Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Ndugu Samson Mwigamba amesimamishwa nafasi ya uongozi hiyo mara moja kuanzia leo na Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini, huku taratibu zingine za kinidhamu zikiendelea kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na taratibu za chama.

Kikao hicho kimechukua hatua hizo mara moja baada ya Ndugu Mwigamba kukiri kwa maandishi kuwa ameandika kwa kutumia jina bandia na kutuma kwenye mitandao ya kijamii, kutoa tuhuma za uongo na kupotosha umma dhidi ya chama na viongozi, kinyume na katiba, kanuni, maadili, miongozo na taratibu za chama.

Hatua hiyo ya kukiri na kusimamishwa uongozi, ilifuatia baada ya Ndugu Mwigamba kutuhumiwa kusambaza katika mitandao tuhuma za uongo, upotoshaji na uchonganishi, ambapo kikao kilimwagiza kusalimisha kompyuta yake ili wataalam wa masuala ya IT wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, waweze kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.