Wednesday, September 24, 2014

BUNGE LA KATIBA KUTUMA OFISA SAUDIA KUSIMAMIA KURA




Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, Andrew Chenge akionyesha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kabla ya kumkabidhi Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, mjini Dodoma jana. Rasimu hiyo inatarajiwa kuwasilishwa bungeni leo. 


Ofisi ya Bunge la Katiba itamtuma ofisa wake kwenda Makka, Saudi Arabia kusimamia upigaji kura kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa wajumbe wa Bunge hilo wanaokwenda Hijja.

Hayo yalielezwa jana na Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad alipotakiwa kueleza idadi kamili ya wajumbe wa Bunge hilo wanaotarajiwa kuwa nje ya nchi na jinsi watakavyopiga kura.

Juzi, Bunge hilo lilizifanyia marekebisho kanuni zake ili kuwaruhusu wajumbe watakaokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge wakiwamo wanaokwenda Hijja kuipigia kura Katiba inayopendekezwa, iliyokabidhiwa kwa Kamati ya Uongozi jana.

Chini ya marekebisho hayo, mjumbe aliye nje ya Bunge, ataruhusiwa kupiga kura ya wazi au ya siri kwa njia ya fax au mtandao kama itakavyoelekezwa na katibu kwa kushauriana na mwenyekiti.

Hamad alisema hadi kufikia jana mchana walikuwa wamewatambua wajumbe wanane ambao watakwenda Hijja huko Uarabuni lakini orodha ya watakaokuwa nchi nyingine bado haijajulikana.

Hamadi alisema ofisa wake huyo atasimamia kura za wajumbe wanaokwenda Hijja katika upigaji kura unaotarajiwa kuanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 mwaka huu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Alisema ni vigumu kutaja vituo watakavyopigia kura sasa kwa sababu bado hawajawauliza wajumbe wengine waliopo nje ya nchi ambao wangependa kupiga kura wakiwa huko.

Kuhusu iwapo watapiga moja kwa moja kwa mtandao au watapiga kwenye karatasi na kutoa vivuli, Hamad alisema suala hilo litaamuliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge chini ya Mwenyekiti, Samuel Sitta.

Ukawa wapinga

Wenyeviti wenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia wamelishukia Bunge hilo kwa kuruhusu upigaji kura nje ya nchi.

Akizungumza jana, Profesa Lipumba alisema kilichofanywa na Sitta na wajumbe wake ni uchakachuaji unaoweza kuliingiza Taifa kwenye mgogoro mkubwa.

“Kwanza taratibu za kura mabunge ya Jumuiya ya Madola ni kura zote zinapigwa ndani ya Bunge. Unapozungumzia akidi imetimia ni wajumbe walioko ndani ya Bunge,” alisema Profesa Lipumba.
Kanuni mpya ya 30 (1) baada ya marekebisho yaliyofanyika juzi inasomeka, “Akidi kwa kila kikao cha Bunge Maalumu itakuwa ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu.”
Awali, kanuni hiyo iliweka sharti la lazima kwamba akidi ya kikao itakuwa ni nusu ya wajumbe, isipokuwa kwa kikao kinachohusu kupitisha uamuzi wa Bunge Maalumu.
“Mwenyekiti hawezi tu kutangaza kuwa akidi imetimia kwa sababu nimepata barua kuna wajumbe wako nje kwa hiyo watapigia kura huko. Ni uvunjifu wa sheria na taratibu ulio wazi,” alisisitiza.
“Hakuna maridhiano lakini zaidi ya hapo huu mchakato wote umeshaharibika. Kinachofanyika hapo ni Sitta kujaribu kuhalalisha matumizi ya Sh20 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Bunge hilo,” alisema.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, alisema kinachofanywa na Sitta ni kuhakikisha wanatoka na Katiba hata kama haina uhalali wa kisiasa.
“Kwa hiyo inabidi lazima atoke na kitu ili aseme tumepitisha uamuzi tumetoka na Katiba hii ili kuhalalisha matumizi,” alisema Lipumba na kuhoji uharaka huo wa Sitta ni wa nini?
“Kama muda hautoshi kwenda kwenye kura ya maoni kulikuwa na sababu gani ya kuendelea na mchakato huo. Mchakato wa Katiba unakwenda katika utaratibu wa sheria,” alisema.
Profesa Lipumba alisema sheria iko wazi na iliweka utaratibu kuwa baada ya kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, isipite siku zaidi ya 120 bila kura ya maoni kufanyika.
“Ni wazi sheria yenyewe itabidi ibadilishwe. Rais atakayekuja akiwa makini hawezi kukubali kuanza na Katiba iliyowagawa Watanzania. Rais gani atakubali kuanza na migogoro ya kisiasa?” alihoji Lipumba.
“Waziri wa Katiba wa SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) hashiriki, AG (Mwanasheria Mkuu) wa Zanzibar hashiriki Katiba ya nchi, watu wa Zanzibar hawashiriki utasemaje ina uhalali wa kisiasa?”
Mbatia alisema anamshangaa Sitta kujigamba kutoka na Katiba inayopendekezwa wakati itakwenda kukaa kabatini kusubiri utashi wa rais ajaye.
“Hatuna kura ya maoni kwa hiyo haiwezi kutumika. Kwa hiyo ikishapokewa inawekwa kabatini. Rais ajaye ni mwingine, sisi tunaendelea na mikakati yetu ya marekebisho ya 15 ya Katiba,” alisema.
Kuahirishwa kwa kura ya maoni kunatokana na makubaliano kati ya viongozi wa Taasisi ya Demokrasia Tanzania (TCD) na Rais Jakaya Kikwete yaliyofikiwa Septemba 8, mwaka huu. Kuwa wa kwanza kupata habari zetu kwa ku-Like page yetu ya facebook kwa ku-click/ bofya neno Jambo Tz

Na Mwananchi

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...