Siku moja baada ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kesho atatua jimboni kwake kuzungumza na
wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Uamuzi wa kumfukuza Zitto (pichani) ulifikiwa juzi
ikiwa ni muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi
aliyofungua Januari 2, 2014, dhidi ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu
wa Chadema, iliyokuwa imeshikilia uanachama wake.
Mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ndiye
alitangaza kutimuliwa kwa Zitto akisema ni kutokana na kufungua kesi
mahakamani, kinyume na Katiba ya Chadema kipengele cha 8 (a) (x). Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Jana, Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) aliongoza kikao cha kamati hiyo,
kilichojadili taarifa ya Tanesco na baadaye alisisitiza kwamba hana
taarifa rasmi ya uamuzi wa mahakama na atakapoipata atazungumzia hatima
yake.
“Kama mnavyoona mimi naendelea na kazi na wala
sina taarifa rasmi lakini nikipata taarifa rasmi na mimi nitatoa taarifa
rasmi, Ijumaa (kesho) ninakwenda jimboni kuzungumza na wapigakura wangu
ambao niliwaahidi kufanya hivyo kabla ya vikao vya Bunge kuanza Jumanne
ijayo,” alisema Zitto ambaye taarifa zinasema alikuwa amepapanga
kuwaaga wapiga kura na baadaye kutimkia kwenye chama kipya cha ACT
alichokiasisi.
“Muhimu kwangu ni kufanya kazi ya Watanzania na
nitafanya kwa mazingira yoyote yale. Siasa yangu inajikita katika
masuala, siyo watu, ukiandika kuhusu Zitto siyo kwa ajili ya mtu bali
masilahi ya Taifa.
“Nakuzwa, nakomazwa na hii ni changamoto, nitaendelea kufanya kazi zangu hadi nitakapopata taarifa rasmi.”
Mwanasheria wa Zitto, Albert Msando juzi
aliliambia gazeti hili kwamba, anafuatilia uamuzi huo wa mahakama kabla
ya kuona ni hatua gani watazichukua.
ACT wachekelea
Baadhi ya wanachama na viongozi wa Chama cha ACT
mkoani Kigoma wamedai kufurahishwa na uamuzi huo, wakidai kuwa
utakinufaisha chama hicho.
Mkazi wa Mwandiga, Dunia Pemba alisema Zitto
alipaswa kujiondoa ndani ya Chadema pale tu alipovuliwa nyadhifa zake
ili atazame sehemu nyingine yenye demokrasia pana kwa vile chama hicho
kilionyesha hakimhitaji tena. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
“Sisi tulitangulia huku ACT na sasa tunamsubiri
kwa hamu, aje kujenga chama hiki ambacho ni tishio kubwa hapa nchini na
bila shaka kitachukua viti vingi vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka huu, ndiyo maana kutimuliwa kwa Zitto Kabwe ni faraja kwetu kwa
sababu atapata muda wa kutosha kujenga chama,” alisema Pemba.
Pia, mwenyekiti wa vijana wa ACT Tawi la Mwandiga, Stili Chuma
alisema anafurahia uamuzi ya Chadema ingawa kitendo cha jimbo lake
kukosa mwakilishi kinasikitisha.
Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo la Kigoma
Kaskazini, Shaban Kasugulu alipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu akidai haki
imetendeka kwa vile suala la Zitto na Chadema lilichukua muda mrefu na
kusababisha watu kukosa mwelekeo.
Hata hivyo, Boaz Chuma aliitupia lawama Mahakama
Kuu kwa kuibeba Chadema katika shtaka hilo kutokana na kutoa hukumu siku
ambayo haikupangwa.
Dk Makulilo
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Alexander Makulilo alisema kufutwa uanachama kwa Zitto ni fundisho
kwa wananchi ambao licha ya kuchagua mbunge wanayempenda, lakini anaweza
kuondolewa na vyama vyao.
“Wananchi wanamchagua mbunge wao kupitia chama cha
siasa lakini hawawezi kumwajibisha hadi baada ya miaka mitano,” alisema
na kuongeza kuwa ni chama pekee kinachoweza kumwajibisha.
Dk Makulilo alisema katika rasimu ya Katiba
iliyokuwa ikipendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulikuwa na
kipengele kilichotaka wananchi wawe na uwezo wa kuwajibisha wabunge wao,
lakini kikaondolewa na Bunge Maalumu la Katiba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel
Mallya kuondolewa kwa Zitto ni taratibu na kanuni za chama
kilichompitisha kugombea nafasi hiyo na hapo ndipo unaona umuhimu wa
kuwapo mgombea binafsi ili wananchi wawe na nguvu zaidi,” alisema
Mallya.
Mbunge wa Mbarali, Modesti Kilufi alisema bado wanaamini Zitto ni mbunge, bado ni mwenyekiti wangu na anaweza kukata rufaa. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment