Thursday, January 22, 2015

JANGA LA TATU JESHI LA POLISI


 
Jeshi la Polisi Tanzania, limekumbwa na janga la tatu katika kipindi kisichozidi miezi saba baada ya watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kuvamia na kuua askari wake wawili katika Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji juzi na kisha kupora bunduki saba na risasi 60.
Tukio hilo limefanya jumla ya askari waliouawa kufikia watano huku bunduki 22 na risasi zaidi ya 120 zikiwa zimeporwa baada ya kuvamiwa kwa vituo vitatu vya polisi tangu Juni 11 mwaka jana.
Mbali na Ikwiriri, vituo vingine vilivyovamiwa ni Mkamba Kimanzichana, Mkoa wa Pwani na Bukombe mkoani Geita.
Matukio hayo yametokea ikiwa ni mwaka mmoja na wiki tatu tangu Ernest Mangu alipoanza kazi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) akimrithi mtangulizi wake, Said Mwema. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Tukio la juzi
Watu 15 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za kivita na mabomu ya kurusha kwa mkono walivamia Kituo cha Ikwiriri ambacho ni kikubwa kuliko vyote wilayani Rufiji ambacho pia ni makao makuu ya polisi ya wilaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo ambalo ni la pili kutokea katika kipindi cha miezi saba mkoani humo, Koplo Edgar Milinga wa Kikosi cha Usalama Barabarani aliuawa kwa kukatwakatwa mapanga na mwenzake, Judith Timoth alipigwa risasi na kufariki dunia.
Kamanda Matei alizitaja silaha zilizoporwa kuwa ni SMG mbili, Shortgun moja, SR mbili na bunduki za kurushia mabomu ya machozi mbili. Kamanda Matei aliapa kuwasaka majambazi hao.
Ilivyokuwa
Habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zimesema kuwa majambazi hao walivamia kituo hicho saa nane usiku na kuwakuta askari hao wawili na kuwapiga risasi.
Mmoja wa wakazi wa Ikwiriri, Arafa Ngwaya alisema usiku wa kuamkia, jana kulisikika milio ya risasi na milipuko ya mabomu lakini hakujua kilichokiwa kinaendelea.
“Inawezekana lengo lilikuwa ni kutisha wananchi na polisi wasitoke nje kutoa msaada wakati wakitekeleza shambulio hilo,” alisema.
“Tumepatwa na taharuki kubwa. Inaonekana walijizatiti vilivyo,” alisema mkazi wa eneo hilo, Mohamed Said.
Alisema majambazi hao walifyatua risasi mfululizo bila kusimama jambo lililokuwa likiashiria kwamba walikuwa wamejizatiti vilivyo.
Viongozi wa mkoa watoa neno
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndekilo ambaye ana mwezi mmoja na nusu tangu alipohamishiwa Pwani, aliwataka wakazi wanaowafahamu watu hao kutoa taarifa kwa siri ili kuwakamata.
“Tutahakikisha tunawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, wote waliohusika na tukio hili,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya alisema: “Nimesikitishwa na tukio hili, sisi tunakimbilia polisi kwa ajili ya usalama, lakini watu wanawaua polisi, ni tukio la kulaaniwa. Tutapambana kila mahali kuhakikisha wote waliofanikisha kitendo hiki wanakamatwa.”
Alisema baada ya tukio hilo na lile la Mkuranga mwaka jana, kamati yake itaweka mkakati wa kuvilinda vituo vya polisi hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi.
Uharibifu
Babu alisema baada ya kuua askari, majambazi hayo yalitoboa matairi ya magari na pikipiki zote zilizokuwapo kituo hapo ili kuwazuia polisi kuwafuatilia.
Alisema: “Gari la Mkuu wa Polisi wa Wilaya na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya yameharibiwa kwa risasi.” Alisema gari la polisi kituoni lilipigwa risasi matairi yote wakati gari la OC - CID lilipigwa risasi kwenye kioo cha kulia na kutokea kushoto.
Alisema baada ya tukio hilo, wananchi walikusanyika kituoni hapo kushuhudia na kusikiliza kauli zozote kutoka kwa viongozi wao na kuwapa pole askari.
Babu alisema baada ya tukio hilo polisi kutoka makao makuu walifika kwa helikopta kusaidia utafutaji wa majambazi hao. Aliwataka wananchi kuwa watulivu wakati jitihada za kuwatafuta wahalifu hao zikiendelea. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Askari akerwa
Mmoja wa maofisa wa Polisi ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema kuwa kituo kikubwa kama hicho kilipaswa kuwa na askari wa kukilinda hasa kwa kujifunza kwa tukio lililotokea wilayani Mkuranga mwaka jana.
Alisema askari waliouawa walikuwa mapokezi huku kukiwa hakuna askari aliyekuwa akilinda kituo hicho.
“Mahali popote kwenye silaha panatakiwa kuwa na mlinzi nje lakini haya hayafanyiki, ndiyo maana majambazi hayo yanapata mwanya,” alisema.
Alisema polisi wanapaswa kujichunguza wenyewe ni kwa nini majambazi wanapata mwanya wa kuvamia vituo vyake kama hakuna taarifa zinazovuja kwenda kwa majambazi hao.
Janga la kwanza
Tukio kama hilo lilitokea Juni 11, 2014 baada ya majambazi kuvamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Mkuranga na kuua askari mmoja, mgambo mmoja na kujeruhi mgambo mwingine na kisha kupora bunduki tano na risasi 60. Waliouawa ni Konstebo Joseph Ngonyani na Venance Francis wakati Mariamu Mkamba alijeruhiwa.
Janga la pili
Pia, Septemba 7, mwaka jana, askari polisi wawili, G.2615 Dunstan Kimati na WP 7106 Uria Mwandiga waliuawa na bunduki 10 aina ya SMG na risasi ambazo idadi yake haikujulikana kuporwa katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Bukombe baada ya watu ambao hawajafahamika kuvamia kituo hicho saa 9.45 usiku na kuwashambulia askari polisi waliokuwa zamu. Wengine watatu walijeruhiwa.
Baadaye polisi walitangaza kupatikana kwa baadhi ya silaha hizo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...