Spika wa Bunge, Anne Makinda (kulia) akiongoza kikao cha Kamati ya
Uongozi kinachojumuisha wenyeviti wote wa Kamati za Bunge kilichokutana
jana kupanga ratiba ya mkutano wa Bunge unaotarajiwa kuanza vikao vyake
Jumanne ijayo. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge.
Danadana zimeendelea juu ya
utekelezaji wa azimio la tatu la Bunge kuhusu kashfa ya Akaunti ya
Tegeta Escrow linaloagiza kuwajibika kwa wenyeviti wa kamati zake tatu
za kudumu, baada ya juzi Spika wa Bunge, Anne Makinda kukaririwa akisema
wameshajiuzulu, lakini wajumbe wake wameibuka jana na kusema
hawatafanya uchaguzi hadi watakapopata maelekezo kutoka Ofisi ya Spika.
Azimio hilo ambalo ni moja ya manane ya Bunge hilo
linasema: “Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na
kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao
wenyeviti tajwa wa kamati husika za kudumu za Bunge.”
Wenyeviti hao na kamati zao katika mabano ni
Victor Mwabalaswa (Nishati na Madini), Andrew Chenge (Bajeti) na William
Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala).
Juzi, Spika Makinda aliwaeleza waandishi wa habari
kwamba wenyeviti waliotakiwa kuvuliwa nyadhifa zao tayari wamejiuzulu
na kamati husika zinatakiwa kufanya uchaguzi kupata wengine wapya. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Hata hivyo, jana, kwa nyakati tofauti Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Jerome Bwanausi na Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Dk Festus Limbu walisema hawatafanya
uchaguzi mpaka pale watakapopata maelekezo kutoka Ofisi ya Spika, huku
wajumbe wa kamati ya Katiba wakieleza hivyohivyo.
Dk Limbu alisema: “Unajua Chenge aliteuliwa na
Spika Makinda kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti. Tunachokisubiri ni
ruhusa ya Spika ili tufanye uchaguzi, kama anateua tena mwenyekiti basi
tunasubiri uteuzi wake.”
Hata hivyo akizungumzia suala hilo la Chenge,
Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilillah alisema: “Chenge aliteuliwa katika
kipindi cha mpito ambacho kikiisha atachaguliwa mwenyekiti mwingine.
Hivyo alisema naye anaweza kuondolewa tu na wajumbe wa kamati.”
Kwa upande wake, Bwanausi alisema: “Hatuwezi
kufanya uchaguzi bila kupata maelekezo kutoka Ofisi ya Spika.
Tulichoamua kamati ni kumwondoa Mwabalaswa katika nafasi yake ya
uenyekiti, ila kama ni uchaguzi bado hatujafanya.”
Jana, kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na
Utawala kiliongozwa na Nyambari Nyangwine badala ya Ngeleja
aliyekiongoza juzi, licha ya kutotakiwa kufanya hivyo kulingana na
maazimio ya Bunge.
Wajumbe wa kamati hiyo waliozungumza walieleza
kuwa Nyangwine aliongoza badala ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Gosbert Blandes ambaye alikwenda kuhudhuria kikao cha Kamati ya Uongozi.
Dk Kashilillah alisema jana kwamba tayari Spika ameshatoa maelekezo na kinachotakiwa kufuatwa na kamati hizo ni utekelezaji tu.
“Kauli ya Spika kwamba wenyeviti wamejiuzulu na
kuzitaka kamati husika kufanya uchaguzi tayari ni maelekezo. Sasa hapo
unataka tuseme kitu gani, labda andikeni kuwa kamati zimekaidi agizo
hilo,” alisema Kashilillah. Tangaza biashara yako hapa kwa bei nafuu zaidi, pia usisahau ku-Like Ukurasa Wetu Wa Facebook Kwa Kubofya/ Click Neno Jambo Tz.
Na Mwananchi
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment