Jana
na leo, Serikali imeona kuzuka kwa tabia ya uvunjaji wa kanuni ya
utunzaji wa siri za taarifa za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa
huduma za simu za mkononi. Taarifa hizo zimefikia hatua ya kuchapishwa
katika vyombo vya habari kwa kutaja bila idhini yao, namba za simu,
wahusika wa namba hizo, maongezi na muda wa mawasiliano Kati yao. Jambo
hili ni Kosa la Jinai. Mfano; tamko la Chadema lililotolewa na Ndugu
Mabare Marando Mjini Dar es Salaam tarehe 14/04/2013.
Serekali inapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wenye makampuni ya
Simu, Vyombo vya Habari na wananchi kwa ujumla kuwa, kutoa taarifa za
mawasiliano binafsi ya simu baina ya watumiaji wa huduma hiyo, ni
uvunjaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Na. 3 ya
mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano (Kulinda Wateja) za mwaka 2005.
Kifungu cha 98 ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta
kinasema;
“Mtu yeyote ambaye ni mfanyakazi wa kampuni yenye leseni ya kutoa
huduma za mawasiliano, au mwakilishi wake, ana wajibu wa kutunza siri za
mawasiliano binafsi na taarifa zozote za siri za wateja kwa mujibu wa
sheria hii”. Aidha, “Mtu yeyote haruhusiwi kutoa taarifa binafsi za
mteja yeyote alizopokea au kusikia kwa mujibu wa sheria hii isipokuwa tu
mtu huyo ameruhusiwa kwa mujibu wa sheria”
Kanuni ya 12 ya Kanuni za Mawasiliano za mwaka 2005 za Tanzania
(Kulinda Wateja) inasema:-
“Mtoa huduma za Mawasiliano haruhusiwa kuingilia kati, kusikiliza au
kutoa taarifa zozote za mazungumzo ya mteja yeyote yaliyopitia kwenye
mtandao wa mtoa huduma, isipokuwa kwa ruhusa kulingana na mahitaji
maalumu kwa mujibu wa sheria zilizopo”
Hivyo
basi wananchi wanapewa tahadhari kuhusu kutafuta au kutaka kupata
taarifa za mawasiliano ya siri kutoka kwa watoa huduma na kuzitumia
taarifa hizo binafsi za mawasiliano pasipo kufuata utaratibu
ulioruhusiwa kisheria.
Aidha Serikali inapenda kuwatoa wananchi hofu kuwa Mawasiliano yao
(maudhui) hayapaswi kuingiliwa kwa kusikilizwa mazungumzo yao au kusomwa
meseji zao katika mitandao ya simu. Serikali Kwa kutumia vyombo vyake
vya usalama inawahakikishia wananchi kuwa haki zao za faragha katika
mawasiliano zinalindwa Kwa Mujibu Wa Sheria Na. 3 ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010 pamoja Na Kanuni zake.
Kwa taarifa ambazo zimechapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari
hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano pamoja na taasisi nyingine husika
kwa mujibu wa Sheria ya EPOCA pamoja na Kanuni zake, wanaelekezwa
kufanya uchunguzi wa uvunjwaji huo wa sheria na Mamlaka husika zichukue
hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuvunja sheria hiyo.
Serikali inayakumbusha Makampuni ya simu, Vyombo vya Habari na wananchi
kwa ujumla kuhakikisha siri za mazungumzo binafsi ya wateja
zinahifadhiwa na hazitolewi kwa yeyote isipokuwa kwa mujibu wa sheria.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo
16 April 2013
No comments:
Post a Comment