Thursday, January 22, 2015

TTCL YAFILISIKA

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk Kamugisha Kazaura

KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imetangazwa kufilisika, kutokana na kutokuwa na mtaji baada ya mwekezaji, Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel, kushindwa kuwekeza kwa miaka 14.
Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) imeamua kupeleka suala hilo bungeni ili kuweka mipango ya kimkakati kuifufua kampuni hiyo. Kwa kuanzia, Msajili wa Hazina amepewa kazi ya kufanya tathmini ya kina.
Hayo yalibainika jana katika kikao cha uongozi wa kampuni hiyo na kamati hiyo, inayoongozwa na Kabwe Zitto, iliyotaka kufahamu maendeleo ya kampuni hiyo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa katika ushindani wa huduma za simu hususani katika siku za mkononi.
Umekuwepo pia mvutano mkali baina ya Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel kuhusu hatima ya asilimia 35 ya hisa, ambazo kampuni hiyo inamiliki ndani ya Kampuni ya TTCL. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Dk Kamugisha Kazaura aliieleza Kamati ya Bunge kuwa kutokana na hasara kubwa ya kiasi cha Sh bilioni 334.5 mpaka kufikia mwaka 2013 na kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji hasi wa Sh bilioni 87.9, kwa sasa ni mufilisi.
Alisema hatua hiyo, inatokana na mbia mwenye hisa kwa asilimia 35, kutofanya uwekezaji mkubwa tangu waingie ubia mwaka 2001, jambo ambalo limesababisha pia uchakavu wa miundombinu na kupungua kwa ubora wa huduma.
Kutokana na hatua hiyo ya kutokuwekeza, kampuni hiyo ilimtaka mwekezaji huyo kuondoa umiliki alionao, ambapo Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru alisema kampuni hiyo ya India, ambayo ni Kampuni mama ya Airtel Tanzania, inataka ilipwe Sh bilioni 14 licha ya kuwa haijawahi kuwekeza chochote ndani ya TTCL, kama ilivyo kwa watangulizi wake; Celtel Tanzania, Celtel International na Zain.
Lakini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Patrick Makungu alisema Baraza la Mawaziri limeunda jopo la majadiliano na mwekezaji huyo, kuzungumzia gharama za kumlipa ili kuondoka katika kampuni hiyo ya TTCL na hawana taarifa ya kiwango hicho cha fedha kilichotajwa.
“Mitambo mingi ni chakavu, kutokana na kutowekeza katika teknolojia za kisasa kwani kampuni nyingine za simu za mkononi kila mwaka zimekuwa zikiwekeza dola milioni 100 kuboresha huduma,” alisema.
Alisisitiza kuwa kwa mwaka 2012, mapato ya kampuni hiyo yalikuwa Sh bilioni 92.4 lakini mwaka uliofuata yaliongezeka kwa asilimia moja na kufikia Sh bilioni 93.6 baada ya jitihada mbalimbali katika kukuza teknolojia.
Akizungumzia hasara ya kampuni hiyo, alisema mwaka 2012 hasara ilikuwa Sh bilioni 20.8 na mwaka 2013 ilikuwa Sh bilioni 16.2, jambo linalosababisha hali ya fedha kuwa mbaya na kushindwa kukopesheka kutokana na serikali kushindwa kuwadhamini.
Alisema asilimia 50 ya miundombinu ya kampuni hiyo ni chakavu huku wakitegemea mapato kwa kutumia wateja. Alitaka serikali kuwafutia deni la Sh bilioni 76 wanazodaiwa baada ya kukopeshwa serikali ilipouza hisa zake na kutumia kulipa wafanyakazi waliostaafu.
Dk Kazaura alisema uhaba wa fedha, pia unasababishwa na madeni mengi kampuni hiyo inadai idara na taasisi ya serikali, ambapo hadi kufikia Septemba 2014 walikuwa wakiidai Sh bilioni 3.2 na dola za Marekani milioni mbili, hivyo waliomba Hazina kusaidia kwa kukata taasisi na idara hizo moja kwa moja kwenye mafungu yao.
Alisema licha ya changamoto hizo, bado wanadaiwa na wazabuni, Mamlaka Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine za kimataifa, jambo lililofanya TCRA kuwaagiza kulipa madeni hayo hadi Oktoba 31,mwaka jana, vinginevyo watafutiwa leseni .
Lakini, pia alisema wanaiomba serikali kuangalia namna ya kuwaongezea mtaji kufikia dola milioni 711 ili kufufua shirika, ikiwa ni pamoja na kuwamilikisha rasmi mkongo wa taifa wa mawasiliano, ambao kwa sasa wanausimamia baada ya kukamilika kwa awamu mbili.
“Pia tunahitaji kurekebisha muundo wa kampuni kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi wanaofikia 1,550 na wengi wao ambao ni asilimia 50 wana miaka zaidi ya 50 na elimu isiyozidi kidato cha nne, hivyo lazima kuchambua watakaoweza kuendana na teknolojia na ikibidi wengine kuwapisha wenye uwezo,” alisema.
Waliomba serikali pia kuangalia suala la taratibu na sheria za manunuzi ili kusaidia ushindani wa kibiashara na kampuni nyingine za simu za mikononi, ambazo ni binafsi na taratibu zake hazichukui muda mrefu.
Alizungumzia pia suala la gharama kubwa za intaneti ya TTCL kuwa inatokana na ubora wake na uhakika kwa huduma zinazotolewa huku akitaka wananchi kuwaunga mkono katika huduma hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kabwe Zitto alisema watapeleka bungeni suala hilo ili litolewe maamuzi ya pamoja na wabunge na kuweka mikakati ya kunusuru kampuni hiyo yenye kukabiliwa na madeni, ukosefu wa mtaji pamoja na kufanya maamuzi ya kwa kuondoka kwa mwekezaji.
Alisema wamemtaka Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya majadiliano na kupeleka taarifa katika kamati hiyo siku ya Ijumaa ili kutafuta njia ya kunusuru kampuni hiyo na kuhakikisha inafanya kazi kwa faida na kushindana na kampuni nyingine.
Zitto alisema baadhi ya maamuzi yaliyofanywa kwenye kampuni hiyo, ikiwemo leseni na masafa yake kutumiwa bure na kampuni ya Celtel ambayo sasa ni Airtel na kufanya TTCL sasa wanatafuta upya.
“Kampuni kwa sasa imefilisika kutokana na kuwa na mizania ya bilioni 157 ya ziada lazima maamuzi yafanyike na tathmini kupelekwa bungeni ili yafanyike maamuzi sahihi,” alisema Zitto.
Februari 21, 2001, TTCL ilisaini mkataba na Kampuni ya SMI/Detecon, ambayo ilinunua asilimia 35 ya hisa kwa Dola za Marekani 120 milioni (Sh bilioni 198).
Hata hivyo, kiasi kilicholipwa ni Dola 65 milioni tu (Sh bilioni 107.3) kwa ahadi kwamba kiasi kilichosalia, kingelipwa baada ya hesabu za TTCL kukaguliwa.
Baadaye MSI/Detecon ambao ulikuwa ushirika wa Kampuni ya Mobile Systems International ya Uholanzi na Detecon ya Ujerumani, ilitumia leseni ya biashara ya simu za mkononi iliyokuwa mali ya TTCL, kuanzisha Celtel Tanzania.
Baada ya kuundwa kwa Celtel Tanzania, TCCL walipewa umiliki wa asilimia 40 ya hisa, baada ya muda mfupi, hisa hizo zilihamishiwa Hazina, hivyo kuiacha TTCL bila hisa wala biashara ya simu za mkononi.
Katika mchakato huo, Celtel Tanzania iliuzwa kwa Celtel International ambayo baadaye iliuzwa kwa Zain. Juni 2010, Zain iliuzwa kwa Kampuni ya Bharti Airtel Limited ambayo ndiye mmiliki Airtel Tanzania. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

Na Habari Leo

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...