JOTO la Uchaguzi wa Rais ndani ya CCM linazidi kupanda huku makada na viongozi wa chama hicho wakipigana vijembe hadharani.
Hali hiyo inatokana na kile kinachojitokeza sasa, kuibuka kwa makundi ya
jamii, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu, kuwashawishi makada
kadhaa wa CCM wawanie nafasi hiyo ya uongozi wa nchi katika Uchaguzi
Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Makada ambao wamekuwa wakishawishiwa kuwania nafasi hiyo ni Mbunge wa
Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Profesa Mark Mwandosya na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Wakati baadhi ya makada wengine wanaotajwa kutaka kuwania urais ndani ya
CCM wakimlalamikia Lowassa, wachambuzi wa siasa wamekuwa wakihoji
mpango wa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, alipochapisha vitabu na kugawa kwa wajumbe wote wa mkutano
mkuu, lakini makada wenzake wamekuwa kimya, hawajalalamikia kitendo
chake hicho.
Mbali na hilo, pia anadaiwa kuwa alinunua simu za Gallaxy Sumsang zaidi
ya 140, akazigawa kwa wajumbe wa Baraza la Vijana la CCM (UVCCM)
Zanzibar suala ambalo bado hadi sasa hajalitolea ufafanuzi.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ambaye anatajwa kuwapo
katika mbio za urais, alikuwa akitembea na mabango ya kuonyesha watu
wakimwomba agombee jambo ambalo lilimfanya aandikiwe barua na Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kusitisha ziara zake ambazo zilitajwa
kuwa za kampeni za kuwania urais. Wafuasi wa Mwigulu pia wanadaiwa
kuandika katika mawe makubwa katika barabara nchi nzima kwamba yeye
ndiye Rais 2015.
Lowassa
Jana, Lowassa amejibu mapigo na kusema hawezi kuwajibu wanaosema
anawalipa wanaomshawishi kuwania nafasi hiyo, kwani kufanya hivyo ni
kuwapa sifa wasizostahili na wanachofanya ni upuuzi na uongo.
Kauli hiyo imekuja baada ya jana baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu
Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais akisema kuna watu
wanatumia vibaya umasikini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha
ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupokea ujumbe wa wachungaji
110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini jana,
Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya kuwagharamia watu wanaofika
nyumbani kwake kumshawishi, na kwamba wengi wanafanya hivyo kwa mapenzi
yao na Mungu wao.
“Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja)
kusema leo kuna mtu (Makamba) kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo
hovyo kidogo, nikimjibu nitakuwa nampa heshima, kwahiyo nampuuza, sina
uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina
sababu.
“Ni mapenzi yao kwa taifa lao na Mungu wao, lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo,” alisema Lowassa.
Akizungumza juu ya ujio wa wachungaji hao, Lowassa alisema umeandika
historia katika maisha yake kwani hakutegemea kupokea kundi kubwa kama
hilo la watumishi wa Mungu.
“Wote waliokuja nimewaeleza kuwa hili ni suala kubwa linalohitaji sala
na mimi ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige
magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye
anitiaye nguvu,” alisema.
Mapema, mratibu wa wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka
Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila
kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.
“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.
Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.
Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi,
Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke,
Kinondoni, Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.
Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe na Kilolo.
Awali Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa wanalipwa, wameishiwa, wamefilisika na sasa wanatapatapa.
Alisema kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.
Mgeja alisema wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma,
Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, alitoa rai kuomba
wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi,
hivyo wanachokifanya si makosa.
“Nitaadharishe tu, tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika
nyumbani kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo
tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni, suala hili ni kubwa linahitaji dua
na maombi.
“Kama viongozi tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea
kijiti na kutupeleka mbele, niungane na Watanzania wenzangu na mimi
kusema tunaona kwamba hakuna mwingine zaidi ila mheshimiwa Lowassa,”
alisema Mgeja.
BULEMBO AIBUKA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah
Bulembo, amewataka wajumbe 20 wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo waliokwenda
kwa Lowassa kumwomba agombee urais, wajitokeze na kukanusha kauli hiyo.
Juzi wajumbe hao walikwenda kwa Lowassa eneo la Area C, Manispaa ya
Dodoma na kumwambia jumuiya hiyo inamtaka agombee urais na kumchangia Sh
600,000 kwa ajili ya kuchukulia fomu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Bulembo, alisema wajumbe hao wa
Baraza waliokwenda sio wasemaji wa chama na wala hawakutumwa na
jumuiya.
“Tunawataka wajumbe wote 20 waliokwenda wakanushe kwenye vyombo vya
habari ndani ya mwezi huu, mbali na kukanusha, Kamati ya Maadili ya
Jumuiya itawajadili na kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa
kanuni na miiko ya uongozi,” alisema.
Pamoja na kutoa tamko hilo, Bulembo yeye binafsi amekuwa mstari wa mbele
kumuunga mkono na kumfanyia kampeni Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika
harakati za kuomba kuteuliwa na chama hicho.
Wanafunzi wamvaa January
Siku moja baada ya Nabu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
January Makamba, kusema watu wanaoenda kwa Lowassa wanahongwa, viongozi
wa wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara waliofika kwa waziri huyo
juzi, wamesema wamedhalilishwa kwa kauli hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, viongozi hao
walisema kauli hiyo inaashiria kuwadharau na kutaka watu wanaotoa
matamko kama hayo wawaombe radhi.
Rais wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii, Angelo Madunda, alisema walifikia
uamuzi wao baada ya kukaa chini kama wasomi na kukubaliana kwa mtazamo
chanya kwamba Lowassa anawafaa.
“Watanzania wenyewe watafakari na kuangalia hili suala kwa ukubwa wake,
pale kwa Lowassa hakukuwa na masufuria ya ubwabwa wala nini, Lowassa ni
kama klabu ya mpira ana mashabiki wake, sisi ni sehemu ya hao mashabiki
wake, wengine nao watafute mashabiki wao wawafuate,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga), Nobati
Pangaselo, alisema kutokana na kauli zilizotolewa juu ya safari yao ya
kwenda kwa Lowassa, ameamini kuwa hata kauli nyingine zinazosemwa juu ya
waziri mkuu huyo wa zamani ni za uongo.
NYALANDU NA KINANA
Machi 20, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Madhehebu ya Dini
Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa, alimjia juu Katibu Mkuu wa
CCM, Kinana, kutokana na kauli anazozitoa kwa watendaji wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sheikh Alhad alisema baadhi ya kauli
za Kinana anazozitoa kwenye mikutano ya hadhara zinawavunja moyo
watendaji wa Serikali katika kutimiza wajibu wao.
Wiki iliyopita, Kinana alikaririwa akiwa mkoani Singida akisema Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, hana anachokifanya, badala yake
anazurura tu na kwamba anathamini wanyama kuliko binadamu.
“Kamati imesikitishwa na kauli hii iliyolenga kumbeza au kubeza jitihada
za Nyalandu. Tunaona kama inalenga kumvunja moyo. Ni vizuri mtu
anapojituma apongezwe na huo ndio uadilifu.
“Mafaniko yamepatikana mengi chini ya uongozi wake (Nyalandu), iweje leo
mtu hodari na mchapakazi kama huyu avunjwe moyo kwa kuambiwa eti
anazurura tu badala ya kupongezwa?” alihoji Sheikh Alhad.
Alimtaka Kinana kuwa makini na kauli zake anapopokea malalamiko kutoka
kwa wananchi na kumtaka atumie busara anapotoa maelekezo kwa viongozi.
NAPE NA MIPANGO
Kutokana na mvutano ulioibuka ndani ya CCM, Katibu wa NEC, Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye, alisema makada wa chama hicho wenye kupanga mipango
ya kuiangusha CCM iwapo hawatateuliwa kugombea urais, wanajisumbua
kwani wataanguka wao na kukiacha chama hicho kikiwa imara.
Kauli hiyo aliitoa juzi Arusha Mjini wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara ya Kinana mkoani Arusha.
“Wapo wanachama wanaopanga mipango haramu ya kukiangusha chama endapo
hawatateuliwa kugombea urais. Wenye mipango hiyo wanajidanganya kwani
hawatafanikiwa na wajue wazi kabla ya kuiangusha CCM wataanguka wao,”
alisema Nape.
KINANA NA CHAMA
Kwa upande wake, Kinana alisema moja ya kazi anayofanya ni kujenga heshima ya CCM na kubwa zaidi kuwa msemaji wa wananchi.
“Zipo changamoto kutoka kwa wana CCM wasiopendezewa na hatua yangu hii.
Hata hivyo sitarudi nyuma pamoja na baadhi ya watu kutaka kunikatisha
tamaa,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vigumu kwa watu hao kumwondoa katika nafasi yake hiyo
kwa vile anazo baraka za Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete
No comments:
Post a Comment