Saturday, April 27, 2013

ISHA MASHAUZI ATIWA MBARONI KWA WIZI WA SH. 700, 000...!!

MWIMBAJI ambaye pia ni bosi wa Kundi la Mashauzi Classic, Aisha Ramadhan Makongo ‘Mashauzi’, Jumatano iliyopita alikumbwa na masaibu mazito kufuatia kudakwa na polisi wa Kituo cha Msimbazi, Dar akituhumiwa kukwapua mkoba wenye kitita cha shilingi laki saba, elfu hamsini na nane na mia mbili (758,200) mali ya Veronica Tarik.
Chanzo cha habari kituoni hapo kilidai kuwa Jumanne iliyopita, Isha Mashauzi na shosti wake aliyejulikana kwa jina la Halima Shaban waliingia duka moja Mtaa wa Mafia na Jangwani, Kariakoo, Dar kwa lengo la kufanya ‘shopping’ lakini walipochomoka, Veronica alishangaa kutouona mkoba wake.

Veronica aliwakimbiza wawili hao na kuwadaka mtaa wa pili na kuwasomea tuhuma zao kisha akawaomba awasachi kwenye mafurushi waliyobeba lakini Isha na mshirika wake waligoma, hali iliyosababisha kuzuka kwa timbwili wakidai mwanamke huyo alitaka kuwadhalilisha.

Baada ya Veronica aliyekuwa na wapambe ‘legelege’ kuzidiwa nguvu, waligeuka na kukimbilia Kituo cha Polisi Msimbazi ambako alifungua kesi ya wizi kwa Isha na shosti wake kwa jalada namba MS/RB/4023/2013.


Maafande wenye difenda waliingia mitaani kuwasaka watuhumiwa hao mtaa hadi mtaa wakitumia mbinu mpya za kikachero na kufanikiwa kuwatia mbaroni Jumatano iliyopita.
Isha akiwa selo, wapambe wake walimiminika kituoni hapo akiwemo Mtangazaji wa Kituo cha Redio Times FM cha jijini Dar, Hadija Shaibu ‘Dida’ kwa ajili ya kuhangaikia kuwachomoa wawili hao.

Saa 5:14 usiku, wapambe hao walifanikiwa kuwawekea dhamana lakini kasheshe nzito ilikuwa wakati wa kutoka rumande kwani wapambe wa Isha waligundua kuwa waandishi walikuwa wamekizingira kituo hicho na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kunasa picha zao.
 Isha alijaribu kujibanza ndani ya selo lakini wapambe walimpelekea taarifa kuwa waandishi nje walikuwa wakijipanga kukesha kituoni hapo mpaka siku itakayofuata.

Baada ya kupata ujumbe huo, Isha alichomoka mahabusu kwa kasi ya mnyama swala na kukimbilia kwenye gari aliloandaliwa kumchukua huku wapambe wake wakiwa wamezikamata kamera za waandishi eti ili wasimpige picha.


Kesho yake Alhamisi, mwandishi wetu alizungumza na Isha kwa njia ya simu ili aweze kuweka bayana juu ya sakata hilo lakini mwimbaji huyo alimjibu mbofumbofu.
“Wewe andika unachotaka si ulikuwepo kituoni na umenipiga picha, sasa unataka nini? Yaani hata wewe unanifanyia hivyo duh! Leo nimeamini waandishi hawana undugu,” alisema Isha na kukata simu.
GPL

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...