NCHI ya Uruguay yenye raia takribani
milioni 4, inatajwa kuwa na bahati ya kuwa na Rais asiye na chembe ya
tamaa. Hana makuu, kiasi kwamba anatajwa kuwa ndiye Rais masikini zaidi
kuwahi kutokea duniani.
Huyu si mwingine, bali ni Jose Mujica,
Rais wa sasa wa Uruguay ambaye pia ni Rais wa 40 wa nchi hiyo. Tangu
aingie madarakani Machi mosi mwaka 2010, amekuwa akionekana kuwa
kiongozi wa tofauti kabisa, tofauti na waliomtangulia.
Mathalan, baada ya kufanikiwa kuishika
nchini, hakuwa na tamaa ya kukimbilia Ikulu, yeye alichokifanya ni
kuamua kuishi katika makazi yake yaleyale, katika nyumba ya mkewe
iliyoko shambani, nje ya Jiji la Montevideo.
Kwa ujumla, anapenda maisha ya kawaida, maisha ya kuwahurumia wengine na kujitahidi kuonesha kwa vitendo.
Ni vigumu kuamini, licha ya kuwa ni Rais
wa nchi, amejishusha mno kiasi cha mara kadhaa kuonekana akijichanganya
na raia wake katika shughuli za ujenzi wa taifa, ikiwamo ujenzi wa
barabara, kulima mashamba ya mfano.
Na wakati mwingine, anapougua huwahi kupanga mstari ili kuonana na daktari, akichelewa anapanga mstari kusubiri zamu yake.
Ni Rais pekee ambaye ameamua kutoa
mshahara wake kwa zaidi ya asilima 90 kugawana na watu masikini wa nchi
yake, kwamba fedha hizo huingizwa katika vikundi mbalimbali vya
maendeleo.
Akiwa amepangiwa na Bunge kupokea dola
za Kimarekani 11,000 (sh milioni 17.6 kwa fedha za Tanzania) kwa mwezi,
hajawahi kupokea fedha hizo na ameiamuru Hazina kuzipeleka fedha hizo
kwa wananchi masikini.
Yeye hupokea shilingi milioni 3 tu, tena
hizi akizitumia kwa ajili ya mafuta ya gari lake alilonunua na mkewe
aina ya Volkswagon Beetle maarufu kama `Mgongo wa Chura’. Gari hilo
lenye umri wa miaka 23, ndio utajiri pekee anaojivunia.
Hana kingine anachokimiliki. Hana
akaunti benki, hana nyumba yake binafsi, wala mali nyingine ya aina
yoyote aliyojilimbikizia. Kuhusiana na gari lake lenye thamani ya dola
za Kimarekani 1,900 (Sh milioni 3), ambalo analiendesha mwenyewe,
anasema:
“Niko mimi na mke wangu, wawili tu, gari
kubwa la nini, sina haja nalo, sitaki kuwaibia wananchi, kunichagua tu
kuwaongoza ni sifa pekee, tena kubwa inayokaribia utukufu wa kawaida,
sasa zaidi ya hapo nini…
“Nahitaji sana kuwatumikia wananchi wa
Uruguay, sio kuwanyonya wala kuwaibia au kuwa mwanya wa kuchuma na
kujifurahisha mimi, mke wangu, watoto wangu na ndugu zangu, sioni haja
hiyo na sitaki kuwa mnyonyaji kamwe,” anasema Rais Mujica. Anasisitiza
anayafurahia maisha ya kawaida, hivyo haoni shida kuishi na watu wa
kawaida mtaani kwake, kupiga nao porojo na hata kushirikiana katika
shughuli za kijamii pale inapolazimu.
“Nikiwa na akaunti benki, nikiwa na
magari makubwa, nitakuwa nakaribisha ushawishi wa kuwa mwizi, kuwaibia
wananchi wangu, sitaki chochote,” anaongeza Rais huyo ambaye hata
anapoamua kunyoa nywele zake, hahitaji kinyozi maalumu, bali yeyote
anayejua kunyoa anamwita nyumbani kwake aweze kumnyoa.
Staili ya maisha ya Rais huyo inaonekana
pia kumwingia mkewe ambaye pia tofauti na wake wengine wa marais, yeye
hajipambi kwa dhahabu, almasi wala aina nyingine ya vito vya thamani.
Anashirikiana na mumewe katika shamba
lao la maua katika makazi yao, huku Rais Mujica wakati mwingine akifanya
usafi wa nyumba na hata kumwagilia maua. Hayo ndiyo maisha ya Jose
Mujica, Rais wa 40 wa Uruguay ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 77,
lakini licha ya kupigania mno kuingia Ikulu, ameonesha kutokuwa na kiu
ya utajiri, hataki kujikweza na wala kuonekana ni tofauti na watu
wengine.
Ndiyo maana ameonekana kuwa Rais wa
ajabu, akitajwa pengine kuwa ndiye asiye na makuu na masikini kuliko
wote duniani. Hata vaa yake ni ya kawaida, mara nyingi akiingia ofisini
na mavazi ya kawaida, lakini mara moja moja tu, akivalia suti na tai
hasa anapokuwa na ugeni mzito.
Angalau Makamu wake, Danilo Astori
anaonekana na `ufisadi’ kidogo, kwani ana nyumba yenye thamani ya dola
250,000 (Sh milioni 400) na gari kama la milioni 30 hivi. Je, kuna
wengine wenye staili ya maisha ya Rais Mujica? Yawezekana, lakini kwa
sasa imeonekana hakuna kama Mujica.
Na Habari Leo
Na Habari Leo
No comments:
Post a Comment