili na kuendelea kuwa na klabu hiyo kwa zaidi ya miongo miwili.

Kuna maoni tofauti kutoka kwa wafuasi wake, wengine wakisema kuwa klabu hiyo inahitaji meneja mpya ili kiweze kurejea hadhi yake.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...