Saturday, February 16, 2013

Balozi Seif Idd aitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kuhamasishana kuanzisha miradi ya kijamii.


Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Taifa ya Mfuko wa  Jamii (NSSF) Kanda ya Dodoma Bibi Maryam Ahmed akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kumsajili rasmi kuwa mwanachama wa Mfuko huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijaza Fomu Maalum ya kuomba uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii ( NSSF) Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
 Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliofika Ofisini kwake Vuga kumsajili rasmi kuwa mwanachama wa mfuko huo.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kitope Bibi Halima Bushir Abeid mchango wa Shilingi 100,000/- kwa ajili ya ulipaji huduma ya umeme ya kituo hicho mbaleni Jimboni humo.
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania (NSSF) umeombwa kufanya utaratibu wa kuishawishi mifuko mingine ya Jamii kuanzisha  miradi ya Jamii ili kuongeza pato la wanachama pamoja na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  wakati akijaza fomu maalum ya kuomba kujiunga kuwa mwanachama rasmi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) shughuli ambayo aliifanya Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif amesema Mfuko huo umeonyesha mwanga na matumaini makubwa kwa wanachama wake hasa kutokana na miradi mingi iliyoianzisha ambayo kwa asilimia kubwa inalenga kuwanufaisha wanachama wake hasa wale wenye kipato cha chini.
Amesema NSSF ni chombo cha wananchi kwa vile kinajihusisha moja kwa moja na hatma ya washirika wake ambao wengi wao ni wafanyakazi wenye kipato cha chini.
Balozi Seif aliuahidi Uongozi wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwamba amehamasika ya mfumo wa mfuko huo na kupelekea moja kwa moja kuamua kujiunga ambapo ameahidi kuchangia kila baada ya kipindi cha miezi mitatu.
Mapema Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Dodoma ambao ndio uliopewa jukumu la kuhudumia Viongozi wa ngazi ya Juu Bibi Maryma Ahmed amesema zaidi ya Wabunge 165 wamekubali kujiunga kwa hiari kuwa wanachama wa Mfuko huo.
Bibi Maryam alimueleza Balozi Seif kwamba wabunge hao hupatiwa mafao yao mara wamalizapo utumishi wao wa Bunge sambamba na huduma za matibabu wakati wa kipindi chote cha kazi zao.
Wakati huo huo Balozi Seif akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope amekabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa Tawi la CCM la Mbaleni liliomo ndani ya Jimbo hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni Mchanga, Matofali pamoja na Saruji Balozi Seif amesema wana CCM lazima waendelea kushikamana kwa lengo la kukiwezesha chama hicho kuendelea kushika dola.
Alifahamisha kwamba amani ya Tanzania itaendelea kuwepo na kuleta matumaini iwapo chama cha Mapinduzi kupitia Serikali zake zote mbili kitaendelea kuliongoza Taifa hili.
Vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa Tawi la CCM Mbaleni Jimbo la Kitope sambamba na ahadi ya Seti moja ya Jezi na Mipira iliyotolewa na Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi vimegharimu jumla ya shuilingi Milioni  Moja Nukta Tisa (1,960,000/)

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...