Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema
Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu
la Katiba imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba
ya mageuzi.
Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya
viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na
muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na
wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika
Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu
kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam
jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa
na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.
“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda
Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge
Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa
kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza
kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka
kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato
ukaanza upya.”
Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati
yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha
ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.
Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni
Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi,
Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa
kuwa si mambo ya muungano.
Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili
kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu
uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia
saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu
iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la
Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa
watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea
mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.
Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili
kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo
kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba
alisema, “Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata
mimi nimeanza kukata tamaa.”
Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu
waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila
mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini
waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya
Katiba wanayoitaka.
Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba pia
alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi
anapumua Katiba’. Dk Mvungi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja
wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini
alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani
kwake.
Maadili ya Viongozi wa umma
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma alisema,
“Wananchi walitoa maoni mazito kuhusu maadili ndani ya jamii na maadili
ya viongozi. Kutokana na maoni ya wananchi Tume iliimarisha misingi
mikuu ya taifa iliyo katika Utangulizi wa Rasimu. Misingi iliyo katika
katiba ya sasa ni uhuru, haki, udugu na amani.”
Alisema kutokana na maoni ya wananchi misingi
mipya iliongezwa ambayo ni; utu, usawa, umoja na mshikamano na kwamba
wananchi pia walipendekeza tunu za taifa ziwekwe kwenye katiba ambazo ni
utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa
(Kiswahili ).
“Bunge Maalumu limeondoa uadilifu, uzalendo,
umoja, uwazi, na uwajibikaji kutoka kwenye orodha ya tunu za taifa na
kuziweka kwenye misingi ya utawala bora. Kila Mtanzania anatakiwa awe
mzalendo, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mwadilifu, kila Mtanzania
anatakiwa aenzi umoja. Inakuwaje mambo haya yahusu utawala tu?” alihoji.
Alisema tunu za taifa ndiyo msingi wa utamaduni na
maadili ya taifa, kwamba mwelekeo wa taifa utategemea jinsi wananchi
wanavyoenzi misingi mikuu na tunu.
Aliponda kitendo cha Bunge la Katiba kutoweka
miiko ya uongozi kwenye Katiba wakati kila siku viongozi wanalalamika
juu ya rushwa na ufisadi, pamoja na fedha za umma kuwekwa kwenye akaunti
za benki nje ya nchi.
“Katika bara la Afrika, nchi kama Afrika Kusini,
Namibia na Kenya zimeweka misingi ya maadili na miiko katika Katiba.
Hapa kwetu sheria tulizonazo haziwezi kupambana na rushwa na ufisadi.
Sijui kwa nini Bunge la Katiba wameondoa hili,” alisema.
Madaraka ya Wananchi
Jaji Warioba alipinga kitendo cha Bunge la Katiba
kuondoa kipengele cha wananchi kuwa na madaraka ya kumwondoa mbunge wao
kama hawaridhishwi na uwakilishi wake bungeni, mbunge kutokuwa waziri
ili aweze kuwawakilisha vizuri na ukomo wa mbunge kuwa vipindi vitatu .
“Bunge lina kanuni za kuwawajibisha wabunge na
wananchi nao wanapenda kuwa na madaraka hayo. Vyama vya siasa vina
madaraka ya kuwaondoa wabunge wao katikati ya kipindi. Wananchi nao
wanataka watumie madaraka yao,” alisema.
Mgawanyo wa madaraka
Akizungumzia mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili
ya Bunge, Serikali na Mahakama, alisema pendekezo lao la kumwondoa rais
na mawaziri kutoka kwenye Bunge linakataliwa kwa sababu nchi imezoea
mfumo wa kibunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za jumuiya ya madola.
“Siyo kweli kwamba mfumo wetu ni wa kibunge. Kwenye mfumo wa
kibunge mkuu wa nchi hana madaraka ya utendaji. Madaraka hayo yako
mikononi mwa Waziri Mkuu ambaye ni mbunge. Hivyo ndivyo ilivyo kwa
Uingereza, India, Canada, Australia, New Zealand,” alisema.
Akitolea mfano mwingiliano huo alisema wakati wa
kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, bunge lilitunga sheria lakini
baadaye Rais alifanya mazungumzo na watu nje ya bunge na baadaye bunge
likalazimika kubadili uamuzi.
“Tanzania ina mfumo wa urais ambapo rais ni mkuu
wa nchi, mtendaji mkuu na amiri jeshi mkuu. Rais na mawaziri wake kuwa
sehemu ya bunge ni kuchanganya mamlaka. Hali hii inafanya Serikali
kuingilia mamlaka ya bunge na pia bunge kuingilia mamlaka ya Serikali,”
alisema.
Aliongeza, “Nchi nyingi zimebadili Katiba zao ili
kutenganisha madaraka ya mihimili. Jirani zetu wa Msumbiji na Kenya
wamefanya hivyo. Kenya imefanya hivyo na sababu zao zinafanana kabisa na
zile ambazo wananchi wa Tanzania walitoa.”
Muungano
Huku akitaja kero 20 za muungano, 11 za Zanzibar
na 10 za Tanzania Bara zilizotajwa na wananchi wakati wa kukusanya
maoni, Jaji Warioba alisema, “Ingawa Rasimu ya Bunge Maalumu limerudisha
madaraka ya rais kuigawa nchi hiyo peke yake haitoshi. Mambo haya ni
magumu kubadilika kwa upande wa Zanzibar.”
Aliongeza kuwa ili kufanya mabadiliko kwenye
Katiba ya Zanzibar ni lazima mabadiliko yapitishwe kwa theluthi mbili au
zaidi ya Wawakilishi. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
No comments:
Post a Comment