WAKATI
wadau wa usafiri nchini wakipendekeza kushuka kwa nauli za daladala na
mabasi yaendayo mikoani, wamiliki wa mabasi wametishia kufuta utaratibu
wa kutowatoza nauli askari na kuongeza kuwa, hata nauli pungufu za
wanafunzi sasa zitakuwa historia.
Wadau wamependekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani
kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za
daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa
kilometa 10.
Hayo yaliibuka jana wakati wa mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu
mapitio ya viwango vya nauli za mabasi ya mikoani na daladala kupungua
kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta ulioandaliwa na Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra). Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Katibu Mkuu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu
na Majini (Sumatra- CCC), Oscar Kikoyo alisema sababu ya kutaka nauli
kupungua licha ya kushuka kwa bei ya mafuta, pia wamiliki wa mabasi
Julai mwaka 2014 walisamehewa ushuru wa forodha kwa asilimia 10 hadi 25
ya mabasi mapya yanayoingizwa nchini.
Alisema mafuta yanachangia katika uzalishaji wa huduma kwa asilimia
20 hadi 30 na si jambo jipya katika kuomba kushusha nauli, kwani mwaka
2009 nauli ilishuka ambapo kwa nauli za kwenda mikoani wanataka ipungue
kwa km moja kuwa Sh 28.05 badala ya sh 36.89.
Alitoa mfano wa nauli wanazotaka kwa mabasi ya kawaida kuwa Moshi na
Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh
42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756
badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh 16,700).
Katika usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa
kuwa Sh 31.39 kwa usafiri wa kilometa 10 badala ya Sh 400 na kilometa 15
iwe Sh 450 na maeneo mengine kupungua kwa Sh 100.
Kikoyo alisema pia wanaandaa ombi kupitia kanuni na sheria kwa
wamiliki wanaotoza nauli kinyume inavyotakiwa walipishwe faini ya Sh
milioni moja badala ya Sh 200,000 za sasa ili wayaone maumivu ya adhabu
hiyo kubwa.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Daladala
(Darcoboa), Sabri Mabruk alisema wao wako tayari kupunguza nauli kwa
asilimia mbili hata kesho kama walivyofanya Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) na siyo asilimia 25 wanayotaka.
Alisema tatizo kubwa katika ukokotoaji wa hesabu ni suala la ujazo wa
abiria ambapo mwaka 2012 walipotakiwa kuunda kikosi kazi kwa ajili ya
kushughulikia suala hilo ambapo Sumatra wanadai ni asilimia 100, lakini
ukweli ni asilimia 80.
“Ni kweli unaweza kuona mabasi yamejaa, lakini wapo wanafunzi
wanaolipa nusu nauli (Sh 200) na askari ambao hawalipi kabisa sasa ni
vema kuangalia suala hilo, kwani hata nyakati za mchana mabasi huwa
yanaota jua tu, hakuna abiria,” alisema Mabruk alisema ni vema kabla ya
nauli mpya kutangazwa kuangalia upya, kwani nafuu ya kupungua bei ya
mafuta ni Sh 12,000 ambayo inaishia kwa wafanyakazi hata wamiliki
hawaipati.
“Iwapo mtaamua kushusha nauli tutafuta `ofa’ ya serikali ya
kubeba askari bure pamoja na kubeba abiria kwa nusu ya nauli inayotakiwa
kisheria na hatutaenda kwenye baraza au mahakamani,“ alisema.
Alisisitiza kuwa ikiwa watatakiwa kwenda mahakamani au kwenye baraza
watasimamisha magari yao kufanya kazi, kwani hatua hizo zitakuwa kufidia
nauli itakayoshushwa.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi ya Nchini (Taboa),
Enea Mrutu alisema hawaoni sababu ya msingi kushusha nauli kulingana na
mahesabu na mafuta pekee si kigezo cha kushusha au kupanda nauli na
kulalamikia masuala hayo kuingiliwa na siasa.
Alishangaa kwa nini suala la kushuka mafuta liwe kwa daladala pekee
na siyo vyakula, magazeti na mengineyo kushuka bei huku akisisitiza kuwa
changamoto kubwa ni suala la ujazo wa abiria linaloleta utata.
Huku Katibu wa Chama cha Kutetea Abiria, Thomas Haule alisema
wanaunga mkono maombi ya Sumatra CCC katika kupunguza nauli, kwani
katika punguzo wamiliki hao wanapata faida kubwa huku akiitaka Sumatra
pia kuangalia nauli za abiria wanaoshuka katikati ya safari, kwani
hazizingatiwi.
Pia alitaka kuwe na mfumo maalumu katika kuongeza na kupunguza nauli
pindi ikitokea suala kama la kushuka au kupanda bei ya mafuta kuliko
kupoteza rasilimali kukaa na kujadili kila wakati. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment