Msaidizi
wa zamani wa Padri (Katekisita) katika Kigango cha Kanisa Katoliki
Kijiji cha Mkwajuni, Florian Mwamosi (70) amekufa baada ya kuzikwa akiwa
hai katika kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kwa njia ya
kishirikina.
Tukio hilo limetokea katika Kitongoji
cha Maweni kijijini hapo wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani alikiri kutokea kwa tukio hilo
akieleza kuwa lilitokea saa 9:00 mchana katika kijiji hicho cha Maweni
Mkwajuni wilayani Chunya.
"Marehemu
aliuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kupigwa na mawe kwa tuhuma za
kuhusika na uchawi na kusababisha kifo cha Peter Robert," alisema.
Mashuhuda wa
tukio hilo walisema kuwa marehemu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kwa
ushirikina aliwahi kuwa Katekista wa kigango hicho hadi mwaka 2007.
Wameeleza kuwa Mwamosi alikwenda
kuhudhuria mazishi ya Peter Robert (28) katika kitongoji hicho cha
Maweni, baada ya kufuatwa nyumbani kwake na watu wakitaka aende kwa
sababu yeye ni mmoja wa wazee wa mila katika kitongoji hicho.
"Bwana Mwamosi alikuwa akituhumiwa
kwa uchawi kwa muda mrefu na wenzie wawili, hivyo alipofika makaburini
ilianza minong'ono ya watu na huku wengine wakiguna na ndipo alipoombwa
aingie kaburini kwa ajili ya kupokea jeneza lililobeba mwili wa marehemu
Peter Robert," alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho aliyejitambulisha
kwa jina moja la Joseph.
Alisema
kuwa baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake
walitoka kwa haraka na kumwacha Mwamosi peke yake ndipo kundi la watu
waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe
huku wakimwamuru akae chini.
Shuhuda
huyo alisema kuwa baada ya kukubali kukaa chini akiwa ndani ya kaburi
hilo, walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya mwili wake waliingiza
jeneza la marehemu Peter na kuliweka juu yake na kuanza kulifukia kaburi
hilo.
"Baada ya kukaa
chini ndani ya kaburi hilo ndipo walianza kumfukia kwa udongo na baadaye
wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu yake, kisha kumfukia na
udongo na taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili ya marehemu
Peter,"alisema.
Alidokeza
kuwa chanzo cha tukio hilo ni marehemu Robert kuugua ghafla tumbo,
ndipo ndugu zake walipoamua kumpeleka kwa mganga wa jadi kwa ajili ya
kupata matibabu na baada ya siku tatu alifariki dunia.
:CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment