Friday, March 22, 2013

‘Love and Power’ ya Kanumba kuzinduliwa Leaders Aprili 7

FILAMU ya aliyekuwa nguli wa tasnia hiyo hapa nchini, marehemu Steven Kanumba, inayokwenda kwa jina la ‘Love and Power’ inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Aprili 7, mwaka huu.
Filamu hiyo, ambayo wengi wanasema marehemu Kanumba alijitabiria kifo chake, itazinduliwa kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni jijini Dar es Salaam, huku ikienda sambamba na kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki dunia kwake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mdogo wa marehemu Kanumba, ambaye pia ni kiongozi wa ofisi yake ya ‘Kanumba The Great’ iliyopo Sinza, Seth Bosco, alisema zaidi ya waigizaji 10 kutoka Ghana wanatarajiwa kuwepo siku hiyo.
Alisema mbali na waigizaji hao wa Ghana, pia rafiki wa marehemu, ambaye ni muigizaji maarufu barani Afrika, Mnigeria Ramsey Noah, pia anatarajiwa kuwepo siku hiyo ya uzinduzi.
“Ramsey tulimpigia simu na tukamtaarifu na akasema kuhusu uwepo wake siku hiyo, atatujulisha kabla kama anakuja au la, kutokana na kuwa na majukumu mengi ya kikazi,” alisema Bosco.

Akizungumzia ratiba ya siku hiyo, alisema itaanzia nyumbani kwa marehemu, baada ya hapo wataelekea makaburini na baadaye Leaders kwa ajili ya uzinduzi huo.
Alisema wapenzi na mashabiki wa filamu za Kanumba wanatakiwa kufika asubuhi nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya ibada itakayoanza saa nne asubuhi na kwisha saa tano.
Alisema mara baada ya ibada hiyo, ndugu, jamaa, marafiki, waigizaji pamoja na mashabiki wake watakula chakula cha pamoja kisha kuelekea makaburini.
Aliongeza kuwa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta, ndiyo itahusika siku hiyo kwa upande wa burudani, kisha uzinduzi rasmi utafanyika huku nakala za filamu hiyo zikiuzwa papo hapo.
Marehemu Kanumba alifikwa na mauti Aprili 7, mwaka jana nyumbani kwake Sinza Vatican, huku kifo chake kikihusishwa na msanii wa filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...