Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameagiza wafanyakazi sita
wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), wafukuzwe kazi na polisi wawakamate
na kuwalaza rumande kuanzia jana kutokana na tuhuma za wizi.
Pia, ameagiza mali za watuhumiwa hao, zichunguzwe na ikibainika ni
zaidi ya kipato chao cha kawaida, zipigwe mnada na Bodi ya Wakurugenzi
ikae na kuangalia hatua zaidi za kuchukua.
Dk Mwakyembe alitoa maamuzi hayo jana baada ya kuzungumza na
wafanyakazi wa TRL na kuonekana kutoridhishwa na vitendo vya wizi,
vinavyoendelea katika shirika hilo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Stanley Makunja, Stanley Andrew, Edward Benedicto, Lucy Mtinya, B. Ruoga na Jackson Moses.
Hata hivyo, Mwakyembe alipoombwa na waandishi wa habari, kufafanua
vituo vya kazi vya watuhumiwa hao, alidai kwamba wote ni wa TRL na
wamewajibishwa kama wafanyakazi wa TRL. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Pia, alisema anayo madai na tuhuma nyingi zaidi ya hizo, lakini
hajayahakiki vizuri na anaendelea kuyafanyia uchunguzi na
utakapokamilika atachukua hatua kali zaidi.
“Tumekuwa tukifanya jitihada nyingi sana kuhakikisha TRL ukiwemo
kutoa upendeleo katika bajeti, lakini bado tunakwama kutokana na vitendo
vya wizi vinavyoendelea... watu wanasimamisha treni wanaiba mpaka
mafuta bila hata woga,” alisema.
Alisema, “nimewabembeleza kwa muda mrefu, nimechoka, mara nyingi
nawaambia na kusisitiza wafanye kazi kwa uadilifu na wasiibe, lakini
hawasikii hivyo nimeamua kuchukua hatua hizi kwa kuanzia”.
Akitoa mfano, Dk Mwakyembe alisema kuwa miongoni mwa wizi uliofanyika
ni wizi wa fedha, zinazotozwa katika tiketi za abiria wa treni, ambapo
abiria hutozwa hela halali ya juu, lakini kinachoingizwa katika kopi
inayobaki TRL ni kiasi kidogo, hata robo ya fedha halisi haifiki.
Alisema wafanyakazi hao wamekuwa wanakatisha tiketi na kuweka ganda
gumu chini hivyo kiasi kile hakiingii na baadaye huandika kiasi cha
fedha wanachotaka.
Alisema baadhi ya tiketi alizofanyia uchunguzi, kuna tiketi moja ya
Sh 61,200 ambayo mteja alipewa na kuilipia, lakini fedha iliyoingia
kwenye kopi ya TRL ni Sh 16,200. “Nasema waliofanya hivi wakamatwe na
watiwe rumande mara moja.
Tiketi nyingine ni ya Sh 50,200 ambayo mteja alipewa na kuilipia,
lakini TRL imeandikwa Sh 13,200,” alisema. Alisema “tiketi nyingine ya
Sh 74,200 mteja aliilipia na kopi yake iliyoingia TRL inaonesha ni Sh
13,600 na nyingine ya Sh 57,600 lakini iliyoingia TRL ni Sh 6,700 tu,
halafu mimi nikae kushindana na Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kumwambia
aongeze mishahara wakati hela mnachukua”.
Aidha, Mwakyembe alisema kuwa Tume imeundwa kukagua mabehewa ya
mizigo, yanayoingizwa na kampuni ya India ya Hindustan Engineering and
Industries Ltd (HEIL), yanayodaiwa kwamba yana hitilafu na hivyo
kusababisha ajali.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara kuungana na timu ya wataalamu
wanne kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TRL, Bodi ya Wakandarasi
na Sumatra kuchunguza mabehewa yaliyodondoka na mizigo hivi karibuni,
pia timu hiyo itakwenda India yanapotoka mabehewa kwenda kujiridhisha
kama kuna dosari, basi tutasitisha mabehewa yaliyosalia yasiletwe nchini
na wahusika watachukuliwa hatua,” alisema.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizo alizochukua Dk Mwakyembe, baadhi ya
wafanyakazi wa shirika hilo walionekana kutoridhika nazo kwa madai
kwamba waliofanya ufisadi mkubwa, wakiwemo viongozi waandamizi,
wameachwa na kuchukuliwa hatua wenzao.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Erasto
Kiwele alisema maamuzi aliyochukua Dk Mwakyembe ni maamuzi mepesi, kwa
sababu wapo watu walioleta mabehewa mabovu, wao wameachwa na
hawajakamatwa wala kufukuzwa kazi, isipokuwa wanaofukuzwa ni wanaoiba
mafuta.
“Maamuzi haya ni mepesi sana na hatukuyatarajia, kwa sababu wameachwa
wanaoiba mabilioni na walioingiza mabehewa mabovu yanayodondoka na
kupata ajali kila mara, pia wameachwa viongozi waandamizi wanaofanya
ufisadi wa kukodisha kiberenge kwa Sh 10,000 kwa mwezi, lakini
wamechukuliwa hao wanaofanya wizi mdogo, tunajua wote wizi sio jambo
jema na hatusemi wangepaswa kuachwa, ila ilitakiwa wachukuliwe hatua
wote, maamuzi haya ni mepesi sana” alisema. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment