Mbunge wa Viti
Maalumu (CCM), Ester Bulaya ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge
katika Jimbo la Bunda ambalo linashikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Kwa nia hiyo, Bulaya anaweza kuwa ametangaza vita
dhidi ya Wasira ambaye hivi karibuni akiwa Bunda, alitangaza kukitetea
kiti chake hicho katika Uchaguzi Mkuu 2015.
Julai 8, mwaka huu Wasira akiwa kwenye kikao cha
kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM wilayani Bunda, alitangaza kuwa
atatetea nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao, huku akijigamba kuwa
yeye ni “mwarobaini wa matatizo” yanayowakabili wakazi wa jimbo hilo.
Kabla ya kutangaza nia hiyo, mara kadhaa Wasira
amekuwa akihusishwa na suala la urais na ni mmoja wa makada sita wa CCM
ambao walipewa adhabu na chama hicho Februari 18 mwaka huu, baada ya
kukutwa na makosa ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili jana, Bulaya alisema atagombea ubunge katika Jimbo la Bunda na
anamtakia kila heri mpinzani wake huyo (Wasira) katika nafasi ya juu ya
urais anayotaka kuwania. Alisema ameamua kufanya hivyo baada ya kuombwa
na watu kadhaa kutoka jimboni humo wakiwamo vijana, wazee na kinamama. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Ninaamini nimepata uzoefu mkubwa katika kipindi
hiki cha ubunge wa viti maalumu na ninawataka wabunge wenzangu wa viti
maalumu waone kuwa nafasi hiyo ni fursa ya kujifunza, lakini mwisho wa
yote lazima urudi jimboni,” alisema.
“Hii ni mara ya kwanza nasema hapa. Nitagombea
ubunge Jimbo la Bunda kwa kuwa nimeombwa sana na vijana, wazee na ni
mara nyingi nimekuwa nikisema bado muda, lakini sasa umebaki muda mfupi
hivyo niseme tu kwamba nitagombea. Uongozi ni mbio za kupokezana vijiti.
Wasira ni kama baba yangu na sina ugomvi naye na namtakia kila la heri
katika position (nafasi) yake nyingine anayoitaka,” alisema.
Kuhusu madai kwamba Wasira anafikiria kuwania
urais, alisema, “Naona ni uamuzi sahihi amefanya, kwani amekuwa mbunge
tangu mimi nazaliwa mwaka 1980 ameona kwamba ni kweli hii position
(nafasi) ya chini ameshaitumikia sana, hivyo ameona katika uzoefu
alionao labda ajaribu katika nafasi ya urais.”
Bulaya alisema si kwamba ameamua kugombea ubunge
wa Bunda kwa kuwa Wasira anataka urais, bali viti maalumu alipo hivi
sasa ni njia ya kupata uzoefu na kujifunza katika kuelekea kugombea
ubunge wa jimbo.
“Ili kuondoa suala la kwamba viti maalumu ni vya
kupewa siyo kwamba nasema vifutwe, lakini unaweza ukawekwa utaratibu
mwingine wa kumpa mwanamke uzoefu katika ngazi ya kibunge,” alisema na
kuongeza;
“Lakini unapopewa hebu itendee haki hiyo fursa,
kama mtu umeingia viti maalumu unajifunza na unakwenda kugombea na huko
kuna kushinda na kushindwa lakini ni lazima nionyeshe hii fursa nimepewa
naweza kwenda kushindana na wanaume.”
Alisema hilo ni jambo la msingi kwa kuwa huwezi
kulemaa kwa kuwa mbunge wa viti maalumu bila kujifunza na kukaa miaka
hadi 15 kwenye ubunge wa aina hiyohiyo kwani wako wengine wanaotakiwa
kupata nafasi hiyo ili wajifunze na kwenda majimboni.
“Katika kushindana kuna mawili na lazima ujiandae kwa yote
ingawa mwisho wa siku wananchi ndiyo wanaona huyu ana uwezo, tumempa
dhamana ya viti maalumu ameitendea haki nafasi hiyo,” alisema.
Uamuzi mbovu
Alipoulizwa ni jambo gani lililowahi kumkera
alilofanya yeye au chama chake katika kipindi cha ubunge wake, Bulaya
alitaja mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyowaondoa waliokuwa
mawaziri; Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Shamsi Vuai Nahodha
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani)
na Dk Mathayo David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) akisema huo
ni uamuzi wa kujutia. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Ninajutia ‘party caucus’ iliyowaondoa mawaziri
kutokana na Operesheni Tokomeza Ujangili, kwani waliotakiwa kuwajibika
ni watendaji na si mawaziri wale. Naamini hao walitolewa kafara kwa
sababu.
Naamini waliopaswa kushughulikiwa walikuwa watendaji na siyo mawaziri,” alisema.
Alisema aliumia kwa kuwa haiwezekani watendaji
wafanye makosa halafu wanaendelea kubaki lakini mawaziri wachapakazi
wakaondolewa na kwamba hilo lisiporekebishwa, wataendelea kutolewa
kafara na mawaziri ambao ni wachapakazi... “Haya mabadiliko
hayakunifurahisha kwa kweli.”
Mbio za urais
Alipotakiwa kutoa maoni yake juu ya wanaojitokeza
kuwania urais, Bulaya haoni kati yao mwenye sifa ya kuwania nafasi hiyo
ya juu ya uongozi.
Ingawa hakutaja jina la mtu, Februari 18 mwaka
jana 2013, Kamati Kuu ya CCM iliwafungia makada sita wa CCM, ambao ni
Bernard Membe, Frederick Sumaye, Edward Lowassa, Stephen Wasira, January
Makamba na William Ngeleja baada ya kuwabaini kuwa walikuwa wameanza
kampeni za urais kabla ya wakati.
Tamko la Kamati Kuu ya CCM lilisema: “Waliohojiwa
wamethibitika kuwa na makosa yafuatayo: Kuanza kampeni za kutafuta
kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na
maadili za CCM Toleo la Februari 2010 Ibara 6 (7), kufanya vitendo
vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo
vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. Kosa hilo nalo ni kwa mujibu wa
Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010 Ibara kadhaa
za kanuni hizo.”
Bulaya alisema, “Kutaka urais ni jambo moja na
kuchaguliwa na ni jambo jingine. Itafika muda Watanzania watasema nani
anafaa, lakini mimi naamini kuna makada wengi wenye sifa kuliko hao,
ambao hawajajitokeza na pengine hawatajitokeza kabisa. Katika nafasi ya
urais hatuhitaji watu ambao Mwalimu Nyerere aliwakataa kwa kuwa ni wala
rushwa na wanaotumia madaraka vibaya. Katika mchakato huo wa Katiba
kumejitokeza maoni ya watu kwamba huyo anafaa na yule hafai. Lakini
kikubwa ni kuangalia watu wenye hulka ya Mwalimu Nyerere.”
Na Mwananchi
“Kimsingi mimi nakereka sana ninaposikia watu wakihusisha urais
na umri. Umri hauwezi kuwa sifa ya urais. Rais anapaswa kuwa mtu
anayejua changamoto na udhaifu wa uongozi uliopita, ajue tatizo la
Taifa, achukie matumizi mabaya ya madaraka na aguswe na umaskini wa
Watanzania.
“Sifa nyingine ni mtu kuwa na uwezo wa kuondoa
tabaka la matajiri na maskini, kuheshimu misingi ya utawala bora na
akatae rushwa kwa vitendo.”
Alipoulizwa kama anaona upinzani una fursa katika
nafasi hiyo ya juu serikalini, Bulaya alisema, “Naamini CCM bado ina
fursa nzuri, ila isibweteke kwa kuwa Watanzania wa leo siyo wajinga.”
Alisema CCM haipaswi kuudharau upinzani, badala
yake ishughulikie changamoto zinazotolewa na upande huo wa pili kwa
ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania ili iendelee kuaminika. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment