Zikiwa zimebaki siku tatu kabla
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza mjini Dodoma, sasa hakuna shaka
kwamba Rais Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri
wakati wowote kuanzia leo na kabla ya Jumapili (saa 48) kutokana na
kukabiliwa na safari ya nje.
Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko hayo baada ya
kumwondoa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kwa kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye
akaunti yake.
Mwingine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, ambaye anatuhumiwa kutoshughulikia kwa makini sakata
hilo na kusababisha Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo kwa uwezekano
mkubwa wa kumvua uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya mabadiliko madogo
kwenye baraza lake, ikiwa ni miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunja
Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza mabadiliko hayo wakati wowote kuanzia leo. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
“Rais anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi
kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa
jinsi yoyote ile ni lazima atangaze baraza kesho (leo) au Jumamosi,”
alisema mpashaji habari wetu.
“Hawezi kutangaza baraza jipya akiwa nje ya nchi,
hivyo ni lazima atangaze kesho (leo) au ikishindikana Jumamosi ili
Jumapili afanye shughuli nyingine na kuondoka.”
Hata hivyo, mabadiliko ya mwisho ya Baraza la
Mawaziri yalitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye pia
anaweza kupewa kazi hiyo.
Baada ya kujadili sakata la uchotwaji wa fedha
hizo kwa takriban siku nne, Novemba 28, mwaka jana Bunge lilifikia
maazimio manane, likiwamo la kutaka wote waliohusika kwenye kashfa hiyo
wachukuliwe hatua na mamlaka husika, akiwamo Profesa Muhongo ambaye Rais
Kikwete alisema Novemba 22, 2014 kuwa amemuweka kiporo hadi baada ya
“siku mbili au tatu” kusubiri matokeo ya uchunguzi.
Hata hivyo, shinikizo liliongezeka baada ya Kamati
Kuu ya CCM, iliyokutana Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete,
kuitaka Serikali iwe imetekeleza kwa vitendo maazimio yote ya Bunge
kuhusu sakata hilo kabla ya kikao cha Bunge kitakachoanza Jumanne ijayo
na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana za uteuzi wachukuliwe hatua
stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara moja.
Pia, Kamati ya Maadili ya CCM iliyokutana Dar es
Salaam mapema wiki hii, iliwajadili wanachama waliohusika kwenye kashfa
hiyo na kupeleka taarifa yake kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa hatua
zaidi.
Wakati CCM ikisema hayo, wabunge wamekuwa
wakimkumbusha kiongozi huyo wa Serikali kuchukua hatua kabla ya kikao
cha Bunge. Wabunge wawili wa mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua
Nassari wote kupitia Chadema, wamediriki kusema kuwa watamwondoa Profesa
Muhongo kwa mabavu kwenye ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria
iwapo Rais hatakuwa amemuondoa.
Pia, nchi wahisani zilieleza mapema mwezi huu kuwa
pamoja na kuruhusu kiasi cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo,
bado zinasubiri tamko la Serikali kuhusu sakata hilo, ikiwa ni pamoja na
hatua ilizochukua kuzuia kashfa kama hiyo isitokee tena, ili Tanzania
inufaike kwa misaada hiyo ya fedha zinazotokana na walipakodi wa nchi
zao.
Wapinzani wanamlaumu Rais Kikwete kwa kuchelea kumwondoa Profesa
Muhongo baada ya kuahidi mwezi mmoja uliopita kuwa angelifanyia uamuzi
suala lake katika muda wa siku mbili au tatu tangu Desemba 22 mwaka
jana.
Kuna habari kwamba kuchelewa kutangazwa kwa
mabadiliko hayo pengine kunatokana na Rais Kikwete kusubiri ripoti ya
uchunguzi wa kashfa ya Operesheni Tokomeza, ambayo habari zinasema
inaweza kuwasafisha baadhi ya mawaziri na hivyo kumpa mwanya wa
kuwarejesha, hasa kutokana na muda wa uhai wa baraza hilo kuwa mfupi,
hivyo angehitaji watu ambao ameshafanya nao kazi.
Kabla ya kutangaza hatua alizochukua kwa mujibu wa
maazimio ya Bunge, Rais Kikwete alikatisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo
Pinda aliyekuwa Arabuni, kitendo kilichotafsiriwa kuwa alitaka ushauri
kuhusu mawaziri waliohusika na hatua za kuchukua, lakini akatangaza
kumvua uwaziri Profesa Tibaijuka pekee.
Awali, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)
ilipendekeza kuwa Waziri Pinda naye awajibishwe kutokana na kushindwa
kushughulikia suala hilo akiwa mtendaji mkuu wa Serikali.
Aidha, habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema
kuwa Rais Kikwete pia alitaka kutumia fursa hiyo kuwaondoa mawaziri wote
waliotangaza nia ya kugombea urais kutokana na kusakamwa kuwa wanatumia
nafasi zao vibaya, huku wakivunja taratibu za CCM.
Hata hivyo, kutokana na ukweli kuwa Pinda ni
miongoni mwa waliotangaza nia, itakuwa vigumu kwake kumuondoa mtendaji
huyo mkuu kwa kuwa itamaanisha kuvunja Serikali.
Katika sakata la Tegeta Escrow, zaidi ya Sh306
bilioni zilichotwa kwenye akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) ambayo ilifunguliwa kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya IPTL,
ambayo iliingia mkataba wa kuliuzia umeme shirika hilo la umma, baada ya
pande hizo mbili kuingia kwenye mgogoro wa viwango vya tozo na hivyo
kufungua kesi mahakamani.
Kesi hiyo iliisha kwa jaji kuamua kuwa pande hizo
mbili zikokotoe upya viwango vya tozo hiyo, lakini fedha zote
zilizokuwamo kwenye akaunti hiyo zikaondolewa mwishoni mwa mwaka jana na
kulipwa kwa Kampuni ya Pan African Power Solutions (PAP), ambayo
ilinunua hisa zote za umiliki wa IPTL.
Wakati malipo hayo yanafanyika, kulikuwa na
pingamizi la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo ilitaka kodi ambayo
Tanesco ilitakiwa ilipe, ikatwe kwanza kabla ya IPTL kulipwa fedha
zake, huku ikihoji kodi nyingine katika ununuzi wa hisa za kampuni
nyingine iliyomiliki kwa muda hisa za IPTL ya Piperlink ulioonekana
kutawaliwa na udanganyifu.
Tayari Jaji Frederick Werema, aliyekuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameshajiuzulu wadhifa huo, wakati Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi
kupisha uchunguzi. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Wenyeviti watatu wa kamati za Bunge, William
Ngeleja, Andrew Chenge na Victor Mwambalaswa, wamejiuzulu nyadhifa zao,
ikiwa ni sehemu ya maazimio ya Bunge. Pia kuna mlolongo wa viongozi wa
umma, vigogo wa zamani wa Serikali na watumishi wa umma walioingiziwa
fedha na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila ambazo
zinahusishwa na kashfa hiyo au kutotangaza masilahi binafsi katika vikao
vilivyohusu sakata hilo.
Chenge, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ambaye ni Mbunge wa Bariadi, aliingiziwa Sh1.6 bilioni,
Ngeleja, waziri wa zamani wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema
aliingiziwa Sh40.4 milioni, wakati Mwambalaswa ameondolewa kutokana na
kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini wakati huohuo akiwa
mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco iliyotuhumiwa kushindwa kushughulikia
vizuri sakata hilo.
Wakati hayo yakiendelea, Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) imeshawafikisha mahakamani maofisa sita waandamizi wa
TRA, Tanesco na BoT kwa tuhuma za kuhusika kwa njia moja au nyingine
kwenye kashfa hiyo.
Kauli ya wasomi
Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St
Augustine, Dk Charles Kitima alisema: “Nchi lazima iundwe na Serikali
imara na itakayoendeleza mikakati yake ya maendeleo. Tunakwenda katika
uchaguzi hivyo nchi inahitaji Serikali yenye viongozi madhubuti.”
Huku akitolea mfano Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba na Kura ya Maoni kupitisha Katiba Mpya, Dk Kitima alisema mambo
hayo yanahitaji viongozi makini wa kuyasimamia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally
alisema: “Nadhani mabadiliko yanaweza kuwa makubwa kutokana na matukio
yaliyopo mwaka huu. Yanaweza kuwa ni mabadiliko ya kuhakikisha kuwa
Serikali iliyopo madarakani inaendelea kuwapo. Mabadiliko ya kuisaidia
CCM kushinda.”
Aliungana na Dk Kitima, kusisitiza kuwa sakata la
escrow, Uchaguzi Mkuu na Kura ya Maoni ni kati ya mambo yanayoweza
kuchangia kufanyika kwa mabadiliko makubwa. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment