Thursday, May 02, 2013

Sendeka, Shelukindo wamtetea Kinana

Tuhuma dhidi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman  Kinana, (pichani) kuhusika katika usafirishaji wa pembe za ndovu, zimewalazimisha wabunge kadhaa wa  CCM kumsafisha.

Hali hiyo ilijitokeza juzi jioni wakati wakichangia hotuba hiyo ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Tuhuma hizo zilitolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mchungaji Peter Msingwa (Chadema), kuituhumu kampuni ya Sharaf Shipping Agency inayomilikiwa na Kinana kukamatwa na pembe za ndovu nchini China.

Mbunge wa Simanjaro , Christopher  Ole Sendeka (CCM), alimtetea Kinana kuwa kampuni yake haihusiki katika sakata la pembe za ndovu.

“Hii ni ‘Allergy’ ya jina la Katibu Mkuu (Kinana). Suala la pembe za ndovu lilikuwa ni mwaka 2009, watuhumiwa wake ni wale wote mliosikia Dk. Nchimbi (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), wako saba…na wote hawatoki katika kampuni inayomilikiwa na Kinana,” alisema na kuongeza:

“Kampuni inayomilikiwa na Kinana baada ya ripoti ya Interpol iliyopelekwa DDP (Mkurugenzi wa Mashitaka) kufungua mashtaka ilimaliza utata kuwa kampuni inayomilikiwa na Kinana ilihusika.”

Alieleza kushangazwa kuwa pamoja na mambo hayo bado kambi ya upinzani bungeni inageuza makosa ya kampuni yanaweza kuwa makosa ya mmliki.

“Ni kama leo unakwenda katika ukumbi wa Bilicanas, unakwenda chooni na kumkuta mvulana anavuta bangi, huwezi kumshtaki Mbowe (Mbunge wa Hai-Chadema), unashughulika na muhalifu,”alisema.

Alisema pia suala hilo limeingia katika familia za waasisi wa Taifa ambapo alisema kitendo cha familia hizo kumiliki vitalu vya uwindaji siyo kosa.  Alihoji iweje kambi ya upinzani kwenye orodha ya kampuni za utalii wasiwataje wamiliki wa upande wao kama Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya-Chadema,  (binti wa Mbunge wa Moshi Mjini, Philimon Ndesamburo).

Aliwataka kwenda katika majukwaa ya kisiasa na kukanusha yale yote aliyosema dhidi ya Kinana wakati akiwa kwenye mkutano wa hadhara.

Hata hivyo, alisema  haimaanishi kuwa hatambui kazi nzuri ambazo zimefanywa na kambi ya upinzani katika hotuba yao ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Alisema miongoni mwa mambo anayoyatambua ni mgogoro wa Loliondo na Ngorongoro. Sendeka alisema mambo yaliyosemwa katika hotuba hiyo ya kambi ya upinzani kuhusiana na migogoro hiyo ni ya kweli.

“Wananchi wa Ngorongoro wana matatizo ya msingi, hawamiliki ardhi,  hawajaliwi, ukiacha fedha wanayotengewa na mamlaka ni kidogo,” alisema.  Hata hivyo, alisema tume iliyoundwa na chama hicho, imetoa mapendekezo mazuri ya kuhakikisha kuwa maslahi ya wananchi wa Loliondo yanapewa kipaumbele.

Mbunge wa Kilindi, Beatrece Shelukindo, (CCM), alisema  hadhani kama Kinana asingekuwa katibu mkuu wa CCM, jina lake lingetajwa ndani ya Bunge.

“Niwaombe Watanzania mnaosikiliza hapa ndani, hatuji kwa ajili ya kushindana kwa sababu ya vyama vyetu, tuna majukwaa ya kisiasa nje ya Bunge, huko nje ni sahihi, lakini hapa tunaongelea maslahi ya wananchi,” alisema na kuongeza:

“Mambo ya kuongelea vyama kutaja majina ya vyama kwa kweli napata uchungu sana, mimi naomba kwa muda mfupi tulionao twende na hoja.”
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Pro

PropellerAds

LinkWithin

Soma na Hizi Pia Plugin for WordPress, Blogger...