JOTO la Uchaguzi wa Rais ndani ya CCM linazidi kupanda huku makada na viongozi wa chama hicho wakipigana vijembe hadharani.
Hali hiyo inatokana na kile kinachojitokeza sasa, kuibuka kwa makundi ya
jamii, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kuwashawishi makada
kadhaa wa CCM wawanie nafasi hiyo ya uongozi wa nchi katika Uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Makada ambao wamekuwa wakishawishiwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Wakati baadhi ya makada wengine wanaotajwa kutaka kuwania urais ndani ya
CCM wakimlalamikia Lowassa, wachambuzi wa siasa wamekuwa wakihoji
mpango wa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, alipochapisha vitabu na kugawa kwa wajumbe wote wa mkutano
mkuu, lakini makada wenzake wamekuwa kimya, hawajalalamikia kitendo
chake hicho.