Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Ndugu Samson Mwigamba amesimamishwa nafasi ya uongozi hiyo mara moja kuanzia leo na Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini, huku taratibu zingine za kinidhamu zikiendelea kwa kufuata katiba, kanuni, maadili, miongozo na taratibu za chama.

Kikao hicho kimechukua hatua hizo mara moja baada ya Ndugu Mwigamba kukiri kwa maandishi kuwa ameandika kwa kutumia jina bandia na kutuma kwenye mitandao ya kijamii, kutoa tuhuma za uongo na kupotosha umma dhidi ya chama na viongozi, kinyume na katiba, kanuni, maadili, miongozo na taratibu za chama.

Hatua hiyo ya kukiri na kusimamishwa uongozi, ilifuatia baada ya Ndugu Mwigamba kutuhumiwa kusambaza katika mitandao tuhuma za uongo, upotoshaji na uchonganishi, ambapo kikao kilimwagiza kusalimisha kompyuta yake ili wataalam wa masuala ya IT wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, waweze kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.



Wataalam hao wa masuala ya IT, wakitumia ushahidi uliokuwa katika bandiko hilo, hasa jina la kiongozi huyo, walibaini pasi na shaka kuwa andiko lililosambazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwa kutumia jina bandia liliandikwa na kuhifadhiwa kwenye kompyuta ya Mwigamba kisha kupostiwa leo.

Ndugu Mwigamba ametuhumiwa kusambaza andiko hilo akiwa katikati ya kikao, baada ya amemaliza kuwasilisha taarifa ya hali ya chama katika mkoa wake wa Arusha, ambapo alikisifia chama na uongozi wa taifa kwa kutekeleza maagizo ya vikao vya chama na kubuni mipango na mikakati mbalimbali ya kukiendesha chama ili kuiondoa CCM madarakani.

Kikao hicho cha Baraza la Uongozi, chini ya uenyekiti wa Mh. Israel Natse, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini (Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Arusha), kiliazimia kwa kauli moja kumsimamisha Mwigamba, huku taratibu zingine za kushughulikia masuala ya kinidhamu zikifuata.