Chama Cha Mapinduzi
kimeonyesha wasiwasi kuhusu matumizi ya teknolojia ya kielektroniki
katika uandikishaji wa wapigakura na mashine za ukusanyaji wa kodi
(EFD).
Wasiwasi huo umeelezewa kwa nyakati tofauti na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na
Uenezi, Nape Nnauye wakati wakihutubia mkutano wa hadhara katika Mji
Mdogo wa Chalinze, wilayani Bagamoyo juzi.
Kinana alihoji utaratibu aliouita mbovu katika
matumizi ya mashine za kielektroniki za kutunza hesabu za
wafanyabiashara (EFD) na Nnauye alieleza wasiwasi wake kuhusu uamuzi wa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kutumia teknolojia ya Biometric Voter
Registration (BVR) katika kuandikisha upya wapigakura.
Nnauye aliishauri Nec kuangalia upya uamuzi wake
huo akisema hauna mantiki kwa kuwa utaliingizia Taifa gharama ambazo
zinaweza kuepukwa kwa urahisi.
Teknolojia hiyo iliwahi kulalamikiwa bungeni na
Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika hotuba yake ya bajeti
mwaka jana, akisema NEC imeanzisha utaratibu huo bila kuwashirikisha
wadau.
Akitoa mifano, Nnauye alisema matumizi ya
teknolojia hiyo yalizua mtafaruku katika chaguzi za nchi za Kenya,
Malawi na Ghana na haitakuwa busara Tanzania nayo kujiingiza kwenye
matatizo kama hayo wakati ina uwezo wa kuyaepuka. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
“Tatizo ni kuwa Tume (Nec) inataka kuandikisha
wapigakura upya kwa kuchukua taarifa zao za kibaiolojia wakati taarifa
kama hizo tayari zimeshachukuliwa na taasisi nyingine. Litakuwa jambo
rahisi na lisilo na gharama kubwa kwa Tume kukaa na taasisi hizo na
kuchukua taarifa hizo na kuziingiza katika majina ya wapigakura ambao
tayari wameshaandikishwa. “Ikishafanya hivyo, Tume itabakiwa na kazi
moja tu ya kuandikisha wapigakura wapya ambao bado hawajaandikishwa na
idadi yao inakadiriwa kuwa kama milioni tatu hivi,” alisema Nnauye.
Alizitaja taasisi ambazo zinachukua alama za
vidole wakati wa kutoa vitambulisho kuwa ni Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (Nida), Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) na Idara ya Uhamiaji.
“Kama NEC wanataka kupata alama za vidole za
wapigakura ni jambo rahisi la kukaa na mamlaka hizi na kupata taarifa
hizo... tusipoangalia Tanzania inaweza kuweka rekodi ya kuwa nchi ya
kwanza barani Afrika kuwa na taasisi nyingi zinazochukua wananchi wake
alama za vidole,” alisema.
Alisema wakati Serikali ikitenga Sh7 bilioni tu
katika bajeti yake ya mwaka huu kwa ajili ya uandikishaji wa wapigakura,
Nec ilikuwa imeomba takriban Sh200 bilioni kwa ajili ya kazi hiyo.
Hata hivyo, juzi Mwenyekiti NEC, Jaji Damian
Lubuva alisema tayari Tume hiyo imepokea Sh290 bilioni kutoka serikalini
kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo na gharama nyingine za mchakato wa
uboreshaji daftari la wapigakura.
Nape alisema CCM imeamua kutoa hadhari na ushauri
huo kwa sababu ipo hatari iwapo uchaguzi utavurugika kutokana na Tume
kung’ang’ania matumizi ya teknolojia hiyo, wapinzani wanaweza
kukinyooshea kidole chama hicho na kukituhumu kuwa kimehujumu.
Na Mwananchi
Matumizi ya EFD
Kinana alihoji utekelezaji wa matumizi ya mashine za EFD na kubainisha kuwa una kasoro nyingi.
Alisema hana matatizo na uamuzi wa kutumia mashine hizo, bali utaratibu uliotumika katika kuanzisha matumizi yake.
“Naomba waandishi wa habari mnielewe vizuri katika
hili. Sina matatizo na uamuzi wa kutumia hizi mashine, lakini utaratibu
unaotumika kuzitumia ndiyo una matatizo na hilo si sawa,” alisema.
Alisema baadhi ya malalamiko ya wafanyabiashara ni ya msingi na yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi.
Aligusia suala la bei za mashine hizo kama moja ya
matatizo yaliyojitokeza... “Zilipoingizwa kwa mara ya kwanza
wafanyabiashara wakauziwa kwa Sh4 milioni. Wakalalamika bei ikapungua
hadi Sh2 milioni, walipolalamika tena ikashuka zaidi hadi Sh800,000
wakazidi kulalamika bei ikashuka hadi Sh600,000. Sasa mtu unajiuliza
hivi bei halisi ya mashine hizi ni ipi?”
Kinana alihoji, wakati TRA inawataka
wafanyabiashara kuzinunua mashine hizo kwa fedha zao kurudishwa kidogo
kidogo kama makato pungufu katika kodi wanazolipa, mfanyabiashara
akifilisika kabla fedha alizotumia kununulia hazijarejeshwa zote ni nani
atamfidia?
Alisisitiza kuwa kuna upungufu katika sheria
inayohusu matumizi ya mashine hizo na wafanyabiashara wanaopinga
wasionekane ni wakorofi... “Watu wakibisha wanaambiwa wanavunja sheria
wakati sheria yenyewe imepinda.”
Serikali ilianzisha matumizi ya EFD kama moja ya
mikakati ya kupanua wigo wa walipakodi ili kuongeza mapato yake na
kuongeza uwezo wa kugharimia matumizi yake kwa fedha za ndani.
Inakadiriwa kuwa watu wanaolipa kodi nchini milioni mbili kati ya
milioni 15 wanaostahili. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz
Na Mwananchi
No comments:
Post a Comment