Thursday, July 20, 2017

RAIS MAGUFULI ATOA SIKU 14 VITUO VYA MAFUTA KUFUNGA MASHINE ZA KIELEKRONIKI


Wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini Tanzania wamepewa siku 14 kufunga na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti la sivyo wafutiwe leseni.

Rais Magufuli, ambaye ametoa agizo hilo, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo ambazo kwa Kiingereza zinafahamika kama Electronic Fiscal Petrol Printer na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

"Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine, ndani ya siku 14," amesema Dkt Magufuli.

Mwishoni mwa wiki Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ilivifungia vituo vya mafuta kutokana kutotimiza vigezo baada ya kutofunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za mafuta.

WAZIRI MKUU AONYA MATAMSHI YA UCHOCHEZI


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali itawashughulikia watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.

Amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana, Julai 19, wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela.

Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

Tuesday, July 18, 2017

WATAKAOKAIDI MAFUNZO YA JKT KUKIONA

Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi amesema vijana ambao watakaidi wito wa kuhudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, watakuwa wamekaidi amri halali na majina yao yatapelekwa mamlaka za ajira kwa ajili ya hatua dhidi yao.

Kauli hiyo ameitoa wakati JKT ikiendelea na mchakato wa kufufua kambi tano nchini ili kufanikisha uwezeshaji wa vijana wanaomaliza elimu ya juu ya sekondari kujiunga na jeshi hilo kwa kujitolea na kwa mujibu wa sheria.

Awali, ilikuwa lazima kwa wahitimu wa elimu ya juu ya sekondari na vyuo kujiunga na mafunzo ya mwaka mmoja  JKT kabla ya kuendelea na masomo au kuanza ajira, na baadaye muda ukapunguzwa.

TUNDU LISSU: “SIPENDI KUKAMATWA, MAHABUSU SI PAZURI”

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema hapendi kukamatwa na vyombo vya dola kwa kuwa mahabusu si mahala pazuri pa kuishi watu hususan wasiokuwa na hatia, hata hivyo amesema kitendo hicho hakitamuogofya na kuzuia harakati zake za kupaza sauti.

Lissu ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari kuhusu matukio ya baadhi ya viongozi na wafuasi wa Chadema kukamatwa na vyombo vya dola, na kuwekwa mahabusu.

“Sipendi kukamatwa mahabusu si pazuri, lakini inafikia hatua inabidi uamue kama kwenda machinjioni ukiwa umenyamaza kimya au kuingia huku unapiga kelele mataifa yasikie,” amesema.

Lissu ambaye mpaka sasa ana kesi za jinai takribani nne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikiwemo ya uchochezi, amedai kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wako katika hali ya hofu katika utendaji kazi wao, huku akiwataka wananchi kupaza sauti ili hali hiyo iondolewe.

“Hofu kila mahali, mahakamani na hata kwenye utumishi wa umma hakuna aliyeko salama. Viongozi wa dini wako kimya wanadhani wako salama. Tunahitaji kupaza sauti kila mmoja kwa nafasi yake,” amesema.

WANA CCM 202 WAJITOKEZA KUWANIA UONGOZI KIBITI

Wanachama 202 wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wilayani hapa, mkoani Pwani.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, jana Jumatatu Julai 17, Katibu wa CCM wilayani hapa, Zena Mgaya amesema idadi hiyo ni nje ya idadi ya Wana CCM waliochukua fomu za kugombea nafasi za uongozi wa Kata,Shina na Tawi.

Zena amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa za mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama hicho, bado mwitikio wa wanachama kuchukua fomu umekuwa wa kuridhisha hasa kuanzia ngazi ya kata na wilaya.

Thursday, July 13, 2017

MABADILIKO MADOGO NDANI YA JESHI LA POLISI, MOHAMED MPINGA RPC MPYA MKOA WA MBEYA

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Saimon Sirro,  amefanya mabadiliko ya Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi  Mohamed Mpinga anaenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, na nafasi yake inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Fortunatus Musilimu.

Aidha,  Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya (DCP) Dhahiri Kidavashari amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi.

Uhamisho huo ni wa kawaida katika kuboresha utendaji wa kazi za Polisi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo ya Jeshi la Polisi.

TRA YAZIFUNGIA OFISI ZA SAHARA MEDIA KISA DENI LA BILLION 4.5

Ofisi za Kampuni ya Sahara Media Group inayomiliki kituo cha televisheni cha Star na cha redio cha Radio Free Africa (RFA) zimefungwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa deni la Sh4.5 bilioni.

Ofisi hizo zimefungwa leo Alhamisi (Julai 13) na wakala wa TRA, Kampuni ya Sukah Auction Mart and Court Brokers ya jijini Mwanza.

Meneja utumishi na utawala wa Sahara Media Group, Raphael Shilatu amesema ni kweli wana malimbikizo ya madeni yanayotokana na kuhama kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali.

WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na kukabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa.

Amesema kati ya magari hayo, moja ni kwa hospitali hiyo ya wilaya na la pili litapelekwa katika Kituo cha Afya cha Mandawa.

Alikabidhi magari hayo jana alipotembelea hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema magari hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.

“Rais wetu Dk. John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono,” alisema.

Waziri Mkuu alisema magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa  wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.

Kabla ya kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama na ya  watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na akasema kwamba ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya, alisema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.

LOWASSA ATAKIWA KURUDI KWA DCI ALHAMISI IJAYO

Nusu saa baada ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa kuwasili katika ofisi ya mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, kama alivyotakiwa kufanya Juni 29, ameruhusiwa na kutakiwa kurudi tena Alhamisi ijayo.

Mwanasheria wa Lowassa, Peter Kibatala amezungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa Lowassa ametakiwa kurudi Alhamisi bila sababu za kuahirishwa kwa mahojiano hayo kuwekwa wazi.

“Hatujaambiwa kwa nini ila tumeambiwa tuje alhamisi ijayo kwa ajili ya maelekezo na kuwasikiliza zaidi,” alisema

SERIKALI YATANGAZA AJIRA 10, 000 KUZIBA PENGO LA WALIOGHUSHI VYETI

Ofisi ya  Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa vibali vya ajira 10,184 kwa mamlaka za serikali za mitaa, sekretarieti za mikoa, wakala za serikali na taasisi na mashirika ya umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amesema hayo leo katika kikao na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Mgawo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki

Ameongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgao wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuziwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi za wazi zilizojitokeza.

Wednesday, July 12, 2017

DIWANI MWINGINE WA CHADEMA ARUSHA, AJIUZULU LEOHali si shwari tena ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, baada ya diwani mwingine wa chama hicho, Japhet Jackson kuandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM.

Diwani huyo ni wa saba kujiuzulu ndani ya mwezi mmoja, katika Jimbo la Arumeru Mashariki na Jimbo la Arusha mjini, majimbo ambayo wabunge wake ni Joshua Nassari na Godbless Lema.

Jackson amewasilisha barua leo mchana ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Christopher Kazeri na kueleza anamuunga mkono Rais John Magufuli.

KLABU YA EVERTON YAWASILI NCHINI, WAYNE ROONEY YUMO.

Klabu ya Everton tayari imewasili Jijini Dar es Salam asubuhi ya leo ikitokea nchini Uingereza nakupokelewa na Waziri wa Habari Dr. Harrison Mwakyembe, huku ikiwakosa wachezaji wake watatu muhimu katika kikosi hicho kutokana na majeruhi waliyokuwa nayo.

Pamoja na hayo, timu ya Everton imeongozwa na mchezaji nyota Wayne Rooney pamoja na Davy Klaassen na Michael Keane ambao pia wamejiunga na klabu hivi karibuni.

 Like page yetu ya facebook/jambotz pia tu-follow Instagram @jambotz.

Tuesday, July 11, 2017

DIWANI WA CHADEMA ARUSHA AJIUZULU NA KUMUUNGA MKONO MAGUFULI

Diwani wa Ngabobo (Chadema), Solomon Laizer ameandika barua ya kujiuzulu udiwani na kujiunga na CCM kwa maelezo anamuunga mkono Rais John Magufuli.

Laizer ni diwani wa tano katika Halmashauri ya Meru kujiuzulu kwa kutoa sababu kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri amethibitisha leo (Julai 11) kupata taarifa za kujiuzulu kwa Ngabobo.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amesema kujiuzulu kwa diwani huyo ni mchezo mchafu akidai  amenunuliwa.

Wednesday, July 05, 2017

MSHINDI WA KUCHORA NEMBO YA EAC KUNYAKUA KITITA CHA DOLA 25,000

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, imewataka vijana wenye uwezo wa kubuni na kuchora kujitokeza kushiriki shindano la kubuni nembo mpya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Msemaji wa wizara hiyo,  Mindi Kasiga amesema shindano hilo ni fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao, pia kujipatia kipato iwapo watashinda. 

Shindano hilo limeanza Juni Mosi na mwisho ni Agosti 31.

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...