Kaimu
Mkurugenzi wa SUMATRA Athman Kilima akizungumza na waandishi wa habari
leo katika makao makuu ya taasisi hiyo wakati akitangaza kupanda kwa
viwango vya nauli ya mabasi ya mikoani na Daladala.
………………………………………………………………..
Mamlaka
ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekamilisha
mchakato na kuridhia viwango vipya vya nauli kwa ajili ya usafiri wa
mijini na usafiri wa kwenda mikoani. Viwango hivi vipya vimefikiwa baada
ya kufuata taratibu za kisheria na za kiutendaji ambazo SUMATRA kama
msimamizi na mdhibiti wa sekta ya usafiri wa barabara inapaswa kuzifuata
kabla ya kuridhia viwango hivyo. Viwango vipya vya nauli vitaanza
kutumika kuanzia tarehe 12 Aprili, 2013.
SUMATRA
ina wajibu kisheria kuhakikisha pamoja na mambo mengine kuwa maslahi ya
watumiaji na watoa huduma za usafiri yanalindwa ili kuwepo na huduma
endelevu ya usafiri ulio bora, salama na wenye kukidhi mahitaji. Aidha
SUMATRA ina jukumu la kujenga na kulinda mazingira mazuri na ya kuvutia
kwa watoa huduma ili huduma ya usafiri inayotolewa inakuwa katika
kiwango na gharama zinazoendana na huduma zenyewe.
Katika
kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012, SUMATRA ilipokea maombi rasmi
kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa barabara yakiwemo makampuni
ya usafirishaji abiria ya Cordial Transport Services P.L.C, Happy
Nation Co. Ltd, ABC Trans na Mwesigwa Mtazaha Kazaula yakipendekeza
mapitio ya viwango vya nauli za mabasi yanayotoa huduma za usafiri
mijini (Daladala) na mabasi yanayotoa huduma katika Mikoa kufuatia
ongezeko la gharama za uendeshaji kwa mujibu wa mawasilisho yao.
Wakati
maombi ya wamiliki wa Daladala yalilenga katika kuongeza viwango vya
nauli kwa 149% ya viwango vya sasa, wamiliki wa mabasi ya masafa marefu
waliomba nyongeza kati ya 35% na 48.5%.
Kwa
mujibu wa Kifungu Na 18 cha Sheria ya SUMATRA, 2001, SUMATRA
iliwashirikisha wadau mbalimbali katika kujadili na kupata maoni yao
kuhusu maombi ya wamiliki ya kuongeza viwango vya nauli kabla ya kufanya
maamuzi ya mwisho.
Aidha
Mamlaka iliridhia viwango vipya kwa mujibu wa kifungu cha 16 Cha
Sheria ya SUMATRA ambacho kinaipa Mamlaka kufanya mapitio ya nauli mara
kwa mara kwa kuzingatia gharama za kutoa huduma, maslahi ya watoa
huduma, faida, maslahi ya watumia huduma ya kulipa nauli yenye uwiano na
gharama za huduma inayotolewa.
Kwa
kuzingatia hoja za waombaji, maoni ya wadau, uchambuzi wa menejimenti,
haja ya kupunguza gharama zisizo za lazima za uendeshaji na udhibiti wa
vitendo vya uvunjaji wa Sheria na taratibu za uendeshaji shughuli za
usafirishaji, Mamlaka ya SUMATRA iliamua kuongeza viwango vya juu vya
nauli za Daladala kwa wastani wa 24.46%.
Aidha
kwa mabasi ya masafa marefu, viwango vimeongezwa kwa 20.3% kwa mabasi
ya kawaida, 16.9% kwa mabasi ya daraja la kati na 13.2% kwa mabasi ya
daraja la juu.
Mchanganuo wa viwango vipya vya nauli ni kama ifuatavyo:
- Nauli za Daladala – Jiji la Dar es Salaam
Umbali wa Njia | Kiwango Kipya cha Nauli | Mfano wa Njia |
Kilomita kati ya 0 – 10 (Na mipaka ya Jiji Kati) | Sh 400/= | Ubungo – Kivukoni |
Kilomita kati ya 11 – 15 | Sh 450/= | Mwenge – Temeke |
Kilomita kati ya 16 – 20 | Sh 500/= | Tabata Chang’ombe – Kivukoni |
Kilomita kati ya 21 – 25 | Sh 600/= | Pugu Kajiungeni – Kariakoo |
Kilomita kati ya 26 – 30 | Sh 750/= | Kibamba – Kariakoo |
Mamlaka imeandaa majedwali kwa njia zote za Dar es Salaam. Majedwali hayo yanaweza kupatika katika tovuti yetu www.sumatra.or.tz.
Nauli
ya Mwanafunzi itakuwa Sh 200/= ambayo ni nusu ya nauli ya mtu mzima ya
kiwango cha chini cha nauli ya Sh 400/=. Nauli hii itatumika kwa njia
zote za Jiji la Dar es Salaam.
- Nauli za Mabasi ya Masafa Marefu
Daraja la Basi | Nauli ya zamani kwa km-abiria | Nauli mpya kwa km-abiria | Mfano wa kiwango kipya cha nauli kwa baadhi ya njia | |
Basi la Kawaida kwa njia ya lami | Sh 30.67 | Sh 36.89 | DSM–Mbeya Km 833 | Sh 30,700 |
Basi la Kawaida kwa njia ya vumbi | Sh 37.72 | Sh 46.11 | S/wanga-KigomaKm 551 | Sh 25,400 |
Basi la hadhi ya kati (Semi Luxury | Sh 45.53 | Sh 53.22 | DSM–Mwanza Km 1,154 | Sh 61,400 |
Basi la hadhi ya juu (Luxury) | Sh 51.64 | Sh 58.47 | DSM–Arusha Km 616 | Sh 36,000 |
Ili
kuhakikisha kuwa kuna uwiano kati ya viwango vipya vya nauli na ubora
wa huduma ya usafiri, Mamlaka imetoa maagizo kwa wamiliki wa mabasi ya
masafa marefu kuboresha maeneo yanayohusiana na huduma ya usafiri kama
ifuatavyo:
- Wamiliki wa mabasi kutokutumia wapiga debe katika kuuza tiketi za safari
- Wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanafuata Kanuni za SUMATRA za Udhibiti wa Tozo na Nauli (SUMATRA Tarrif Regulations) ambazo zinahimiiza kuwepo kwa kumbukumbu sahihi za mahesabu ili kurahisisha mapitio ya viwango vya nauli
- Kufuata Sheria, Kanuni na Masharti ya Leseni ya usafirishaji abiria
- Kutoza nauli kwa mujibu wa daraja la basi lenye sifa kamili la daraja husika kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Usalama na Ubora
Aidha kwa mabasi ya mjini, Mamlaka imetoa maelekezo yafuatayo:
- Kuhakiksha kuwa abiria wote wanapatiwa tiketi
- Kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa Sheria ikiwemo kutokamilisha safari maarufa kama kukata ruti, kubadili njia na unyanyasaji wa aina yoteyote kwa abiria
- Kutokutumia wapiga debe
- Wafanyakazi wa mabasi kuvaa sare nadhifu wakati wote.
Mamlaka
ya SUMATRA inaendelea kuimarisha ushirikiano kwa kufanya kazi kwa
karibu na Mamlaka zingine kama Wakuu wa Mikoa, Serikali za Mitaa,
Mamlaka za Miji, Polisi, TBS, TANROADS, Kamisheni ya Bima na wananchi
kwa ujumla, katika kuleta mageuzi kamili ya utoaji wa huduma za usafiri
wa barabara kwa kiwango cha juu.
A.S.K. Kilima
KAIMU MKURUGENZI MKUU
2 Aprili, 2013
No comments:
Post a Comment