Thursday, May 18, 2017

SERENGETI BOYS YAWASHIKISHA ADABU WAANGOLA KATIKA MICHUANO YA AFCON U17

Serengeti Boys imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza kwenye michuano ya AFCON U17 baada ya kuifunga Angola kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa Kundi B uliochezwa jioni ya leo Alhamisi Mei 18, 2017.

Vijana wa Serengeti Boys ndio walikua wa kwanza kupata bao la kuongoza dakika ya sita kipindi cha kwanza baada ya Kelvin Naftal kupasia kamba kwa kichwa akiunganisha krosi ya Nickson Kibabage.

Dakika ya 18 Angola walisawazisha bao hilo kupitia kwa Pedro baada ya kutumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Serengeti Boys na kufanya timu zote kwenda mapumziko zikiwa sare kwa kufungana 1-1.

Kipindi cha pili Serengeti waliongeza kasi kutafuta bao na kufanikiwa kufunga dakika ya 69 mfungaji akiwa ni Abdul Suleiman baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Yohana Mkomola. Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania.

SHILOLE AWATAJA DIAMOND, ZALI KWENYE KESI YAKE

 
MSANII wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed ‘Shilole’, ameieleza mahakama jinsi mwanafunzi wa Chuo cha Bandari, Thomas Lukas, alivyokuwa akitumia mtandao wa kijamii wa Instagram kutuma meseji za matusi ya nguoni kwa watu mbalimbali.

Shilole alitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni mbele ya Hakimu, Boniface Lihamwike.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Tumaini Mfikwa, Shilole alidai shughuli zake ni muziki na anatambulika kwa jina la Shilole ama Shishi baby.

Shilole: Mheshimiwa mimi nafanya kazi sehemu nyingi hasa kwenye Instagram, WhatsApp, Facebook na Twitter…, nipo kwenye mitandao hiyo tangu nilipokuwa superstar miaka mitano iliyopita.

Alieleza Shilole huku akidai kwamba mwaka jana alipokea simu za watu tofauti wakiwemo wasanii wenzake na mashabiki wake wakimlalamikia kuhusu meseji za matusi anazowatumia kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Shilole: Yaani mimi kama mwanamke nilidhalilishwa sana na hayo matusi, mheshimiwa Hakimu ukitaka nayataja hapa.
Hakimu: Subiri…
Shilole: Ndipo nikaamua kwenda kituo cha Polisi Osterbay kuonyesha jinsi mtuhumiwa alivyotumia jina langu vibaya.

Hata hivyo, alipotakiwa na Wakili wa utetezi, Julias Kamote na Christina Roman ataje baadhi ya majina ya wasanii waliomlalamikia, aliwataja kwamba ni Queen Darlin, Diamond, Zali, Ant Ezekiel na Harmonize mwingine ni mtangazaji, Efrahim Kibonde.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 6, mwaka huu na mtuhumiwa yupo nje kwa dhamana.

TRUMP AIMWAGIA TANZANIA FEDHA ZA KUPAMBANA NA UKIMWI

Serikali ya Marekani kupitia mpango wa dharura wa Rais wa nchi hiyo wa kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), umeidhinisha Dola 526 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja ujao kwa ajili ya kukabiliana na VVU na Ukimwi nchini.

Msaada huu utaongeza idadi ya Watanzania wanaopatiwa matibabu ya kufubaza VVU kufikia milioni 1.2.

Pia utaimarisha mapambano dhidi ya VVU kupitia huduma za upimaji, matibabu, kufubaza na kuzuia maambukizi ili hatimaye kufikia lengo la kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.

Taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini imesema fedha hizo zitafadhili miradi inayotekelezwa chini mpango wa utekelezaji wa  Pepfar utakaoanza kutekelezwa Oktoba hadi Septemba 2018, na ni ongezeko la asilimia 12.3 ya bajeti ya mwaka jana.

Bajeti iliyotengwa inajumuisha pia utoaji wa huduma na matibabu kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi pamoja na kukabiliana na ukatili wa kijinsia.

Pepfar pia itasaidia mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume, walengwa wakiwa 890,000.

Mpango huu unaendeleza ubia wa muda mrefu kati ya Marekani na Tanzania katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na muongo mmoja wa ushirikiano uliowezesha kudhibiti kwa mafanikio maambukizi ya VVU.

Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Virginia Blaser alisema, “Kwa pamoja tunafanya kazi ili hatimaye kuwa na kizazi kisicho na Ukimwi Tanzania – ambacho hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma.”

MWILI WA MTOTO ALIEPOTEA, WAKUTWA HAUNA MACHO, ULIMI NA MENO MAWILI

Mtoto Felister Isack Skali (7) pichani, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chekechea katika Shule ya msingi Mwagala Mbuyuni Wilaya ya Songwe Mkoa wa Songwe aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu mei 11 mwaka huu, mwili wake umekutwa porini ukiwa hauna baadhi ya viungo kama ulimi, macho na meno mawili ya chini.

Akithibitisha kupatikana kwa mwili wa marehemu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni Athanas Hamis amesema alipata taarifa kutoka kwa wachungaji wa mifugo ambapo alifika eneo la tukio jioni na wanachi kulazimika kulinda mwili hadi asubuhi walipofika askari Polisi wa kituo cha Galula na Daktari na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kisha mazishi kufanyika jana.

Tukio hilo ni la kwanza kutokea katika kijiji cha Mbuyuni ambalo linahusishwa na imani za kishirikina.

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...