Basi la Majinja likiwa limeangukiwa na kontena na kusababisha vifo katika eneo la Changalawe mafinga.
Watu 42 wamepoteza maisha na wengine 23
kujeruhiwa baada ya lori la mizigo kugongana na basi na kontena
lililokuwa limebebwa kuangukia gari hilo la abiria, katika ajali ya aina
yake iliyotokea eneo la Mafinga Changalawe mkoani Iringa.
Watu 37 waliokuwa kwenye basi hilo la kampuni ya
Majinjah Express lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam,
walifariki papo hapo na wengine watano kufariki wakiwa Hospitali ya
Mafinga. Dereva wa basi na wa lori hilo la kampuni ya Cipex, pia
wamefariki.
Shuhuda mmoja wa ajali hiyo, Nyasio Pascal,
aliyekuwa akiendesha basi la Saibaba, alisema aliliona lori hilo
likijaribu kukwepa mashimo kwenye barabara hiyo ambayo ni nyembamba, na
mara likaanza kuyumba kulia na kushoto baada ya kukanyaga shimo na ndipo
lilipolifuata basi na kugongana nalo.
Alisema kontena lililokuwa limebebwa na lori hilo,
liliangukia juu ya basi na kulikandamiza, jambo ambalo lilisababisha
vifo vya watu wengi na pia kuzuia watu waliokuwa karibu na ajali kuokoa
watu waliojeruhiwa hadi tingatinga lilipowasili. Hata hivyo, alisema
mtoto mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja, alinusurika kwenye ajali hiyo
bila ya kudhurika. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Miili ya waliokufa imehifadhiwa kwenye Hospitali
ya Mafinga, ambayo ina chumba cha kuhifadhia miili ya watu saba tu, na
mingine imepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Iringa.
“Hii ni ajali mbaya ambayo haijawahi kutokea
mkoani hapa,” alisema mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliyefika
eneo hilo la ajali.
Wanaume saba na wanawake 35 wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo, iliyochukua maisha ya watoto watatu.
Katika eneo hilo ambako ajali hiyo imetokea hali
ilikuwa mbaya kutokana na kontena la lori hilo kulalia basi na
kukandamiza miili ya abiria, jambo ambalo lilisababisha ugumu katika
kuokoa abiria waliokuwemo ndani ya basi.
Polisi wakishirikiana na watoa huduma ya afya
kutoka Mufindi walifika kusaidia katika kutoa huduma ili kuokoa wale
ambao walikuwa wamejeruhiwa na kuhitaji matibabu ya haraka.
Tingatinga lilifika na kusaidia kulinyanyua
kontena na hivyo kurahisisha kazi ya kutoa miili ya wale waliokuwa
wamebanwa na miili ya waliokufa pia.
Majeruhi wazungumza
Kevin Humprey, aliyekuwa amekaa viti vya nyuma
kwenye basi hilo, alisema alisikia kishindo kimetokea na kuona kontena
limelalia sehemu kubwa ya basi.
“Baada ya kuona hivyo, nilianza kupiga kelele za kuomba msaada kwa kuwa tulikuwa porini,”alisema Humprey.
Abiria mwingine aliyekuwa amekaa viti vya nyuma, Josam Obel, alisema alishtukia tu kontena likiwa limelalia gari lao.
Alisema lori lililokuwa linakwenda Mbeya liliacha
njia kutokana na mashimo yaliyokuwepo barabarani na kugongana uso kwa
uso na kusababisha kontena lililokuwa limebebwa na lori kuangukia kwenye
basin a kulikandamiza.
Alisema basi hilo lilikuwa na abiria wengi kuliko
uwezo wake kwa kuwa lina uwezo wa kubeba abiria kati ya 50 na 54, lakini
lilibeba zaidi ya abiria 60.
Hali mbaya katika Hospitali ya Mufindi
Hali katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi ilikuwa
mbaya kutokana na watu wengi kufurika kutaka kujua kama ndugu zao ni
kati ya hao walikufa au kujeruhiwa kwenye ajali hiyo.
Vilio vilitanda kila kona ya hospitali hiyo hasa
wakati miili ya waliokufa ilipokuwa ikishushwa na kuwekwa eneo maalumu
kwa ajili ya utambuzi, jambo lililofanya kazi hiyo kuwa ngumu kutokana
na kila mtu kutaka kuona maiti hizo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Boaz Mnenegwa
alisema walipokea miili ya watu 37 ambao walikufa kwenye ajali na kwamba
wengine watano walifia hospitalini.
Alisema majeruhi 23 walifikishwa hospitalini hapo
na kati yao watano walifariki na wengine zaidi ya 10 wamepelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
“Majeruhi hao wameumia maeneo mbalimbali ya mwili ikiwemo kichwani, miguuni na mikononi,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa magari hayo mawili.
Alisema madereva wa magari yote waliofahamika kwa
majina ya Baraka Gabriel wa basi na Makka Sebasian wa lori walikufa papo
hapo na haikuweza kujulikana idadi ya watu waliokuwamo kwenye lori
hilo.
Hata hivyo, Kamanda Mungi alisema ni vigumu kupata majina ya
waliokufa na majeruhi kutokana na shughuli za kutafuta kuendelea ili
kuweza kuwatambua.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa ajali hiyo ni mbaya ambayo haijawahi kutokea katika mkoa huo
“Tuko hapa kwa ajili ya kuhifadhi maiti na kutambua ndugu wa marehemu,” alisema.
Masenza aliongeza kuwa barabara hiyo imekuwa na
ubovu kila mara, hasa wakati wa mvua inapochimbika na kuweka mashimo
ambayo yalichangia ajali ya jana kwa sababu gari zote zilikuwa
zikipishana na kukwepa mashimo hayo.
Dereva wa basi la Saibaba, Nyasio Pascal aliungana
na mkuu huyo wa mkoa akisema: “Sisi kama madereva ambao tunatumia
barabara hii, kiukweli tunakerwa na kipande hiki cha barabara kwa sababu
ya mashimo na ni finyu hamuwezi kupishana kwa hiyo ajali hii imetokea
kwa sababu ya ubovu wa barabara,” alisema. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
No comments:
Post a Comment