Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema
vurugu zinazoendelea bungeni zinasababishwa na Kambi Rasmi ya Upinzani
inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe, kushindwa kujenga hoja na mbinu za kuwabana
wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema wabunge wa Chadema wana tabia ya kufuata mfumo wa kwenda bungeni
na hoja zinazobeba chama chao na si za Watanzania wote kama jinsi CCM
wanavyofanya.
Alisema kambi rasmi ya upinzani pia
imeshindwa kulinda utaratibu mzuri wa kutetea masilahi ya umma bila
jazba na hoja zenye mashiko kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ilipokuwa
ikiongozwa na CUF, Kiongozi huyo alisema kambi ya upinzani inapaswa
ijipange upya kwa utaratibu na mikakati mizuri ya kuteta hoja za
wananchi bila kuyumbishwa na wabunge wa CCM.
“Bunge usiwe uwanja wa kuonyesha
mbwembwe za chama bali uwe uwanja wa kutetea haki za wananchi, wabunge
wanapaswa wabadilishe mitazamo ya kuona bungeni ni sehemu ya kujionyesha
kisiasa na chama chako kinafanya nini nje ya Bunge,” alisema Lipumba.
Alisema viongozi wa Serikali wanapaswa
kubadilika kuhusu namna ya kutoa majibu bungeni.
Profesa Lipumba alisema mawaziri wengi
wanakuwa wakitoa majibu mepesi katika maswali ya msingi yanayoulizwa na
wabunge wa upinzani.
Alisema Bunge linatumia muda na pesa za
walipakodi vibaya kwa baadhi ya wabunge kuwa na ubishi usiokuwa na tija,
kutoleana matusi na wengine kuingilia hoja za wenzao bila sababu za
msingi.
Profesa Lipumba pia alisema Spika wa
Bunge, Anne Makinda amepoteza uwezo wa kuliongoza Bunge.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment