Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jana walishambuliana huku waliokuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali katika vikao vya bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma wakituhumiwa kukiua chama na kukipa nguvu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kilifanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa mjini Dodoma.
Pinda alianza kwa kuweka hoja mezani akitaka wabunge wa CCM kuchangia Sh.100,000 kila mmoja kwa ajili ya kuwezesha ushindi katika uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika katika kata 26 nchini.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge hao, lakini alisimama Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Khangi Lugola, akihoji kulikoni wanaosaidiwa na chama wakawa madiwani ili hali wabunge walio na kesi mahakamani wakiachwa kugharamia kila kitu wenyewe.
“Si unajua nyoka wa shaba (Lugola), ana kesi mahakamani, sasa ndiyo maana akaamua kuhoji, iweje yeye hasaidiwi na chama wakati huo huo anaambiwa akisaidie chama,” alisema mmoja wa wabunge aliyekuwa ndani ya kikao hicho.