Friday, January 23, 2015

CCM YAREJESHA AMANI SUDAN KUSINI

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini (kushoto), Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan, Dk Riek Machar (wa pili kulia) na Deng Alor Kuol wakitia saini mkataba wa makubaliano ya kukiunganisha upya chama cha SPLM cha Sudan Kusini katika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha juzi usiku. Nyuma yao ni mjane wa marehemu, John Garang aliyekuwa Mwenyekiti wa SPLM, Rebecca Nyandeng de Mabior na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Thobias Makoba. Nyuma yao wakishuhudia utiaji saini huo ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda. (Picha na Ikulu).
BAADA ya miezi mitano ya mazungumzo ya kurejesha amani Sudan Kusini yaliyoratibiwa na chama tawala, CCM, hatimaye Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na hasimu wake, Riek Machar wamesaini makubaliano ya kusitisha mapigano, yaliyoibuka tangu mwaka 2011.
Kutokana na machafuko hayo, zaidi ya raia 20,000 wa Sudan Kusini, wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya milioni moja wakikosa makazi.
Walisaini makubaliano hayo juzi usiku jijini hapa, huku marais wa ndani na nje ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, wakishuhudia.
Wengine walioshuhudia makubaliano hayo ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Naibu Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa , Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Salva Kiir, Riek Machar na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Kutokana na makubaliano hayo ya kihistoria yenye lengo la kurejesha amani ya taifa hilo changa, lililojitenga kutoka Jamhuri ya Sudan yenye makao yake makuu Khartoum, Rais Kikwete aliwapongeza Salva Kiir, Machar na kundi jingine la tatu ambalo baadhi ya viongozi walikamatwa na kuwekwa kizuizini nchini humo na kuwaambia kuwa makubaliano hayo zaidi ya 40, wahakikishe wanayazingatia ili amani na upendo vitawale nchini mwao.
Makubaliano hayo ambayo awali yalikuwa yasainiwe juzi saa 8:00 mchana, yalisainiwa saa 2:30 baada ya makubaliano rasmi.
Baadhi ya makubaliano hayo ni pamoja na kufanyia marekebisho katiba ya chama tawala nchini humo cha SPLM, kupunguza madaraka ya Rais, kuongeza idadi ya wajumbe katika kamati kuu ya chama, kukubali kuwajibika wote kwa yote yaliyotokea na kuwaomba msamaha wananchi wa Sudan Kusini kwa kuwasababishia machafuko na vita.
Mengine ni haki ya kila mwanachama kugombea uongozi, kuleta mabadiliko ya kidemokrasia katika chama, utawala bora na uwazi katika chama na kutumia makubaliano ya Arusha kuharakisha mazungumzo ya Addis Ababa (Inter Governmental Authority Development (IGAD).
Mara baada ya maazimio hayo kusomwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliwaomba kutimiza kwa dhati maazimio waliyojiwekea na kuyatekeleza kwa faida ya nchi yao.
Rais Kikwete aliyeungana na marais wenzake na viongozi wengine wa kimataifa, kushuhudia tukio la kihistoria la utiaji saini ya makubaliano ya amani na kusitisha mapigano katika nchi mpya ya Sudan Kusini; alisema “Nawapongeza kwa hatua hii mliyofikia mlipokuja kuniomba kuwasaidia kutatua tatizo lenu la vita. “Nilijiuliza maswali mengi, lakini nashukuru nimeshirikiana na wenzangu wa CCM kuhakikisha amani Sudan ya Kusini inapatikana kupitia chama, hivyo nawasihi kuhakikisha mnasimamia haya mliyoyasaini ili kuleta maendeleo kwa nchi sambamba na kuleta amani na furaha ndani ya nchi yenu”.
Kikwete alisema kila kiongozi kabla ya kufanya kitu ni lazima atafakari mara mbili jambo lolote analotaka kufanya, kuwa lina faida kwa wananchi wa nchi hiyo au la.
“Lakini mkiyatekeleza makubaliano haya, kila kitu kwenu kitakuwa rahisi na hakuna litakaloshindikana kwenu na kuna usemi wa Kiswahili usemao kuzaa si kazi, kazi kulea mwana , hivyo nawasihi mkayasimamie haya,” alisema.
Rais Kenyatta aliwapongeza kwa kukubali kusaini makubaliano hayo na kuwakaribisha kwake pale watakapohitaji msaada wowote kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya nchi hiyo.
Kwa upande wa Rais Museveni, aliungana na wenzake kuwapongeza kwa kufikia hatua hiyo na kusema nchi hiyo ni ndugu wa karibu na Uganda na hivyo imekuwa furaha kuona sasa wanakwenda kutulia bila mapigano. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
“Hata hivyo napenda kuwapongeza hawa wenzetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukubali kuratibu mazungumzo haya hadi kufikia hapa na nasema ni vyema ukiona ndugu yako amekosea, Waswahili husema hatuwezi kuambizana ukweli kitu ambacho kinatugharimu,” alisema.
Baada ya hatuba hizo za wosia kwa wapinzani hao ndani ya chama kimoja, Rais Salva Kiir na mpinzani wake, Riek Machar ambaye ndiye aliyekuwa Makamu wa Rais kabla ya mtafaruku, walionekana wenye furaha muda wote na kupongezana kwa kupeana mikono mara kwa mara, huku wakishangiliwa na wapambe wao waliofurika ndani ya ukumbi wa Ngurudoto, jijini Arusha.
Wapinzani hao wote kwa pamoja waliahidi kutimiza kwa vitendo makubaliano hayo na kupeana ushirikiano katika mambo yote na kuwashukuru wote waliohusika kusuluhisha ugomvi huo hadi kufikia hatua hiyo.
Alikuwepo pia Rebecca Nyandeng De Mabior, mjane wa kiongozi wa kwanza wa chama cha SPLM, John Garang, ambaye ndiye aliyeongoza harakati za kupigania uhuru, kuelekea kujitenga kwa nchi hiyo, kutoka kwa iliyokuwa Jamhuri ya Sudan.
Mazungumzo ya awali ya vikundi vinavyozozana katika chama cha SPLM yaliongozwa na ujumbe mzito wa ngazi ya juu wa CCM ili kutafuta suluhu ya mgogoro ndani ya chama hicho, kinachotawala nchini Sudan Kusini.
Ujumbe huo uliongozwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na Kinana.
Kwa upande wa SPLM, mazungumzo hayo yaliongozwa na Taban Deng Gai, Daniel Awet Akot, na Deng Alor Kuol. Miongoni mwa makundi hayo ni kutoka chama cha SPLM, kundi kutoka kwa wafungwa wa kisiasa, pamoja na kundi lililojitenga kutoka chama cha SPLM.
Chama hicho kiligawanyika makundi matatu na kusababisha jeshi kwa upande wake, kumeguka katika makundi hayo na kusababisha wananchi nao kugawanyika katika makundi hayo matatu .
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Norway, Misri, Umoja wa Mataifa (UN) na Ethiopia. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...