Sunday, April 28, 2013

Mawaziri, wabunge CCM warushiana 'makombora'



Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), jana walishambuliana huku waliokuwa mstari wa mbele kuikosoa serikali katika vikao vya bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma wakituhumiwa kukiua chama na kukipa nguvu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mwenyekiti wake, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kilifanyika katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa mjini Dodoma.

Pinda alianza kwa kuweka hoja mezani akitaka wabunge wa CCM kuchangia Sh.100,000 kila mmoja kwa ajili ya kuwezesha ushindi katika uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika katika kata 26 nchini.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge hao, lakini alisimama Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Khangi Lugola, akihoji kulikoni wanaosaidiwa na chama wakawa madiwani ili hali wabunge walio na kesi mahakamani wakiachwa kugharamia kila kitu wenyewe.
“Si unajua nyoka wa shaba (Lugola), ana kesi mahakamani, sasa ndiyo maana akaamua kuhoji, iweje yeye hasaidiwi na chama wakati huo huo anaambiwa akisaidie chama,” alisema mmoja wa wabunge aliyekuwa ndani ya kikao hicho.

Alipomaliza alinyanyuka Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba, akiwashtumu Lugola na Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe kuwa badala ya kuisaidia serikali wao wamekuwa wakiishambulia jambo ambalo limekuwa halileti picha nzuri kwa wananchi wanaowaangalia na kuwasikiliza.

“Kitendo cha huyu Filikunjombe kusema serikali imevaa miwani ya mbao kinaonyesha kuwa hatuko pamoja, kama wana kesi mahakamani waacheni waendelee nazo maana hatuko pamoja nao,” chanzo kilimkariri Nkumba akiwashambulia.
Chanzo hicho kilisema Nkumba alisema mwezi ujao wana kikao na mwenyekiti wao (Rais Jakaya Kikwete) na kwamba angetumia nafasi hiyo kusema mengi aliyonayo.
“Alipomaliza kuzungumza alisimama Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kibajaji), akamuunga mkono Nkumba, kuwa Lugola anatakiwa kushughulikia kesi yake mwenyewe kwa kuwa hakisaidii chama,” chanzo kilimkariri Lusinde.

Chanzo hicho kilisema kuwa Lusinde, alimtaka Waziri Mkuu kuwaachia kazi ya kupambana na vyama vya upinzani kwa kuwa wanaimudu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alimshtumu Lugola kwa kauli yake ya kwamba, kuna mawaziri wanajishughulisha na dawa za kulevya bila kuwataja jambo ambalo linawaacha wananchi njia panda.

Alisema wananchi wanadhani kuwa na wabunge wao wamo katika biashara hiyo. “Pia alihoji kama wabunge wana kero zao ni kwanini wasiwafuate mawaziri na kuwaeleza badala ya kuzungumza ndani ya Bunge ambapo wananchi wanaona,”chanzo kilimkariri Malima akimpasha Lugola.
Alipomaliza kuzungumza alisimama Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu, na kusema kuwa kesi nyingi CCM inashindwa kwa sababu majaji wengi wanakipenda Chadema na kuichukia CCM.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema Mangungu aliungwa mkono na Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk. Cyril Chami, ambaye alidiriki kumtaja kwa jina mmoja wa majaji nchini, ambaye alidai amekuwa na upendeleo wa wazi wazi anapofanya maamuzi kwa kesi zinazoihusu Chadema.

“Baada ya hapo alisimama Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, na akatoa ushauri kuwa kuna haja ya chama kusaidia majimbo ya uchaguzi kwa viongozi wa juu wa chama kwenda katika majimbo kama kinavyofanya chama cha Chadema.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia naye alitumia kikao hicho kumshambulia Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuwa hakuwa msaada wowote wakati wa vurugu zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara.
Ghasia alilalamika kuwa wakati wa vurugu zilizosababishwa na wananchi kutaka gesi isitoke mkoani humo, alimpigia simu Dk. Nchimbi lakini hakupokea na hata pale alipotuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi hakujibu.
“Waziri alilalamikia kuwa chama hakimsaidii katika jimbo lake wakati Lipumba (Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba) amekuwa akienda kila mara jimboni kwake,” kilisema chanzo hicho.
Ghasia alihoji iweje wakati wa vurugu nyumba zote za wabunge wa CCM wanawake zichomwe moto na za wabunge wanaume wa CCM zisiguswe.
Hata hivyo, Filikunjombe, alipopata nafasi ya kujibu aliwashambulia mawaziri kwamba wao sio wafanyaji wa kazi na kumtolea mfano Waziri wa Maji, Profesa Jummane Maghembe , kwamba katika wizara zote hakuwahi kufanikiwa japokuwa amekuwa akihamishwa kila mara.
Filikunjombe alikaririwa akisema kuwa chama kinatakiwa kiwe na miradi kama chama cha ANC cha nchini Afrika Kusini ambacho kina miradi ya uhakika ambayo inawafanya watu wavutike na kufanya kazi ndani ya chama hicho cha siasa.
Kisha Filikunjombe akamgeukia Nkumba akimshangaa kwa kumshambulia yeye badala ya mashambulizi hayo kupeleka kwa kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana anayetoa maelekezo yasiyo sahihi.

Bila kufafanua maelezo hayo, Filikunjombe alisema yuko sahihi kuikosoa serikali kwa kuwa hafurahishwi na utendaji wa baadhi watendaji wa serikali.
“Baadhi ya wabunge ni wanafiki kwa sababu wanajifanya kukipenda chama wakati hawakipendi…..kama serikali haifanyi kazi kwanini nisiikosoe,” chanzo kilimkariri Lugola na kuongeza kuwa wakati akiyasema hayo alimtaka Nkumba kuacha unafiki.
Lugola alihoji mbona Rais Kikwete alipotaja kuwa kuna viongozi wa dini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya Malima hakumtaka awataje majina.

‘Lugola aling’aka akitaka kuyataja majina ya mawaziri wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini wabunge wengine walimsihi asiwataje,” kilisema chanzo hicho.
Aidha, Lugola aliwashambulia mawaziri kwa kuwaeleza kuwa wanapochaguliwa kushika nafasi hizo wanapandisha mabega juu, jambo ambalo linawafanya kushindwa kuwaona. “Ni rahisi kumuona George Bush kuliko kuwaona ninyi,”alisikika Lugola akiwapasha mawaziri.
Naye Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, alikaririwa akisema kuwa wanavyofanya Filikunjombe na Lugola ni sahihi kabisa na kwamba yeye ameshakuwa mzee anawachia vijana wafanye kazi zao.
Katika hatua nyingine Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, alimpasha Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, kuwa wakati akijibu swali lake la nyongeza bungeni kuhusiana na deni la taifa, alimdhalilisha mbele ya Watanzania.
“Ulitakiwa kabla ya kujibu swali langu uangalie kwanza wasifu wangu,”alikaririwa akisema Mpina ambaye kitaaluma ni mchumi.

SOURCE::: NIPASHE

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...