Thursday, November 06, 2014

NUSU YA WANAFUNZI WAFAULU DARASA LA SABA


Wanafunzi wa Shule ya Msingi Peaceland ya mkoani Mwanza wakishangilia baada ya kupata taarifa ya shule yao  kushika nafasi ya tatu kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba wa mwaka 2014 yaliyotangazwa jana. 

Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2014 yakionyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo Septemba mwaka huu, wamefaulu.
Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde yanaonyesha kuwa wasichana wamefanya vizuri zaidi ya wavulana, huku ufaulu kwa jumla ukiwa umeongezeka kwa asilimia 6.38 ikilinganishwa na mwaka 2013.
Katika matokeo hayo Shule ya Twibhoki iliyopo mkoani Mara iliibuka ya kwanza kitaifa kati ya shule 15,867 zilizofanya mtihani huo ikifuatiwa na Mugini, Peacland na Alliance zote za mkoani Mwanza.
Shule ya tano ni Kwema ya Shinyanga ikifuatiwa na St Severine ya Kagera, Rocken Hill ya Shinyanga, Tusiime ya Dar es Salaam, Imani ya Kilimanjaro na iliyoshika nafasi ya 10 ni Palikas ya Shinyanga.
Wakuu wa shule vinara wazungumza
Mkuu wa Shule Twibhoki iliyopo Mugumu - Serengeti, Alphonce Magori alisema siri ya mafanikio hayo ni kila mwalimu kutambua nafasi yake. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Akizungumza ofisini kwake muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo alisema: “Kwanza ni mapenzi ya Mungu na uongozi wa shule kutambua nafasi ya kila mtumishi na wajibu wake na tunapata muda wa kujitathmini kama malengo yanafikiwa,” alisema.
Alisema wanafunzi nao hupata nafasi ya kutoa tathmini ya kile wanachofundishwa na wanapewa mazoezi ya mara kwa mara ambayo husaidia kujua uwezo wao na namna ya kuwasaidia.
Mwaka 2008 na 2010 ilikuwa ya pili kitaifa na tangu mwaka 2007 imekuwa ikiongoza kiwilaya na kimkoa.
Mkurugenzi wa Shule ya Alliance iliyoshika nafasi ya nne, James Bwire alisema baada ya mwaka jana kushika nafasi ya 15 waliweka mikakati. Alisema siri ya mafanikio hayo ni ushirikiano wa wazazi, walimu kujituma, mazingira mazuri ya shule na Ofisi ya Ukaguzi wa Shule Wilaya ya Nyamagana.
Meneja wa Shule ya Peacland ya Ukerewe ambayo mwaka jana ilikuwa ya 23, Halima Salum alisema alitarajia kupata mafanikio hayo kutokana na ufahamu wa wanafunzi waliomaliza mwaka huu.

Mchanganuo
Kati ya watahiniwa 808,085 waliosajiliwa kufanya mtihani huo, walikuwamo wasichana 429,624 sawa na asilimia 53.17 na wavulana 378,461 sawa na asilimia 46.83 lakini watahiniwa 792,118 ndiyo waliofanya mtihani huo.
Kati yao, watahiniwa 451,392 sawa na asilimia 56.99 wamefaulu kwa zaidi ya alama 100 kati ya 250.
Dk Masonde alisema kati ya watahiniwa hao waliofaulu, wasichana ni 226,486 na wavulana 224,909 na wanafunzi wengi wamefanya vibaya zaidi kwenye somo la Hisabati huku wakifanya vizuri kwenye somo la Kiswahili. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Pamoja na kufanya vibaya katika Hisabati, wapo wasichana wanane na wavulana 26 waliopata alama zote 50/50 katika somo hilo.
Watahiniwa 15,963 sawa na asilimia 1.98 hawakufanya mitihani hiyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo utoro na ugonjwa, kati yao wasichana ni 6,999 na wavulana ni 8,964.
Dk Masonde alieleza kuwa mwaka huu udanganyifu kwenye mtihani huo umeshuka kwa kiasi kikubwa na ni mwanafunzi mmoja tu aliyefutiwa matokeo wakati mwaka jana walikuwa 13.
Kuhusu sababu za ongezeko la ufaulu, Dk Msonde alisema Baraza bado halijafanya tathmini ya kubaini chanzo cha ongezeko hilo... “Sisi tulicholetewa ni kile kilichofanyika kwenye chumba cha mtihani na haya hapa ndiyo majibu yake.”

Ufaulu kimasomo
Alisema mwaka huu ufaulu kwa masomo yote umepanda kwa asilimia kati ya 0.64 mpaka 8.94 ikilinganishwa na mwaka jana ambao ufaulu ulipanda kwa asilimia sita mpaka 28.06.
Alisema somo ambalo watahiniwa wengi wamefanya vizuri ni Kiswahili ambalo ufaulu wake umefikia asilimia 69.70 na walilofeli zaidi ni Hisabati ambalo ufaulu wake ni asilimia 37.56.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2013 ufaulu kwenye somo la Kiswahili ulikuwa ni asilimia 69.06 na Hisabati ulikuwa ni asilimia 28.62.
Kwenye somo la Kiingereza ufaulu mwaka huu ni asilimia 38.84 wakati mwaka jana ilikuwa ni asilimia 35.52, huku kwa Sayansi mwaka huu ufaulu ukiwa 54.89 na mwaka jana ilikuwa ni asilimia 47.49. Maarifa ya Jamii mwaka huu ufaulu ni asilimia 57.33 na mwaka jana ulikuwa 53.00

Dk Msonde alisema wanafunzi wote walifanya mtihani kwa kutumia karatasi maalumu za OMR (Optical Mark Reader), ambazo zilisahihishwa kwa kutumia mfumo wa kompyuta.
Matumizi ya teknolojia ya OMR yalianza rasmi kwenye mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2012. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...