Sina
mpango wa kujitoa kwenye Tume kwa kuwa nimekula kiapo kwa ajili ya
Watanzania, hadi sasa sijaona sababu ya kutaka kujitoa, alisema Profesa
Baregu.
Dar es Salaam. Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshindwa kutoa kauli kuhusu
kujitoa kwake kwenye mchakato wa Katiba Mpya baada ya muda kilioutoa kwa
Serikali kutaka kurekebishwa kwa baadhi ya mambo katika mchakato huo
kumalizika juzi.
Mwenyekiti
wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
alisema bungeni Aprili 11, mwaka huu kuwa chama chake kitajitoa katika
mchakato huo endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi hadi
kufikia Aprili 30, mwaka huu.
Hata
hivyo, hivi karibuni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba alisema tume haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la
wanasiasa na kwamba itafuata mwongozo uliopo ambao utaisaidia nchi
kupata Katiba ya Watanzania.
Kauli
hiyo imepingwa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ambaye
amemtaka aanze kukikanya CCM akidai kuwa kimepanga mkakati wa
kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya yenye masilahi kwa chama hicho.
“Tuna
ushahidi jinsi CCM inavyoshiriki kuharibu mchakato wa Katiba na sasa
tunajipanga kufanya vikao vyetu vya ndani, baadaye tutatoa tamko zito
tukieleza jinsi hawa watu wanavyofanya mchezo wao,” alisema Dk Slaa.
Kuhusu
ahadi ya kujitoa katika mchakato wa Katiba Aprili 30, alisema Mbowe
alitoa kauli bungeni kutokana na vikao vya nyuma vya chama hivyo kauli
nyingine itatolewa baada ya vikao vingine.
“Tutakaa
na kuamua nini cha kufanya kwa kuwa tayari ‘deadline’ (muda wa mwisho),
yetu imeshafika na kauli ya Warioba tumeshaisikia na hawajafanya
tuliyoyataka hivyo tutakaa na kutoa uamuzi mwingine,” alisema Dk Slaa.
Hata
hivyo, taarifa zinaeleza kuwa tayari chama hicho kimeshafanya uamuzi wa
kujitoa katika mchakato huo baada ya madai yao kushindwa kutimizwa na
kimemtaka Mjumbe wake wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu ajitoe
kwenye Tume.
Akizungumzia
hilo, Dk Slaa alisema hawezi kuzungumzia masuala ya kujitoa kwa Profesa
Baregu... “Mimi nazungumzia masuala ya chama.”
Alipoulizwa
kuhusu uamuzi huo, Profesa Baregu alikiri kuelezwa kwa mdomo kuwa chama
kimefikia uamuzi huo lakini akasema hautakisaidia chama wala nchi hivyo
akashauri Kamati Kuu irejee upya uamuzi wake.
“Sielewi
mpaka sasa kwa nini Chadema inajitoa wakati imekuwa ikipambana
kupatikana kwa Katiba Mpya. Mimi niko kwenye Tume na sijaona tatizo
linalozungumziwa,” alisema Profesa Baregu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment