MIPANGO
endelevu inapaswa kufuatwa na kila mwanadamu, katika familia zetu za
Kiafrika mara nyingi tunaanguka katika suala la mipango mikakati ya muda
mrefu. Mwanadamu akifariki, mara nyingi wanaoachwa kuendeleza kazi za
marehemu wanaishia kusuasua na kutofikia malengo.
Yapata
mwaka mmoja tangu, aliyekuwa legend wa simema za Kibongo, Steven
Kanumba ‘The Great’ afariki dunia na kuiacha Kampuni yake ya Kanumba The
Great Film ikiendeleza shughuli zake za kuzalisha filamu kama kawaida.
Kampuni
aliyoiacha pale Sinza-Mori, jijini Dar ilibaki chini ya mikono ya
wafanyakazi wake wakiongozwa na mdogo wa marehemu, Seth Bosco, mpiga
picha za video, Zakayo Magulu pamoja na Mayasa Mrisho ‘Maya’ ambaye
alikuwa akifanya kazi kama msimamizi wa ‘location’ (location manager) na
masuala ya makeup.
Kadiri
siku zilivyozidi kusonga, umoja kati yao ulianza kupungua. Kila mmoja
anaonekana kuhangaika kivyake licha ya kwamba kampuni bado ipo. Mikakati
ya jumla ikawa haijadiliwi, kila mmoja akawa anaangalia namna ya
kujikwamua kivyake.
Mara
kadhaa nimekuwa nikizungumza na baadhi ya wasanii waliokuwa tegemezi
katika kampuni hiyo, wamekuwa wakiniambia wapo bize kufanya kazi zao
binafsi nje ya Kanumba The Great Film. Hiyo inaonesha dalili kwamba kazi
za umoja zimeanza kulegalega.
Miongoni
mwa bidhaa zilizokuwepo katika ofisi hiyo ni pamoja na DVD za marehemu
alizokuwa akiziuza lakini baada ya kifo chake, ofisi hiyo imepoteza
mvuto wa kibiashara na hata mpangilio kwa jumla. Hakuna mtu wa kukemea
au kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.
Kabla
Kanumba hajapatwa na mauti, alikuwa mpiganaji. Alipambana kuhakikisha
anafikia malengo yake. Lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha tasnia ya
filamu inafika levo za Kimataifa.
Enzi
za uhai wake, Kanumba ndiye aliyeanza kuthubutu kutoboa mianya ya
kuwashirikisha wasanii wa Nigeria. Alifanikiwa kucheza simema ya Dar 2
Lagos na filamu nyingine kadhaa kwa kuwashirikisha wasanii mbalimbali wa
nje ya Tanzania.
...Akiwa kazini enzi za uhai wake.
Kama
hiyo haitoshi, mwaka 2011 marehemu alizidi kujitanua zaidi katika soko
la Nollywood kwa kumchukua mwigizaji mkubwa nchini Nigeria, Ramsey Noah
na kufanya naye filamu ya Devil King Dom ambayo kwa kiasi kikubwa
imeleta mapinduzi makubwa katika gemu.
Kuonesha
anapenda maendeleo, Kanumba hakuishia hapo kwani mwaka huohuo alipiga
hatua nyingine kubwa katika sanaa baada ya kufanikiwa kwenda New York,
Marekani na kununua vifaa vya kisasa vya kuzalishia filamu.
Mpaka
mauti yanamkuta Aprili 7, mwaka jana tayari alikuwa ameshajiwekea
misingi mizuri katika sanaa kwani alikuwa anamiliki kampuni yenye vifaa
vya kisasa pamoja na kutoa ajira ya wafanyakazi wasiopungua kumi.
Marehemu
alijiwekea mikataba na Kampuni ya Steps Entertainment kuzalisha filamu 6
kwa mwaka. Hilo alifanikiwa kwa kiasi kikubwa, tena aliweza kuigiza na
filamu nyingine za kushirikishwa mbali na zile za Steps.
Hadi
kufikia Aprili 7, mwaka huu marehemu alikuwa akitimiza mwaka mmoja
kaburini. Mdogo wake, Seth Bosco ambaye amejitoa kuendeleza kampuni
hiyo, amefanikiwa kuingiza sokoni filamu tatu tu.
...Akiwa katika pozi.
Mbaya
zaidi mbili kati ya hizo (Love and Power na Ndoa Yangu) zilisharekodiwa
na marehemu, wao wakazikamilisha kwa kuzifanyia ‘editing’. Yeye kama
yeye alifanikiwa kuingiza filamu moja sokoni ya Malaika.
Kwa
mwendo huo utagundua spidi aliyoiacha marehemu imepungua, filamu
walizoingiza ni chache sana. Kifupi wanasuasua kama si kupoteza
muelekeo. Kwa mfumo aliokuwa akienda nao marehemu, mwaka mmoja baada ya
kifo hadi sasa, kampuni ilipaswa kuzalisha filamu sita au zaidi.
Kuna kitu cha kujifunza katika mfumo ambao aliuacha marehemu. Walioachiwa kampuni wakiongozwa na Seth wanapaswa kujitazama upya.
...Akiandaa filamu ya Devil's Kingdom aliyocheza na Ramsey (kulia).
Hii
ni changamoto ngumu inayohitaji akili ya ziada kuweza kuvuka, katika
hali kama hiyo hakuhitaji masihara wala utani hata kidogo. Hapo ndipo
watu wanapotafutana uchawi. Wenye mamlaka ya kuiendesha kampuni kwa
namna moja au nyingine wanapaswa kuwa wakali kidogo ili mambo yaende.
Kujituma
kwa marehemu ndiyo kulisababisha ashinde tuzo mbalimbali za filamu
zikiwemo zile za Zanzibar Film Festival (Ziff). Ingependeza basi heshima
ile aliyoiacha marehemu ikaenziwa kwa kuvuka mipaka, ikiwezekana zaidi
ya pale alipokuwa akipapigia mahesabu yeye enzi za uhai wake.
Naamini inawezekana kama wahusika wataweka nia.
No comments:
Post a Comment