Saturday, September 27, 2014

UKAWA WASEMA JK, CCM HAWAELEWEKI



 
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umesema kuwa Rais Jakaya Kikwete na CCM hawaeleweki ukidai ni kutokana na kukiuka makubaliano yao kuhusu kuendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.

Umoja huo pia umedai kwamba Mahakama Kuu ya Tanzania imeshindwa kutoa uamuzi fasaha kuhusu tafsiri ya kisheria ya mamlaka ya Bunge hilo katika kurekebisha Rasimu ya Katiba kwa kuogopa lawama kutoka Ukawa na CCM.

Ukawa unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, DP, NLD na NCCR-Mageuzi ulieleza hayo jijini hapa jana ulipozungumzia Mchakato wa Katiba ulipofikia, hasa baada ya Bunge hilo kufanya marekebisho ya kanuni kwa wajumbe wake kuruhusiwa kupiga kura kwa njia ya mtandao.

Mwenyekiti mwenza wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa makubaliano ya kusitishwa kwa Bunge hilo kati yao na Rais Kikwete yameshindwa kutekelezwa, jambo ambalo wanashindwa kuelewa sababu zake. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

“CCM na Rais Kikwete hawaeleweki, tulikubaliana liahirishwe, tufanye marekebisho katika Katiba ya sasa hasa uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi, mshindi wa urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura. Lakini, hatuelewi imekuwaje, Bunge linaendelea sasa tunashindwa kumwelewa,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Tunaitaka Serikali na Rais Kikwete wasiingize nchi hii katika machafuko. Wasiwajengee utamaduni Watanzania wa kufanya mapambano yasiyo rasmi. Ukizuia watu kufanya harakati zao za siasa, unawafundisha kufanya mbinu zingine. Tusifikie huko.”

Akinukuu kauli ya Rais wa Kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliyoitoa mwaka 1964 alipohukumiwa kifungo cha maisha gerezani alisema: “Utawala wowote unaotumia majeshi na vyombo vyake vya dola kuzima sauti ya raia wake, unafundisha raia hao namna ya kutafuta mbinu nyingine tofauti ya kupambana na utawala huo.”

Akifafanua kauli hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema kuwa miaka miwili na nusu imepita sasa tangu walipozuiwa kufanya maandamano kupaza sauti na kilio chao, lakini CCM wanaruhusiwa.

Alisema kwamba wakati yeye akizuiwa kufanya ziara katika jimbo lake la uchaguzi la Hai, wabunge wa upinzani wa Arusha, Mwanza na maeneo mengine wakiendelea kutoruhusiwa kufanya mikutano, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana anaendelea na mikutano na ziara katika mikoa ya Pwani na Tanga.

Mbowe aliongeza: “Hawa polisi wanaosema hawana uwezo wa kulinda mikutano yetu, leo wana uwezo mkubwa wa kuzuia mikutano yetu. Tunapoelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, kama CCM hawatabadili mbinu zingine, hakika...hakika wanawafundisha Watanzania kubuni njia mbadala ya kupinga uonevu huu.”

Awali, akisoma tamko la Ukawa juu ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema kuna mgongano katika maana ya maneno yaliyotumika kwenye kifungu cha 25 cha Sheria hiyo kwenye toleo la Kiingereza la sheria hiyo.

Hata hivyo, licha ya mgongano huo, tafsiri sahihi ya maneno ya kifungu hicho ni kwamba; mamlaka ya ‘kujadili na kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa’ maana yake ni mamlaka ya kutunga na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa ajili ya kupelekwa kwa wananchi wa Tanzania ili kupigiwa Kura ya Maoni.”

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema kuwa ilivyokuwa kwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu iliyohusu mgombea binafsi, Mahakama Kuu ya Tanzania imekwepa kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki kwa kufuata Katiba na Sheria za nchi kwa kujificha nyuma ya kichaka cha ‘uamuzi wa kisiasa.’
Naye Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Sitta anatutia aibu Watanzania kwa kupitisha mambo ya ajabu ajabu...kwamba  kura ya kupitisha Katiba itapigwa kwa email, fax na itaweza kupigwa hata kwa simu watu wakiwa bar, guest. Halafu wanabadilisha tena kanuni kwamba kura itapigwa kwa sura, si kwa kifungu. Hii ni kuhalalisha mabilioni batili ya fedha wanayokula bila faida yoyote baadaye.”
Aliongeza: “Tatizo letu katika nchi yetu kuna ombwe la uongozi, Rais Kikwete alikuwa anaunga mkono Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, lakini walipomtisha wenzake akaogopa. Ndiyo maana leo hii hayupo nchini huku nchi ikiwa katika kipindi muhimu.”
Alisema, “Tumeshawaeleza kwamba theluthi mbili haitapatikana hasa Zanzibar lakini hawasikii, Sitta anasimamia mambo anavyojua yeye. Ni wakati wa Watanzania kusimama kidete kupigania Katiba bora inayokubalika na makundi yote.”
Chadema waandamana Dar
Katika hatua nyingine, Polisi jijini hapa jana walizima maandamano ya wafuasi wa Chadema Jimbo la Ubungo waliokuwa wakiandamana kupinga Bunge la Maalumu la Katiba linaloendelea Dodoma.
Kabla ya kuanza kwa maandamano hayo yaliyoanzia kwenye ofisi za Chadema Tawi la Kimara Korogwe, wafuasi hao walipeana mbinu za kufanya endapo Polisi wangetokea kuwasambaratisha.
Wakiwa na mabango yenye maandishi mbalimbali ya kupinga Bunge hilo na fedha zilizotumika kuliendesha, walikubaliana kuwa endapo Polisi wakitokea na kumkamata mmojawao, wote wangeingia kwenye gari la polisi.
Saa 8:45 asubuhi maandamano yalianza kuelekea katikati ya jiji, huku baadhi ya wafuasi hao wakisikika kuwalaumu madereva wa bodaboda waliokuwa wakiogopa kujiunga kwenye msafara.
Akizungumza baada ya maandamano hayo, Justine alisema kuwa lengo lao limetimia kwa kuwa walitaka viongozi wa serikali wajue kwamba kuna watu hawakubaliani na kinachoendelea kwenye Bunge Maalumu.
Kamanda
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kuwa kuna watu walikuwa wameingia barabarani kwa ajili ya kuandamana eneo la Kimara Korogwe saa 3:00 asubuhi.

Alisema kuwa kundi hilo lilitawanyika baada ya kuwaona polisi wakienda sehemu waliyokusanyika lakini haikuweza kufahamika mara moja kama watu hao walikuwa ni wafuasi wa Chadema au la. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...