Thursday, July 13, 2017

SERIKALI YATANGAZA AJIRA 10, 000 KUZIBA PENGO LA WALIOGHUSHI VYETI

Ofisi ya  Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetoa vibali vya ajira 10,184 kwa mamlaka za serikali za mitaa, sekretarieti za mikoa, wakala za serikali na taasisi na mashirika ya umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, amesema hayo leo katika kikao na watumishi wa umma wa Wilaya ya Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

“Mgawo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki

Ameongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgao wa nafasi za ajira 4,816 zilizosalia unaendelea ili kuziwezesha wizara na taasisi nyingine zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri watumishi wapya kuziba nafasi za wazi zilizojitokeza.



Waziri Kairuki amesema Serikali imetoa vibali ili kuajiri  watumishi wapya 15,000 watakaoziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti.

Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo  wanatarajiwa kuripoti kazini kuanzia Agosti mwaka huu.

Aidha Kairuki amesema kuwa utaratibu wa ajira mpya bado uko pale pale hivyo amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wa ajira hizo.

“Napenda nisisitize kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile vinavyoziba pengo la walioghushi vyeti, naomba wananchi watambue kuwa suala la ajira mpya bado liko palepale kama Serikali ilivyopanga,’’amesema Kairuki.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...