Saturday, February 16, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ASIMAMIA ZOEZI LA UTEKETEZAJI SILAHA HARAMU JIJINI DAR LEO

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akivuta waya kuashiria kufyatua mtego wa kuwasha moto wa kuteketeza Silaha haramu, wakati alipokuwa mgeni rasmi katika zoezi hilo la uteketezaji wa silaha haramu, Lililofanyika katika Kambi ya Magereza jijini Dar es Salaam, leo Feb 16, 2013. Kushoto kwake ni Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Siro na wa pili kulia kwake ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perera Ame Silima na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kmataifa, Benard Membe.
 Sehemu ya Silaha hizo zikianza kuteketea kwa moto baada ya Makamu wa Rais, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, kufyatua waya maalumu wa kuwasha moto huo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi, baada ya kusimamia zaoezi la uteketezaji wa Silaha haramu, lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Simon Siro, wakati wakipita kukagua sihala hizo haramu kabla ya kuanza kwa zoezi la uteketezaji wa silaha hizo haramu lililofanyika Ukonga jijini Dar es Salaam, leo.


 Silaha haramu zilizoteketezwa hii leo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati wa zoezi la uteketezaji wa Silaha Haramu, lililofanyika Ukonga Jijini Dar es Salaam leo.
Wimbo wa Taifa, kabla ya kuanza kwa zoezi hilo. 
*******************************************************

DKT. BILAL AWATAKA WANANCHI KUWAFICHUA WANAOMILIKI SILAHA HARAMU

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameongoza zoezi la uteketezaji silaha haramu na kuwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuwafichua wanaomiliki silaha hizo mapema kabla athari haijawa kubwa zaidi.

Akizungumza katika zoezi hilo la kuteketeza silaha haramu, ambalo limefanyika pamoja kwa  nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye viwanja vya Magereza, Ukonga Jijini Dar es salaam Dkt. Bilal alisema  kila mwananchi ni mlinzi wa kwanza wa amani ya nchi yake  na  wanaomiliki silaha haramu ni wazi kuwa siyo raia wenye malengo mema na amani ya nchi zao.

“Naomba kuchukua nafasi hii kuushukuru uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanikisha zoezi hili ambalo linalenga kutukumbusha kuwa ili tuwe na Jumuiya bora yenye kupiga hatua, hatuna budi kuhakikisha eneo letu linabaki kuwa salama na kwamba wananchi wetu wanapata nafasi ya kufanya kazi zao za kujiongezea kipato bila kuwa na hofu ya usalama wa maisha yao,”

Alisema ndani ya Jumuiya kumekuwa na migogoro mbalimbali sambamba na matukio ya kihalifu ambayo mengi huchangiwa na uwepo wa silaha ndogo na kubwa ambazo hazimilikiwi kihalali.

Alisema takwimu zilizopo zinabainisha kuwepo kwa silaha haramu zipatazo 500,000 (laki tano) katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki hali ambayo inaonesha kuwa kuna kazi kubwa ya kukabiliana na migogoro ya aina mbalimbali ya uhalifu inayojitokeza katika jamii.

Alisema kufuatia raia wasio waaminifu kumiliki silaha haramu kumekuwepo na ongezeko la matukio ya kihalifu yanayotumia silaha na matukio mengi katika ukanda wa Afrika Mashariki yanatokea katika maeno ya mipakani na yale yanayohusisha muingiliano wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine, matukio ya ujambazi,  uvamizi na mengine ya aina hiyo.

Alisema ongezeko la silaha haramu lina athari nyingi katika maisha na maendeleo kwa ujumla na kutaja athari ya wazi kabisa inayotokana na ongezeko la silaha hizo kuwa ni ile inayojitokeza katika sekta ya Utalii ambako watu wameshuhudia kuongezeka kwa matukio ya ujangili unaofanywa katika mbuga za wanyama ambao unahatarisha kwa kiasi kikubwa mafanikio katika sekta ya Utalii.

“Tusipowadhibiti majangili mapema, siku wanyama wakipungua watahamia katika sekta nyingine. Kazi hii itakuwa rahisi kama tukiifanya kama Jumuiya na sio nchi moja moja,” alibainisha Makamu wa Rais.

Dkt. Bilal alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia Jumuiya ya Afrika Mashariki kukabiliana na tatizo la silaha haramu na hasa Shirika la Maendeleo la Ujerumani GTZ ambalo limesaidia katika kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Ujerumani nchini Klaus Brandes alisema  Serikali ya Ujerumani itaendelea kuisaidia Jumuiya katika kukabiliana na tatizo la silaha haramu ili kuhakikisha eneo la ukanda wa Afrika Mashariki linabaki kuwa na amani na salama.   

Alielezea kufurahishwa kwake na juhudi za Rais Jakaya Kikwete katika kutatua migogoro kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwenye Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
Februari 16, 2013

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...