Friday, March 22, 2013

WAFUASI WA SHEIKH PONDA WATUPWA JELA

WAFUASI 52 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya maandamano haramu, wamehukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela kwa kila mmoja.


Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, baada ya wafuasi hao kukutwa na hatia kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili. Hata hivyo watakaa jela kwa mwaka mmoja kutokana na adhabu zote kwenda kwa pamoja.


Hata hivyo aliyekuwa mshtakiwa wa 48, Waziri Omar Toy, aliachiwa huru baada ya Mahakama kuridhika kwamba hana hatia kutokana upande wa mashtaka kushindwa kuthitibisha madai dhidi yake.


Baada ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo kusoma hukumu hiyo, ilizuka tafranwi miongoni mwa ndugu wa washtakiwa hao ambapo wengine waliangua vilio na wengine kuanguka na kujigaragaza chini.



Mwanamke ambaye ni ndugu wa washtakiwa hao, alionekana kama mtu “aliyepandwa mashetani” na kutaka kumvamia askari wa kike ambaye katika kujihami alimpiga ngumi, kisha watu wakafanikiwa kumdhibiti kumshika.


Hakimu Fimbo katika hukumu hiyo alisema baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za pande zote pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha mashtaka matatu dhidi ya washtakiwa hao.


Hata hivyo, Hakimu Fimbo alisema kuwa katika shtaka la uchochezi lililokuwa likiwakabili washtakiwa wanne, upande wa mashtaka umeshindwa kulithibitisha.


“Mahakama imeridhika na ushahidi uliwasilishwa na upande wa mashtaka kuwa umethibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa 48,” alisema Hakimu Fimbo na kuongeza:


“Hivyo Mahakama imewatia hatiani washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa 48, katika shtaka la kwanza, la pili na la tatu na katika shtaka la nne, Mahakama imeona kuwa washtakiwa hawana hatia.”


Washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutenda makosa, kufanya maandamano yaliyozuiwa na Polisi na kwa pamoja kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani.


Akitoa adhabu kwa washtakiwa hao baada ya kuwatia hatiani, Hakimu Fimbo alisema: “Nimezingatia kuwa karibu kila mshtakiwa ana majukumu ya kifamilia na kwa kuzingatia `nature’ (asili) ya mashtaka.”


Aliongeza: “Katika kosa la kwanza ninawahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela na kosa la pili pia mwaka mmoja jela na tatu mwaka mmoja jela. Adhabu zote zinakwenda kwa pamoja.”Kauli za Mawakili
Kabla ya adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya aliyekuwa akisaidiana na Wakili Joseph Maugo, aliieleza Mahakama kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya jinai kwa washtakiwa hao na akaiomba Mahakama iwape adhabu kwa mujibu wa sheria.


Kwa upande wake, Wakili wa washtakiwa hao, Mohamed Tibanyendela aliiomba Mahakama iwaonee huruma kwa kuwaachia huru washtakiwa hao au kwa kuwapa adhabu ndogo sana.
Wakili Tibanyendelea alidai kuwa washtakiwa hao ni mara yao ya kwanza kutenda makosa hayo na kwamba wana familia ambazo zinahitaji huduma kutoka kwao huku akidai kuwa wengine tangu walipokamatwa, familia zao hazijui waliko.

Pia Wakili Tibanyendelea alidai kuwa washtakiwa wengine wanaumwa kisukari na shinikizo la damu, huku akitoa mfano wa mshtakiwa wa 21, Kassim Mohamed Chogo, aliyefutiwa mashtaka kuwa alikuwa mgonjwa na ameshafariki dunia.

Ponda ajitetea
Wakati hukumu hiyo ikitolewa, Sheikh Ponda (55) amemaliza utetezi wake akiieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa yeye hana nyaraka za umiliki wa kiwanja cha Malkazi Chang’ombe bali historia ya eneo hilo inawafanya wao kuwa wamiliki.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, Sheikh Ponda alitoa utetezi wake dhidi ya mashtaka matano yanayomkabili yeye na wenzake 49 likiwamo la uchochezi na wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni.

Ponda alidai kuwa awali kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na Taasisi ya Jumuiya ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society(EAMWS) ambayo ilivunjwa na Serikali mwaka 1958 na Serikali kuunda Bakwata.

Akiongozwa na wakili wake kutoa utetezi, Juma Nassoro, Sheikh Ponda alidai; “Bakwata iliundwa ili kusimamia shughuli zilizokuwa zikiendeshwa na Taasisi ya Jumuiya ya Kiislamu ya East African Muslim Welfare Society na siyo mali kama majengo, viwanja na hata shule.
“Tulitumia njia ya mazungumzo ya Kidiplomasia kurejesha kiwanja cha Malkazi Chang’ombe kwa kuzingatia kuwa itatatua mgogoro huo katika njia nyepesi,” alidai Sheikh Ponda.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alimuuliza Sheikh Ponda ni kwa nini hawakuwahi kwenda kuonana na mmiliki wa shule ya Yemeni, ambao nao walinunua eneo hilo la Chang’ombe Malkazi wakaenda kwenye Kampuni ya Agritanza Ltd.

Aliendelea kuhoji kuwa ni kwa nini, pia walikubali kutafutiwa eneo lingine na Kampuni ya Agritanza Ltd kama nyinyi ni wamiliki halali wa lile eneo?

Akijibu hoja hizo, Sheikh Ponda alidai kuwa ; “Tulitumia njia ya kumshawishi mtu ili aweze kuliona tatizo kwa sababu alikuwa na umiliki, ndiyo sababu tulikubali kutafutiwa eneo lingine.

“Wakili Kweka Sheikh Ponda nafikiri unajua taratibu za kisheria, kwa nini ulipoona huo ni mgogoro wa ardhi hukwenda kwenye Mahakama ya Ardhi?”
Sheikh Ponda akijibu, alimwambia wakili huyo kuwa hakuna mahali katika ushahidi wake aliomwambia kuwa mazungumzo yalishindikana bali alisema yalikuwa yanakwenda vizuri ndiyo sababu hakufanya hivyo.

Wakili wa Serikali aliuliza;”Utakubaliana na mimi kuwa mali za Kampuni ya Agritanza Ltd ambazo zinadaiwa kuibwa mlizitumia katika ujenzi wenu wa msikiti wa muda?”

Sheikh Ponda alidai kuwa hilo ni gumu kulijibu, bali wanachotakiwa ni kwenda eneo la tukio ili wathibitishiwe ni kipi kilitumika na kipi hakijatumika.

Baada ya kujibu hilo, Wakili wa Serikali alisisitiza swali hilo ambapo Ponda alimwambia; “Mimi mwenzio nafanya mijadala na Jeshi la Polisi toka enzi za Nyerere sasa tusilete mijadala isiyokuwepo.”

Hata hivyo, Sheikh Ponda alikubali kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliohusika kutoa taarifa kwa maimamu wa misikiti mbalimbali kuwaeleza waumini wao kushiriki kujitolea katika ujenzi wa msikiti wa muda uliojengwa katika eneo la Malkazi Chang’ombe, Oktoba 11 na kukamilika Oktoba 14, mwaka jana.

Alidai kuwa walijenga msikiti huo baada ya kufanya makubaliano na mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Agritanza Ltd, Hafidhi na kukubaliana kuweka alama ambayo kila mwislamu akiiona ataiheshimu na kutofanya shughuli zake binafsi katika eneo hilo na kupendekeza kujenga msikiti huo wa muda.

Kuhusu kukamatwa kwake
Sheikh Ponda alidai kuwa yeye alikamatwa Oktoba 16, 2012, nyakati za saa 4 kasoro robo usiku alipokuwa akijiandaa kuingia katika msikiti wa Tungi Temeke, akipanda ngazi alitokea mtu mmoja aliyekuwa kwenye gari nyeusi aina ya Toyota Harrier akimtaka amfuate.

Anadai alimpuuza na akaamua kuingia ndani ya msikiti huo, lakini alisikia kishindo cha gari na alipogeuka nyumba aliona gari tatu zilizojaa askari wa FFU wakiwa wamebeba silaha.

Aliendelea kudai kuwa, baada ya kuona hivyo aliendelea kuingia ndani lakini alipofika katikati ya msikiti alivamiwa na askari hao ambao walikuwa wamevalia sare zao na viatu na kumbeba kama mtu aliyetekwa nyara kwa kumshika mguu na mkono na kuondoka naye kwa kasi hadi Kituo cha Polisi
Chang’ombe na baadaye Kituo cha Polisi Kati.

Alidai kuwa alipofika huko alielezwa kuwa anatuhumiwa kuwa yeye siyo raia wa Tanzania, ni Mrundi na pia alidhalilishwa kwa lugha ya matusi.
Lakini baadaye alielezwa na askari mmoja kuwa anakabiliwa na tuhuma za kuingia kwa kosa la jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Malkazi.

CHANZO CHA HABARI NI MWANANCHI

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...