Friday, January 23, 2015

MWAMUZI YANGA, RUVU AFUNGIWA

Mshambuliaji wa Yanga, Amis Tambwe 
SIKU moja baada ya Klabu ya Yanga kulalamika kudhalilishwa kwa mchezaji wake, Amisi Tambwe katika mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting, Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemwondoa kuchezesha mechi za Ligi Kuu mwamuzi wa pambano hilo kwa kushindwa kulimudu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama, mwamuzi huyo Mohammed Theofil ameondolewa kuchezesha ligi hiyo ya Tanzania Bara kwa kipindi kilichobaki.
Katika mchezo huo uliochezwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam na kusimamiwa na mwamuzi huyo wa kati, timu ya Ruvu Shooting ilionesha mchezo wa kibabe ambapo baadhi ya wachezaji wake walifanya vitendo vya utovu wa nidhamu pasipo kuadhibiwa.
Mchezo huo ulisababisha mshambuliaji wa Yanga, Tambwe ambaye ni raia wa Burundi, kulalamika kwamba alidhalilishwa, huku akidai kuumizwa baadhi ya maeneo ya mwili wake na akidai kuwa aliitwa mkimbizi.
Lakini akizungumza jana akiwa jijini Mwanza, Chama ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Katibu wa Chama cha Soka Kagera, alithibitisha kuondolewa kwa mwamuzi Theofil. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

“Ndio, ni kweli tumemwondoa mwamuzi Mohammed Theofil wa Morogoro kwa kushindwa kumudu mchezo huo wa Yanga na Ruvu Shooting,” alisema Chama na kuongeza: “Tarehe sita mwezi ujao, Kamati (ya Waamuzi) itakutana na kupitia CD ya mchezo pamoja na taarifa ya Kamisaa wa mchezo huo na kuchukua hatua zaidi kwa mwamuzi kama itaonekana anastahili adhabu zaidi.”
Alisema kwa sasa wamechukua hatua ya kumwondoa katika kuchezesha Ligi Kuu kwa sababu katika ratiba yao mpya kwa mechi zijazo za Ligi Kuu, mwamuzi huyo alikuwa amepangwa kuchezesha mechi nne, hivyo wameona si vyema kumwacha aendelee kuchezesha mechi zaidi.
“Kwa sasa tumeamua kumwondoa asichezeshe, na kwa hiyo huu ni uamuzi wa dharura kwa sababu tumeona kuwa ana mechi nyingine nne ambazo kwa ratiba mpya ya waamuzi alikuwa amepangwa kuchezesha, kwa hiyo tumeona asiendelee na mechi hizo,” alisema Chama.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema jana hatua iliyochukuliwa dhidi ya mwamuzi huyo ni ya kwanza kwani wao walipendekeza waamuzi wote waliokuwepo katika mchezo huo waadhibiwe. Pia alisema wanapenda kuona baadhi ya wachezaji waliomdhalilisha Tambwe wanachukuliwa pia hatua za kinidhamu.
“Tumefurahi kwa hatua hiyo, lakini tunasema ni ya kwanza, tulipendekeza iwe kwa wote, tunasubiri kauli ya TFF na hatua zaidi dhidi ya wengine,” alisema Muro ambaye kesho timu yake inaikabili Polisi Moro mjini Morogoro.
Miongoni mwa mambo waliyopendekeza juzi ni TFF kuchukua hatua kali dhidi ya wale waliohusika kwa utovu wa nidhamu aliyofanyiwa Tambwe kwa kuzingatia sheria na kanuni za soka. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...