Thursday, November 06, 2014

WASOMI, WANASIASA WAPINGA KAULI YA KIKWETE




Rais Jakaya Kikwete. PICHA|MAKTABA 
Makundi mbalimbali ya wasomi, wanaharakati na wanasiasa nchini wamepinga kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kuzuia kampeni za utoaji wa elimu juu ya Katiba Inayopendekezwa wakisema yeye mwenyewe na chama chake ndiyo waliohusika kuanza kampeni mapema hivyo hana haki ya kuzuia makundi mengine.

Juzi, Rais Kikwete alisema muda wa kampeni za ama kuiunga mkono au kuipinga Katiba Inayopendekezwa bado na hakukuwa na sababu ya wanasiasa na taasisi za kiraia kuanza kampeni mapema, lakini wakati huo huo yeye na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wamenukuliwa wakiipigia debe.

Wakati Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama akisema si sahihi kuzuia makundi fulani kutoa elimu hiyo wakati wengine wakiendelea na kampeni za kuipigia debe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema Kikwete ameshindwa kuficha hisia zake kama mwenyekiti wa CCM. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Profesa Mlama alisema iwapo kampeni za mapema zitazuiliwa, basi uamuzi huo utekelezwe na makundi yote bila upendeleo.

“Hatutakuwa fair (hatutatenda haki) kama itazuiliwa kwa makundi mengine. Kama kuzuia basi iwe kwa makundi yote mpaka muda utakapofika,” alisema na kusisitiza, “Lakini binafsi ninadhani hakuna shida yoyote endapo elimu itaendelea kutolewa kwa sasa.”

Dk Slaa alisema: “Ndiyo sababu ya kupendekeza katika utawala ujao lazima tuwe na kiongozi atakayevua kofia moja, kwa sababu athari zinaendelea kuonekana kwa Rais Kikwete na chama chake.”

Alisema mbali na kufanya kampeni za kulazimisha Watanzania wakubaliane na Katiba hiyo, Serikali imefanya ufisadi wa kutumia fedha za umma ili kuendesha kampeni hizo.

“Ni Rais aliyeamua kuvuruga mchakato huo tangu mwanzo na yeye ni mhusika mkuu. Sisi tunachokifanya kwa sasa ni uchambuzi wa Katiba hiyo inayopendekezwa na siyo Kampeni. Kwa hivyo ningependa kuwaomba Watanzania wenye dhamira na Taifa hili wasikubaliane na ushawishi wake wakati ukifika wa kura ya maoni.”

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Sikika, Irenei Kiria alisema pamoja na kauli hizo, Rais hana mamlaka ya kuwalazimisha wananchi wafuate matakwa yake.

Kiria alisema mara kadhaa Rais Kikwete amekuwa akipigia chapuo ili Watanzania wakubaliane na hoja zake bila wao kuhoji jambo lolote.

“Rais Kikwete amekuwa akilazimisha badala ya kuomba wakubaliane naye, jambo ambalo ni hatari katika mchakato huo kwani wananchi wanaweza kuipigia kura ya kuipitisha pasipo kuhoji wakiamini alichokisema juu ya Katiba hiyo ni sahihi,” alisema Kiria. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Katibu Mkuu wa zamani wa NCCR-Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema kuanza kwa vurugu za kampeni mapema ni matokeo ya Rais Kikwete na chama chake kuanzisha kampeni hizo awali.
“Baba anapoanza kuharibu jambo siyo tatizo kwa mtoto anayeendeleza kuharibu utaratibu uliokuwapo. Kukosa uvumilivu ndiyo tatizo lilipoanzia kwa CCM baada ya kuanza uhamasishaji mapema kabla na baada ya Bunge kumalizika,” alisema Ruhuza.
Alisema fedha zilizobainika kuombwa Ikulu ni mwendelezo wa fedha zinazokusanywa na Serikali kwa ajili ya kampeni hizo. “CCM walishaanza kukusanya tangu bajeti ya fedha za Bunge la Katiba kwa hiyo hizi Sh2.5 bilioni ni mwendelezo tu wa ufisadi,” alisema.
Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi ya Siasa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema pamoja na kuanza kwa kampeni hizo kinyume cha sheria, bado itakuwa ni vigumu na si haki kwa makundi ya kijamii kuzuiwa yasiendelee na kampeni za uelimishaji.
Dk Bana alisema makundi yote yamekuwa na shinikizo la kuhakikisha kila upande unafanikisha maazimio yake. Hata hivyo, alisema mambo yanayotofautisha makundi hayo ni vyema yakawekwa wazi ili kuondoa athari ambazo zinaweza kujitokeza hapo baadaye.
“Hawa wanaopinga wanasemaje na wale wanaounga mkono wanasema nini. Kusubiri wakati wa kampeni itakuwa vigumu kwani watu wanataka kuhoji mapema yaliyoondolewa kwenye rasimu ya Jaji Warioba.
“Kwa mfano, hata mimi kuna mambo ya msingi ambayo nilitegemea yangepitishwa na Bunge la Katiba likiwamo suala la mbunge kutokuwa waziri, hivyo ni vyema watu wakaelezwa kwa nini yameondolewa na kwa nini waipitishe au waikatae.”
Hata hivyo, Dk Bana alisema pamoja na shinikizo kubwa lililopo, Rais wa nchi anabakia kuwa na mamlaka ya kutoa kauli ya mwisho juu ya uendeshaji wa mchakato huo hivyo hakuna chombo wala taasisi yoyote inayoweza kutoa kauli ya mwisho katika mchakato huo. Asante kwa kutembelea blog hii na endelea kuwa nasi siku zote, kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...